Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Haki za wachache wa kidini

Kutoka wikishia

Haki za wachache wa kidini: Haki za wachache wa kidini ni mjumuisho wa uhuru na haki stahiki wanazopaswa kupewa wasio Waislamu katika jamii ya Kiislamu, ikiwemo uhuru wa kuabudu na uraia. Wanahistoria wanaeleza kuwa tangu awali, Uislamu ulitambua haki hizi kupitia 'Mkataba wa Kodi ya Dhimma', ambao ni mkataba wa kuwalinda wasio Waislamu wanosishi ndani ya himaya za Uislamu kwa dhamana maalumu. Kwa mujibu wa wanazuoni wa Kishia, serikali ya Kiislamu hutoa ulinzi, msamaha wa vita, uhuru wa ibada, haki za kiuchumi na mahakama adilifu kwa jamii hizi kama mbadala wa malipo ya kodi ya jizya wanayotoa na kuipa serikali ya Kiislamu. Kadhalika, watafiti wa Kisunni wanasema kwamba, mafakihi wa madhehebu yao nao wametambua haki hizo kwa msingi wa sheria na mkataba huo huo wa Dhimma. Kiuchambuzi, kumbukumbu za kihistoria zinaonesha wazi kuwa serikali za Kiislamu zilitekeleza kivitendo haki za walio wachache, ijapokuwa palikuwepo na changamoto za kiutendaji na ukiukwaji wa sheria uliojitokeza katika baadhi ya nyakati. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 7 Hijiria, mfumo wa jizya ulianza kutoweka polepole na kuongeza fursa za kupata haki za kisheria kwa wasio Waislamu, japo kigezo cha kutoshika hatamu nyeti za uongozi kilibaki kuwa ni hoja muhimu zinazotukima kuzilaumu serikali mbalimbali za Kiislamu. Mafaqihi wa kisasa wa karne ya 14 na15 Hijiria (20 na 21 Miladia) wanaamini kuwa, heshima ya kibinadamu inaweza kutumika kama nyenzo muhimu ya kuimarisha haki za watu wenye itikadi na mirengo mbalimbali, bila ya kuathiri mfumo wa sheria za Kiislamu zinazotawala ndani ya nchi fulani. Utafiti wa Dhana ya Haki za Wachache wa Kidini Dhamana ya Usalama na Heshima kwa Wakristo wa Najrani: Mkataba wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Wakristo wa Najrani ni miongoni mwa vielelezo muhimu vya kihistoria vinavyoonesha ulinzi na heshima za haki za wachache wa kidini katika Uislamu. Kwa mujibu wa mkataba huo, uhai, mali, ardhi na imani za Wakristo hao zilihifadhiwa dhidi ya madhara mbalimbali. Vilevile, familia zao, makanisa na mali zao ziliwekwa chini ya dhamana ya Uislamu, huku kukiwa na umarufuku wa kuwafukuza makasisi au watawa wa kidini kutoka katika taasisi zao za kidini, au kuwavua hadhi yao ya kiroho. Mkataba huo pia ulipiga marufuku aina yoyote ile ya kuwadhalilisha au kuwalazimisha kushikamana na itakadi fulani kinyume na matakwa yao. [1] Haki za wachache wa kidini zinahusisha jumla ya uhuru na fursa ambazo serikali inalazimika kuwapatia waumini wa dini tofauti. Kwa kuegemea hati za kimataifa zinazotetea haki za binadamu, kwa mfano Ibara ya 18, haki hizi ni pamoja na uhuru wa kuabudu na haki ya kumiliki uraia kamili. Ijapokuwa uhuru huo una mipaka kisheria, ila hairuhusiwi kwa serikali fulani kuwapokonya watu fulani haki zao kwa kisingizio kwamba imani zao zinakinzana na msimamo rasmi wa kidini wa taifa husika. [2] Kulingana na mtazamo wa wanafikra (wanazuoni) wa Kiislamu, uanachama wa jamii ya Kiislamu hupatikana kwa imani ya hiari ya kuamini unabii wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), bila kujali tofauti za rangi, utaifa au jinsia. [3] Sambamba na hilo, wanazuoni wa fiqhi, wakitegemea misingi maalumu ya kisheria, kama vile mizani ya kuhifadhi utu na heshima ya binadamu, kanuni ya uadilifu wa kifiqhi, na kanuni ya nafyu al-sabīl (kutotoa mwanya kwa wasio Wasilamu kuwatawala Waislamu), wameweka haki mahususi kwa wachache wa kidini wasiokuwa Waislamu wanaoishi pamoja na Waislamu, haki ambazo hutolewa chini ya mkataba wa dhimma (kulipa kodi maalumu). [4] Haki za Wachache Chini ya Mkataba wa Dhimma Barua ya Imam Ali kwa gavana wa ardhi ya Fars (Irani ya zamani) na Bahrain inaweka wazi sera zake kuhusu haki za wachache walio chini ya mkataba wa dhimma. Baada ya kupokea malalamiko ya udhalilishaji wa wachache wa kidini waliokuwa wakiishi maeneo hayo, alitoa maelekezo yake kumnasihi gavana huyo akisema; “Ingawa ushirikina wao unawazuia kuaminiwa na kuwaweka karibu na uongozi, ila pia ieleweke kwamba mkataba wa dhimma tulioingiana nao unawalinda dhidi ya uonevu na ubaguzi. Kwa hivyo, tumia njia ya kati isiyo ya udhalilishaji wala ulegevu katika kuamiliana nao”. [5] Kulingana na mfumo wa kifiqh, mkataba wa dhima hutumika kama msingi wa kisheria wa kusimamia haki za raia wasio Waislamu wanaoishi ndani ya mamlaka ya Kiislamu. Serikali hudhamini ulinzi wa nafsi na mali kwa sharti la kulipa kodi ya jizya, [6] kodi ambayo wanazuoni wengi wa Kishia huielekeza kwa wanaume huru miongoni mwa Ahlul-Kitab (Wayahudi, Wakristo na Wamajusi), [7] huku wakiwasamehe wanawake na watoto wadogo. [8] Hata hivyo, kulingana na uchambuzi ulitolewa na baadhi ya watafiti wa Kiislamu ni kwamba, ahadi hiyo haikuzuiliwa ndani ya mipaka hiyo pekee, [9] kwani baadhi Hadithi zinaashiria kuwepo kwa makubaliano na mikataba kama hiyo hata na baadhi ya washirikina katika zama za awali. [10] Jee Kulipo Jizya Kunapingana na Haki Msingi za Wachache wa Kidini? Bado dhana ya ulipaji wa jizya imebaki kuwa ni kitendawili mbele ya watetezi wa haki za binadamu; wakosoaji huihisabu kodi hii kama ni nyenzo ya udhalilishaji dhidi ya jamii za wachache, ilhali wanazuoni wa Kiislamu huitetea na kuitambua kama utaratibu wa "usawa wa majukumu kati ya Waislamu na wachache wa kidini." [11] Kwa mujibu wa ufafanuzi wa Mortadhaza Mutahhari ni kwamba, jizya inapaswa kufasiriwa kama fidia ya ulinzi (kama kama waislamu watoavyo kodi mbali mbali). Tofauti ya msingi ni kwamba, wakati Waislamu wanawajibika kulinda dola kwa mali na nafsi zao (jihad), wasio Waislamu huchangia kifedha badala ya kushiriki vitani. [12] Ushahidi wa hoja hii ni ile kanuni ya kisheria inayowaondolea wanawake na watoto wadogo wajibu wa kulipa kodi hiyo. [13] Hii inamaanisha kwamba msingi wa tozo si "imani" wala "mapato," bali ni "uwezo wa kupigana." Hivyo, jizya ni mbadala wa utumishi wa jeshi, pamoja na za ulinzi zitolewazo na serikali ya Kiislamu. Hakiza za Wasio Waislamu Ndani ya Fiqhi ya Kishia Haki za wasio Waislamu zilizoainishwa na wanazuoni wa Kishia ni kama ifuatavyo: Haki Msingi Miongoni mwa haki za wasio Waislamu zinazosimamiwa na mfumo thabiti wa dhimma unaratibu haki mbalimbali ni haki msingi, kama vile ulinzi wa maisha, mali, na heshima ya mtu. Haki hizi ni lazima zilindwe na serikali ya Kiislamu kwa hadhi sawa na ile ya Waislamu. [14] Kwa hiyo, iwapo serikali itashindwa kuwapa ulinzi raia hawa, sheria za fiqhi zinasema kwamba, ni lazima jizya watu hawa warejeshewe kodi yao iliyokussanywa kutoka kwao. [15] Haki za Kimahakama Kwa mujibu wa fiqhi ya Kishia, wasiokuwa Waislamu wamepewa haki kamili ya kisheria ya kutendewa haki mahakamani. [16] Ili kulinda uhuru wao, wanazuoni wamekubaliana kuwa migogoro ya kiraia baina yao imalizwe katika mahakama zao wenyewe, [17] lakini wakaweka angalizo lisemalo kwamba, iwapo mmoja wa waoshitakiana atakuwa ni Mwislamu, basi lazima shitaka hilo lirejeshwe katika mahakama za Kiislamu. [18] Aidha wanazuoni wanasema kwamba, endapo raia mwenye kuishi chini ya mkataba wa dhimma atamuua Mwislamu fulani kwa bahati mbaya na akawa hana uwezo wa kulipa fidia, mzigo huo utabebwa na mtawala wa Kiislamu, na fidia hiyo italipwa kwa kutumia hazina ya mali ya Baitulmal (mali ya umma). [19] Uhuru wa Imani (Dini) Uhuru wa imani (itikadi/dini) ni haki msingi ya kila mwanadamu, na kwa mujibu wa mafaqihi wa Kishia, hakuna mtu wala mamlaka yoyote yale yenye uhalali wa kumwingiza mtu katika Uislamu kwa mabavu. [20] Msingi huu ni imara mno kwenye dini ya Kiislamu kiasi kwamba, hata kama kafiri aliye katika uhasama na Waislamu atakuja katika ardhi yao ili kutafuta elimu ya dini kisha akabaki bila ya kusilimu, bado atakuwa na haki ya kulindwa. Katika hali hiyo, Waislamu wana deni la kimaadili na kisheria la kumsindikiza na kumrejesha mtu huyo makwake akiwa salama, pasipo kumlazimisha kufuata itikadi asiyokuwa na yakini nayo. [21] Uhuru wa Kuabudu Kwa mujibu wa fiqhi ya Kishia, wasiokuwa Waislamu wana haki kamili ya kutekeleza ibada zao, iwe ni kwa mtu mmoja mmoja au kwa pamoja. Majengo ya ibada yaliyojengwa kabla ya kufikiwa kwa mkataba wa dhimma hulindwa kisheria. Hata hivyo, ujenzi wa maeneo mapya ya ibada hutegemea masharti ya mkataba huo, ila kwa mujibu wa fatwa za baadhi ya wanazuoni, haujuzu kuwapa ruhusa ya kujenga majengo mapya ya ibada. [22] Haki ya Kuchagua Eneo la Kuishi Katika muktadha wa haki za kiraia, mafaqihi wa Kishia wanasisitiza kuwa raia wasio Waislamu wana uhuru kamili wa kuchagua miji na maeneo ya kuishi ndani ya himaya ya Kiislamu. [23] Aidha, wana haki ya kushiriki au kuanzisha kazi zenye ajira mbalimbali, mradi tu shughuli hizo ziwe haziendi kinyume na misingi ya sheria za Kiislamu. Haki hizi ni sehemu ya mkataba mpana wa ulinzi unaohakikisha ushirikiano wa kijamii na ustawi wa raia wote. [24] Haki za Kiuchumi Katika nyanja ya uhuru wa kiuchumi, fikihi (fiqhi) ya Kishia inatambua rasmi haki ya umiliki wa mali na biashara huru kwa raia wasio Waislamu. Wala hairuhusiwi kuleta chagizo za aina yoyote ile katika milki au mahusiano yao ya kibiashara bila idhini ya kisheria. [25] Kulingana na fiqhi ya Kishaia; iwapo Muislamu fulani ataharibu mali au bidhaa haramu ya raia asiye Muislamu (kama vile pombe au nguruwe), ambayo kwa imanai ya mhusika ni bidhaa halali, mhusika atalazimika kulipa fidia kamili ya mali hiyo. [26] Aidha, serikali ya Kiislamu ina wajibu wa kisheria wa kusimamia na kulinda mali za wakfu zilizotengwa na Waislamu [27] kwa ajili ya ustawi wa wasio Waislamu ili kuhakikisha manufaa yake yanawafikia walengwa wake ipaswavyo. [28] Hazi za Wasio Waislamu Ndani ya Fiqhi ya Ahlu Al-Sunna Kwa mujibu wa maelezo ya watafiti wa masuala ya Kiislamu, wanazuoni wa madhehebu ya Ahlu al-Sunna wanatambua rasmi haki za wasio Waislamu kupitia mfumo (mkataba) wa kisheria wa dhimma. [29] Tofauti kimsingi kati ya fikihi ya Ahlu al-Sunna na ya Kishia ni kwamba, idadi fulani ya mafaqihi wa Kisunni wanawachukulia watu wote wasioamini (wakiwemo washirikina) kuwa na uwezo na kuingia nao katika mkataba wa dhimma. [30] Mfano wa wazi wa upanuzi huu wa kisheria unaonekana nchini India, ambapo mafaqihi wa Ahlu al-Sunna waliwajumuisha wafuasi wa dini za Kihindi ndani ya mfumo wa dhimma ili kuwahakikishia ulinzi na kuwapa haki zao. [31] Uchunguzi wa Haki za Wachache wa Kidini Ndani ya Serikali za Kiislamu Haki za Watu Waliongia Mkataba wa Dhimma Ndani ya Risala ya Haki ya Imamu Sajjad (A.S): Ama kuhusu haki za Watu wa Dhimma, hukumu yake ni kukubali kutoka kwao kile ambacho Mwenyezi Mungu amekiridhia kwa ajili yao, na kuwa mwaminifu juu ya ahadi walizowekewa na Mwenyezi Mungu kupitia mkataba wao wa dhimma. Ni wajibu wako kuwaruhusu kutekeleza yale wanayoyahitaji na yale waliyolazimika kufuata kulingana na imani yao. Pia katika miamala nao, unapaswa kutekeleza hukumu za Mwenye Ezi Mungu na kuzingatia kuwa watu hao wapo chini ya hifadhi ya Uislamu; hivyo basi, ili kutekeleza ahadi ya Mwenye Ezi Mungu na Mtume Wake, unatakiwa kutowadhulumu watu hao. [32]

Watafiti wengi wameitathmini historia ya mahusiano kati ya Waislamu na wachache wa kidini kuwa na matokeo chanya zaidi ikilinganishwa na tawala nyenginezo zisizo za Kiislamu. [33] [34] Kwa mujibu wa itikadi za wanahistoria, katika vipindi ambavyo watawala wa Kiislamu walizingatia kikamilifu masharti ya mkataba wa dhimma, wasio Waislamu walifurahia kiwango kikubwa cha haki na uhuru wa kijamii. [35] Pamoja na hayo, rekodi za kihistoria hazisiti kuainisha mapungufu yaliyojitokeza, hasa kabla ya karne ya kumi na tatu, ambapo baadhi ya tawala ziliweka vikwazo vyenye utata, ikiwemo kulazimishwa kuvaa mavazi maalumu, marufuku ya kutumia vipando, na katazo la kujenga majengo marefu. [36] Mwanzoni mwa Uislamu Katika zama za awali za Uislamu, Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliweka misingi madhubuti ya kisheria kwa kuingia mikataba na Wakristo, ambapo aliahidi kwa dhati kabisa kulinda haki zao pamoja na kuhifadhi tamaduni zao. [37] Ulinzi huu ulienda mbali zaidi ya haki za msingi, hadi ikafikia watu wanaoishi chini ya dhimma kuliondolewa wajibu wa kufuata baadhi ya kanuni za kijamii za Kiislamu, ikiwemo sheria ya vazi la hijab. [38] Msisitizo wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) juu ya umuhimu wa kulinda mkataba wa dhimma ulikuwa na nguvu kubwa mno katika jamii ya Kiislamu, kiasi kwamba hata na makundi yenye msimamo mkali kama vile Makhawarij walionekena kuuheshimu mkataba huo. Ripoti za kihistoria zinaonesha kuwa kundi la Khawarij, ambalo lilikuwa na sifa ya kuwaua mateka wa Kiislamu, liliamiliana na Wakristo kwa heshima na taadhima kuu kutokana na uzito wa ahadi ya ulinzi iliyotolewa na bwana Mtume (s.a.w.w). [39] Baada ya zama za Mtume, Imam Ali (a.s.) aliimarisha utamaduni huu kwa kuwaagiza magavana wake kuzingatia huruma na upole (ra’afat) katika kushughulikia masuala ya wasio Waislamu. Katika maelekezo yake kwa baadhi ya magavana wake, alisisitiza akiwaambia kuwa, hata kama raia hao hawashiriki imani moja na Waislamu, ila bado wanastahili kutendewa kwa uadilifu, kwa wao pia ni viumbe wa Mwenyezi Mungu. [40] Karne ya 2 - 12 Hijiria Wanahistoria wanabainisha kuwa Wayahudi wa Andalusia waliwaona wapiganaji wa Kiislamu kuwa ndiyo nguvu na sababu ya ukombozi wao. [41] Hali hii ilitokana na ukweli kwamba ndani ya ardhi za Kiislamu, Wayahudi walifurahia uhuru mkubwa zaidi [42] ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika mataifa ya Ulaya yaliyokuwa yakitawaliwa na Wakristo. Ustawi huu uliwafikisha Wayahudi katika nyadhifa za uwaziri, [43] na kipindi hicho kinatajwa kama zama zenye mafanikio makubwa zaidi ya sayansi na fasihi ya Kiyahudi katika historia. [44] Hali ya ukombozi haikuishia Andalusia peke yake; hata katika eneo la Sham (Levant), kiongozi wa Wakristo wa Antiokia aliuchukulia ushindi wa Waislamu kama neema na fursa ya kujikwamua kutoka katika dhuluma za Warumi. [45] Wanahistoria wansema kwamba, chini ya utawala wa Khilafa ya Fatimiyyah (Shia Ismailiyya), makundi madogo ya kidini yaliishi maisha ya amani na utulivu, isipokuwa tu katika kipindi cha utawala wa Al-Hakim bi-Amri Llahi. [46] Katika zama hizi, Wakristo wengi walishika nafasi za uwaziri, [47] hali iliyowapelekea wanahistoria wa Kikristo kuutambua ujumla wa kipindi hichi kama "Enzi ya Dhahabu ya Wakristo nchini Misri". [48] Katika kipindi cha utawala wa Safavi, vyanzo vinaonyesha kuwepo kwa alama za uvumilivu na ustahimilivu (tolerance) katika kuamiliana na makundi madogo ya kidini. [49] Pamoja na hayo, historia inanakili pia vipindi vya unyanyasaji na mateso dhidi ya wasio Waislamu, ambavyo wanahistoria wanavinasibisha na chuki na mihemko ya kidini iliyojitokeza katika nyakati fulani za utawala huo. [50] Karne ya 13 - 15 Hijiria Ripoti za kihistoria zinaonesha kuwa kuanzia karne ya 13 Hijiria na kuendelea, kodi ya Jizya ilianza kuondolewa hatua kwa hatua katika nchi mbalimbali za Kiislamu. [51] Sambamba na mabadiliko haya, kuibuka kwa katiba katika nchi hizi kulipelekea kurasimishwa kwa haki za "Watu wa Kitabu" (Ahl al-Kitab). [52] Pamoja na mageuzi hayo ya kisheria, ila baadhi ya watafiti wanasema kwamba, mabadiliko mengi yaliyofanyika kwa manufaa ya makundi madogo ya kidini hayakuleta matokeo makubwa katika uhalisia wa kiutendaji. Hivyo basi Ingawa sheria zilifanyiwa marekebisho, ila bado kulikuwa na changamoto katika utekelezaji wake kwenye ngazi ya kijamii na kiutawala. [53] Hoja za ukosoaji zinaainisha mambo makuu mawili ambayo yamekuwa yakikosolewa katika mifumo ya utawala wa Kiislamu katika zama hizo: • Kutokuwepo kwa Usawa katika Adhabu ya Kisasi (Qisas): Kanuni inayozuia Muislamu kupewa adhabu ya kisasi (kunyongwa) anapomuua mtu asiye Muislamu. • Vizuizi vya Kiungozi: Umarufuku ya makundi madogo kushika nyadhifa kuu na nyeti za uongozi serikalini, jambo ambalo linaonekana kama kikwazo cha usawa wa kiraia. [54] Hadhi ya Makundi ya Wachache wa Kidini katika Katiba za Nchi za Kiislamu Kwa mujibu wa maelezo ya watafiti mbalimbali, nchi za Kiarabu zimepiga hatuakubwa katika kurasimisha uhuru wa kidini kupitia sheria mama: • Misri: Ibara ya 46 ya Katiba ya Misri inabainisha waziwazi uhuru unaohusiana na madhehebu mbalimbali ya kidini. • Iraq: Katiba ya Iraq inahakikisha uhuru wa itikadi na utekelezaji wa ibada kwa raia wote wa Iraq. [55] Aidha, katika mfumo wa uwakilishi wa kisiasa, wasio Waislamu wametengewa viti sita katika bunge la Iraq ili kuhakikisha sauti yao inasikika katika maamuzi ya kitaifa. [56] • Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran: Katiba ya Iran, inayofuata misingi ya Kishia, inatambua rasmi haki za Ahlul-Kitab (Watu wa Kitabu). [57] Katika ngazi ya uwakilishi, wasio Waislamu wana haki ya viti vinne katika bunge la Iran. [58] Raia wasio Waislamu hawalipishwi tena kodi ya Jizya, huku kukiwa na fungu maalum la bajeti lililotengwa kwa ajili ya mahitaji ya makundi madogo ya kidini. [59] Moja ya mabadiliko makubwa zaidi ni usawa wa malipo ya fidia (diya) kati ya Muislamu na asiye Muislamu. [60] Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna ukosoaji unaoelekezwa katika mfumo wa kisiasa na kisheria. Miongoni mwa ukosoaji huo ni malalamiko ya ukosefu wa ustahimilivu (tolerance) katika utendaji wa kila siku wa kijamii, kutokuwepo kwa haki ya kubadili dini (kutoka Uislamu) na kutotambuliwa rasmi kwa makundi yaliyo nje ya "Watu wa Kitabu". [61] Mwelekeo wa Kutathmini Upya Haki za Makundi ya Wachache wa Kidini katika Sheria za Kiislamu Baadhi ya watafiti wa sheria, katika kutetea haki za makundi ya wachache wa kidini, wanajenga hoja isemayo kwamba, kuzitambua haki hizi chini ya mfumo wa "mkataba maalumu" (Contractual Approach), kunapelekea utekelezaji wa uadilifu miongoni mwa rai. [62] Kinyume na mtazamo huo wa kimkataba, wasomi wengi wa Kishia wanaamini kuwa katika Uislamu, hadhi na heshima ya utu na ubinadamu (Inherent Dignity), ni sifa ya asili na ya ndani (intrinsic) ya kila mwanadamu. Hii ina maana ya kwamba, utu huo hauwezi kuhamishwa au kufutwa kutoka kwa Muislamu au asiye Muislamu, wala hauwezi kutolewa kama "zawadi" au fadhila kupitia mkataba fulani, kwani ni haki ya kuzaliwa nayo. [63] Kwa kurejea Aya za Qur'ani, Allama Tabatabai anasisitiza akisema, “Utu wa binadamu unawahusu Waislamu na wasio Waislamu kwa usawa na bila ubaguzi ule ndani yake. [64] Yousef Saanei naye akitegemea msingi wa kuheshimu utu asilia, ametoa fatwa madhubuti yenye kutaka utekelezaji wa usawa kamili katika malipo ya fidia (diya) pamoja na adhabu ya kisasi (qisas) kati ya Muislamu na asiye Muislamu. [65] Baadhi ya wanafikra wa kisasa wanaamini kuwa inawezekana kufanya mageuzi na mabadiliko katika baadhi ya kanuni za Kiislamu ili kuendana na mahitaji ya wakati. Wao wanaamini kwamba, mageuzi haya yanaweza kufanyika huku misingi mikuu ya sheria za Kiislamu ikibaki salama bila ya kupatikana maharibiko yoyote yale ndani yake. [66]