Mkopo:Dhana ya Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu
Dhana ya Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu: Kuamrisha mema na kukataza maovu ni dhana inayofasiriwa kama ni hatua na jukumu la kuwahimiza watu kutenda mema na kuwakataza maovu. Dhana hii ni mojawapo ya nguzo kuu za dini, ambayo imesisitizwa mno ndani ya Qur'ani pamoja na Hadithi. Kwa mujibu wa wanazuoni wa Kishia, wajibu huu ni wa Kifaya (Faradhi ya Kutoshelezana); ikimaanisha kuwa, iwapo kundi moja litatekeleza jukumu hili, basi wengine huondolewa lawama ya kutolitekeleza kazi hiyo. Katika Fiqhi ya Kiimamia (Shia Ithnaasharia), jukumu hili linahesabiwa kuwa ni sehemu ya Matawi ya Dini (Furu' ad-Din), ilhali katika madhehebu mengine kama Mu'tazila na Zaidiyya, linahesabiwa kuwa ni sehemu ya Misingi ya Imani (Usul ad-Din). Mafakihi wametaja sharti nne zinazothibitisha wajibu wa amri hii: Kwanza, ni elimu (ujuzi) wa mwamrishaji na mkatazaji juu ya hukumu za kisheria za lile jema analoliamrisha au ovu analolikataza. Pili, ni uwezekano (ihtimal) wa kuleta taathira kwa mlengwa wake. Tatu, ni kuwa na yakini juu ya azma ya mkosaji ya kuendelea na baya alitendalo (israr). Nne, ni kutokuwepo kwa madhara (intifa' al-dharar) juu ya nafsi, mali, au hadhi ya mwamrishaji au Waumini wengine. Aidha kuna daraja (maratib) tatu maalum zilizoainishwa kuhusiana na namna ya utekelezaji wa jukumu hili; kwanza ni kukataa kwa moyo (inkar al-qalbi) na kudhihirisha karaha kupitia vitendo visivyotumia maneno. Ikikosekana taathira katika hatua hiyo, hufuata hatua ya kukemea kwa ulimi (inkar al-lisani). Endapo hatua mbili za awali hazitozaa matunda, hapo hujuzu kuchukua hatua za vitendo (amali), ambazozinatakiwa zitekelezwe kwa kuzingatia kuanzia ngazi ya chini na kuendelea (tadrijyyun) na kwa idhini maalum ya Imamu au Naibu wa Imamu wa umma. Mwongozo wa Kisheria Kuhusu Wajibu wa Kuamrisha Mema Sheria ya Kiislamu na mapokezi ya Kishia yameuainisha uamrishaji wa mema na ukatazaji wa maovu kuwa ni miongoni mwa mambo ya lazima katika dini. Msisitizo wa Maimamu watukufu umeifanya mada hii kuwa na sura na milango ya kipekee katika vitabu vya sheria, ikiwemo sehemu maalumu iliyomo ndani ya babu ya Jihadi. Hadithi zilizokusanywa katika vitabu vikuu vya mapokezi zimefafanua vigezo na hukumu zinazostahili kuzingatiwa. Katika sayansi ya akida, jambo hili limeorodheshwa kama moja ya misingi ya wema, huku kukiwa na mjadala wa kina wa kielimu kuhusu chimbuko la wajibu wake—ikiwa ni amri inayotokana na akili timamu au ni maelekezo ya kisheria yaliyofunuliwa kupitia dini. Umuhimu wa Kuamrisha Mema na Kukataza Maovo Katika mfumo wa kisheria na kimaadili wa Kiislamu, uamrishaji wa mema na ukatazaji wa maovu unahesabiwa kuwa miongoni mwa wajibu mkuu na muhimu zaidi wa kidini. [1] Jambo hili limesisitizwa na kupewa uzito mkubwa katika mafundisho ya Maimamu watukufu (a.s). [2] Tukirudi ndani ya vitabu vya sheria (Fiqhi), tutaikuta mada hii imetengewa mlango na sehemu maalumu inayojitegemea. [3] Kwa mfano, katika kitabu cha al-Lum‘atu al-Dimashqiyya, mada hii imeshughulikiwa kama mlango huru ndani ya maudhui ya Jihadi. [4] Aidha mwandihi wa kitabu al-Kafi pia naye ameichambua mada hii katika mlango maalumu wenye Hadithi zinazozungumzia mada ya kuamrisha mema na kukataza maovu. [5] Vilevile, wasomi wa Hadithi kama vile Hurr al-Amili wamekusanya mamia ya mapokezi (Hadithi) katika kitabu cha Wasa'il al-Shia, wakibainisha vigezo na masharti 41 tofauti ya utekelezaji wa amali hii adhimu. [6] Pia tukitupia macho vitabu vya elimu ya Akida, tutalikuta tendo hili linatazamwa kama kielelezo maalumu cha neema za Mungu (lutf), [7] huku kukiwa na mjadala iwapo wajibu wake unatokana na mantiki ya akili au ni amri ya kisheria. [8] Kuna Aya kadhaa zinazozungumzia nadharia ya kuamrisha mema na kukataza mabaya ndani ya jamii ya Kiislamu. [9] Kuamrisha mema na kukataza maovu hufanya kazi kama injini ya utekelezaji wa wajibu mwingine wote ndani ya umma. Ndani ya Aya za Qur'ani, uamrishaji mema na ukatazaji maovu umeainishwa kama jukumu la msingi la kijamii ambalo limeunganishwa moja kwa moja na imani ya dkumuamini Mwenye Ezi Mungu iendayo sambamba na utekelezaji wa nguzo za ibada. [10] Aidha ukubwa na uzito wa wa jukumu hili unadhihirika kupitia kauli ya Imam Ali (a.s), ambapo anafananisha matendo mengine mema na tone la maji mbele ya ukubwa wa bahari ya uamrishaji mema na ukatazaji maovu. [11] Pia kulingana na Riwaya ya Imam Sadiq (a.s), wajibu huu ndio msingi wa utulivu na maendeleo ya jamii; kwani jambo hili ndilo linalopelekea kukubalika amali mbalimbali pamoja na kudhamini usalama wa usafiri, uhalali wa shughuli za kiuchumi, na uhifadhi wa haki za watu. Vilevile, uamrishaji mema na ukatazaji maovu ndio unaostawisha ardhi na kudhamini ulinzi dhidi ya maadui wenye tamaa za kuvamia ardhi za Waislamu. [12] Katika mfumo wa kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ibara ya nane ya Katiba inatambua jukumu la “Amru bil-Maaruf na Nahyu an al-Munkar” kama kanuni ya msingi ya utawala wa nchi hiyo. Ibara hii inausimika wajibu huu kama wajibu wa kidunia na wa kidini kwa raia wote (universal duty) wa Irani. [13] Ili kuratibu utekelezaji wa kisheria wa dhana hii, dola hii imeanzisha taasisi maalumu (Setadi Amr Bilmaaruf) inayoshughulika na uratibu na uhamasishaji wa maadili hayo, ikilenga kuhakikisha kuwa nidhamu ya kimaadili inazingatiwa katika nyanja zote za utawala na maisha ya kijamii. [14] Uamrishaji Mema kama Kiunganishi cha Madhehebu ya Kiislamu Dhana ya Uamrishaji mema na ukatazaji maovu (Amr bilmaaruf na Nahyu an al-munkar) ni miongoni mwa dhana zinazoshirikishwa na madhehebu mbalimbali ya Kiislamu, na hutajwa kama kiunganishi cha pamoja cha fikra za Kiislamu. Kwa upande wa wafwasi wa madhehebu ya Muutazila, dhana hii ni nguzo ya tano ya misingi yao ya kiitikadi (Nguzo za Dini), [15] wakisisitiza kuwa Mwislamu ana wajibu wa kumwamrisha mema na kumkataza mabaya hata yule ambaye ni kafiri au mtenda dhambi asiyejali dini (fasiq). [16] Vilevile, madhehebu ya Zaidiyyah huihesabu amali ya kuamrisha mema na kukataza mabaya, kuwa ni msingi wao wa tano wa imani (wa Nguzo za Imani), [17] na simulizi za kihistoria zinaeleza kuwa hata Zaid bin Ali alijenga harakati yake juu ya msingi huo. [18] Kwa upande mwingine, katika mfumo wa madhehebu ya Shia Imamiyyah (Shia Ithna Ashariyyah), dhana hii imeainishwa na kuhisabiwa kuwa ni moja kati ya matawi ya dini (Furu al-Din), na ni wajibu wa kisheria uliosimamama nje ya upande wa nguzo za kiitikadi (Usulu al-Din). [19] Fasili ya Kisheria Juu ya Dhana ya Uamrishaji Mema na Ukatazaji Maovu Katika mfumo wa sheria za Kiislamu, "Kuamrisha Mema" inamaanisha kuwahimiza watu kutekeleza matendo yanayokubalika, yenye sifa njema, na yaliyo halali kisheria. Kwa upande mwingine, "Kukataza Maovu" inahusu kuzuia utendaji wa mambo machafu na madhambi. [20] Jukumu hili la kisheria lina upana mkubwa, na linaweza kutekelezwa kwa njia tofauti, ikiwemo njia ya kauli (mawasiliano ya mdomo kwa mdomo), kwa njia zisizo za maneno, ikiwemo kutumia vitendo na mienendo mingine inayofaa ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii husika. [21] Katika majibu wa mtazomo wa Mwanazuoni wa Kishia ajulikanaye kwa jina la Sayyid Ali Sistani ni kwamba; dhana ya 'Maaruf' (amali njema) inajengwa juu ya misingi miwili: utambuzi wa kiakili (kimantiki) na mwongozo wa kisheria (dini). Hivyo basi tendo huchukulika kuwa ni jema ima kwa kipimo cha mantiki ya binadamu au kupitia andiko fulani la kidini linalothibitisha ubora wake. Vilevile, 'Munkar' (amali mbovu) inafasiriwa kwa maana ya kitendo ambacho ima ubaya wake unafahamika kupitia akili ya binadamu, au kwa kukupitia katazo lililotangazwa na mamlaka ya kisheria. [22] Kulingana na nadharia ya kisheria ya Muhaqqiq Hilli na Allamah Hilli, fasili ya 'Maaruf' (amali njema) na 'Munkar' (amali mbovu) imepanuliwa kwa kuingiza kigezo cha ziada cha utambuzi wa mtendaji wa amali hiyo (the performer's cognition). Wanazuoni hawa wanasema kuwa; 'Maaruf' ni kila kitendo cha heri ambacho mbali na sifa yake ya kisheria, pia mtendaji wake anakifahamu kwa dhati kuwa ni kitendo chema. Vivyo hivyo, 'Munkar' ni tendo lenye madhara ambalo mtendaji pia analifahamu kwa tendo hilo ni tendo baya. Mtazamo huu wa kielimu unalenga kuhakikisha kuwa uwajibikaji wa mwanadamu unazingatia uwezo wake wa kupambanua kati ya mema na maovu. [23] Maelezo ya Sahib al-Jawahir Kuhusu Ngazi za Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu Muhammad Hasan al-Najafi, anayejulikana kama Sahib al-Jawahir, amesema: Moja ya daraja kubwa, za juu na imara zaidi za kuamrisha mema na kukataza maovu kwa upande wa kuleta mabadiliko, hasa miongoni mwa viongozi wa dini, ni wao kuvaa vazi la mambo mazuri, yawe ni ya lazima (wajibu) au yanayopendekezwa (mustahabu), na kuvua vazi la mambo mabaya, yawe ni ya haramu au yanayochusha (makruhu), na wajikamilishe wenyewe kwa maadili mazuri na wajitakase na tabia mbaya. Kazi kama hii inasababisha kuwasukuma watu kwenye kufanya heri na kuacha mambo yaliyokatazwa; hasa kama itakamilishwa na mawaidha mazuri, ya kuhimiza kheri kwa njia ya kuwapa motisha na kuonya mabaya kwa njia ya kuwatahadharisha na hatari inayowakabili. Hii ni kwa sababu kila nafasi ina maneno yake mahususi na kila maumivu yana dawa yake maalumu, na kutibu roho na akili ni jambo la juu sana kuliko kutibu miili. Muhammad Hassan Najafi, Jawahiru al-Kalam, Juz. 21, Uk. 382-383, Chapa ya Mwaka 1404 Hijiria Hukumu za Kisheria Kuhusiana na Amali ya Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu Kwa mujibu wa fatwa za wanazuoni wa fiqhi ya Kishia, kuamrisha mema na kukataza maovu ni miongoni mwa amali za wajibu iiliyoko juu ya shingo ya kila Muislamu. [24] Baadhi ya wasomi wameainisha wajibu huu kuutaja kuwa ni miongoni mwa mambo ya msingi na ya lazima katika dini; kiasi kwamba mtu anayekanusha kwa makusudi wajibu huo, huku akiwa na elimu juu yake, huhesabiwa kuwa ametoka na kusimama nje ya mipaka ya imani (mritadi). [25] Aidha Mafaqihi wa Kishia wameeleza kuwa kiwango cha wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu hufuata uzito wa jambo lenyewe. Endapo jambo jema linalohimizwa ni la daraja la sunna (mustahabu), na jambo baya linalokatazwa ni la kuchusha tu (makruhu), basi uamrishaji na ukatazaji katika hali hiyo hubadilika na kuwa tendo linalopendekezwa (mustahabu), si wajibu wa lazima. [26] Wajibu wa Pamoja au wa Binafsi? Katika fiqhi ya Kiislamu, wanazuoni wamejadili kwa kina huku wakikhitilafiana iwapo kuamrisha mema na kukataza maovu ni wajibu wa kutosheleza (wajib kifā’i) au ni wajibu wa kila mtu binafsi (wajib ‘aini). [27] Rai iliyoenea miongoni mwa mafaqihi na wanazuoni mbalimbali, ni ile isemayo kuwa jukumu hili ni wajibu wa kutosheleza. Kwa mujibu wa mtazamo huo, iwapo kundi la watu fulani litalitekeleza jukumu hilo kwa kiwango kinachofanikisha madhumuni yake ya kisheria, wajibu huo huwaondokea wengine waliomo katika jamii hiyo. [28] Shahid Thani akielezea msimamo wake kuhusiana na jambo hili anasema kwamba, kusudio kuu la sheria katika uamrishaji mema na ukatazaji maovu ni kuhakikisha kuwa mema yanadumu katika jamii na maovu yanaachwa. Kwa msingi huo, wajibu huu haujaelekezwa kwa mtu maalumu, bali unawahusu watu wote walio chini ya dhamana ya kisheria (mukallafun). Hivyo basi, endapo kundi fulani litachukua jukumu hilo na kulitekeleza ipasavyo, wengine hawabebeshwi tena lawama za kisheria. [29]
Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wakubwa wa Kishia wamechukua msimamo tofauti. Kwa mfano Sheikh Tusi katika al-Nihayah, [30] Ibn Hamzah katika al-Wasilah, [31] pamoja na Muhaqqiq Karaki [32] wanaona kuwa, kuamrisha mema na kukataza maovu ni wajibu wa binafsi (wajib ‘aini) unaomkabili kila mtu katika jamii. Kwa mtazamo huu, kila muumini anayekidhi masharti ya kisheria anawajibika kulitekeleza jukumu hilo yeye mwenyewe, bila kutegemea utekelezaji wa wengine. Je, Wajibu Huu ni Wajibu wa Kiakili au wa Kisheria? Kumekuwepo mjadala wa muda mrefu katika fiqhi na teolojia ya Kishia, kuhusu asili ya wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu: na kwamba je, ni wajibu unaotokana na sheria ya dini (wajib shar‘i) au ni wajibu unaothibitishwa na akili (wajib aqli)? [33] Idadi kubwa ya mafaqihi na wanazuoni wa akida wanaona kuwa wajibu huu ni wa kisheria. Hoja yao inajengwa juu ya dalili za kimaandiko, zikiwemo Aya za Qur’ani, Hadithi zilizosimuliwa kwa wingi (mutawatir) kutoka kwa Maimamu watoharifu, pamoja na makubaliano ya wanazuoni (ijmai). [34] Kwa mtazamo huu, mamlaka ya wajibu huo hutokana moja kwa moja kwenye maandiko ya sheria ya dini. Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni wameutazama wajibu huu kuwa ni zao linalotokana na msingi wa kiakili. Kwa mujibu wa mtazamo huo, akili yenyewe inahitimisha ulazima wa kuamrisha mema na kukataza maovu kwa misingi miwili mikuu ifuatayo: • Kwanza kabisa ni msingi wa lutf (msaada wa huruma ya Kiungu): kwa kuwa kuamrisha mema humwelekeza mwanadamu kwenye utiifu na humkaribisha kwenye wema, kunachukuliwa kuwa ni aina ya neema ya Kimungu. Kwa hoja ya kiakili, inafaa kwa Mungu kuweka mazingira yanayomsaidia mja kuelekea utiifu; hivyo, kuweka wajibu wa uamrishaji wa mema huonekana kuwa ni mwendelezo wa neema hiyo. [35] • Pili ni msingi wa kuchukuwa tahadhari dhidi ya madhara tarajiwa: kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu kunaweza kuleta madhara ya kijamii na ya kiroho duniani na akhera. Kwa kuwa akili inahukumu ulazima wa kujiepusha na madhara yanayotarajiwa, inahitimishwa kuwa utekelezaji wa jukumu hili ni wajibu wa kiakili unadhamini kuzuia madhara hayo. [36] Tofauti hii ya mitazamo haiondoi ukubwa wa nafasi ya uamrishaji wa mema na kukataza mabaya ndani ya mfumo wa maadili ya Kiislamu, bali inaonesha upana wa tafakuri ya wanazuoni juu ya uhusiano kati ya akili, sheria ya dini, na wajibu wa kijamii wa kila muumini.
Masharti ya Kuamrisha Mema na Kukataza Maovu
Kwa mujibu wa fatwa za mafaqihi, wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu hufungamana na kutimia kwa masharti maalumu. Endapo masharti hayo hayatatimia, wajibu huo hauwi ni wajibu wa lazima. [37] Masharti hayo ni haya yafuatayo: • Kwanza, nia lazima mwenye kuamrisha mema na kukataza maovu awe na ujuzi wa kisheria unaomwezesha kutambua kwa uhakika lipi ni jema na lipi ni baya kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Utekelezaji wa jukumu hili bila elimu unaweza kusababisha kuchanganya haki na batili na kuleta athari hasi, jambo ambalo halikubaliki kisheria. • Pili, kuwepo kwa uwezekano wa athari (natija chanya). Ni sharti pawepo matarajio ya kuridhisha kwamba amri au katazo hilo litakuwa na matokeo chanya kwa anayeelekezwa. Endapo itajulikana au kudhaniwa kuwa juhudi hiyo haitakuwa na athari yoyote, wajibu huo hauwi ni wa lazima. • Tatu, kuendelea kwa tendo la kosa. Ni lazima ijulikane kuwa mhusika bado anaendelea na kosa lake. Ikiwa itathibitika kuwa mhusika huyo tayarti ameacha kosa kwa hiari yake au ametubia na hana nia ya kulirudia, basi hapatakuwa na wajibu wa kumkanya juu ya kosa hilo. • Nne, kutokuwepo kwa madhara makubwa. Kuamrisha mema na kukataza maovu kusisababishe hatari kwa maisha, mali, au heshima ya anayetekeleza jukumu hilo au ya waumini wengine. Iwapo kutakuwa na hofu ya madhara makubwa yanayotarajiwa, wajibu huo huondoka, kwa kuwa sheria haimlazimishi mtu kujitumbukiza katika madhara makubwa yasiyostahimilika. [38] Ngazi za Utekelezaji wa Uamrishaji Mema na Ukatazaji Maovu
Mafaqihi wa Kishia wameainisha hatua maalumu za utekelezaji wa wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu. Fatwa zao zinasisitiza kuwa utekelezaji wa jukumu hili lazima ufanyike kwa kufuata ngazi moja baada ya nyengine (maratib) na kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa. Ni imani ya wanazuoni hawa kuwa hatua hizi zinapaswa kufuatwa kwa mtiririko maalumu na kwa namna ya taratibu (gradualism), ili kuhakikisha kuwa lengo la kisheria linafikiwa kwa hekima na ufanisi kamili. [39]
Hatua ya Kukataza Mabaya Kupitia Moyo
Hatua ya kwanza kabisa katika mchakato wa kuamrisha mema na kukataza maovu ni kukataa kupitia uchukivu na katao la moyo. [40] Katika hatua hii, mtu anapaswa kudhihirisha hali yake ya kutopendezwa na kutoridhika na mwenendo wa muovu kupitia ishara na vitendo mbalimbali. Hatua hizi ni pamoja na kukunja uso (kuonyesha sura ya ukali), kufumba macho, kukasirika (kununa), kugeuza uso, kujitenga na mhusika, au hata kusitisha mahusiano naye kabisa. Hii ni njia ya awali ya kuonyesha msimamo wa kimaadili bila kutumia maneno. [41]
Hatua ya Kukataza Mabaya kwa Njia ya Kauli Hatua ya pili katika mfumo wa kuamrisha mema na kukataza maovu ni uamrishaji na ukatazaji kwa njia ya maneno. [42] Ikiwa itabainika kuwa hatua ya awali ya kukataa kwa moyo haina athari inayokusudiwa, mhusika anawajibika kutumia kauli. Katika ngazi hii, mchakato unapaswa kuanza kwa mawaidha ya hekima na nasaha za kiungwana zinazolenga kugusa hisia za mhusika. [43] Kanuni ya kisheria inasisitiza kuwa, ikiwa kuna uwezekano wa kuleta mabadiliko kupitia lugha hii ya upole, ni marufuku kabisa kushadidisha hatua au kuvuka kiwango hicho cha mawasiliano. Kwani lengo la sheria ni kurekebisha bila kudhalilisha. [44] Hatua za Kivitendo na Matumizi ya Nguvu Udhibiti Hatua ya tatu katika mfumo wa uamrishaji mema na ukatazaji maovu ni kuchukua hatua za kivitendo na kutumia nguvu. [45] Ngazi hii imeruhusiwa kisheria ikiwa tu hatua mbili za awali (kukataa kwa moyo na kwa maneno) hazikuleta athari inayokusudiwa. [46] Utekelezaji wa hatua hii unapaswa kufuata utaratibu wa hatua kwa hatua, ukianzia na njia nyepesi kuelekea zilizo nzito zaidi. Hatua hizi zinaweza kujumuisha vitendo kama vile kupiga, kuweka vikwazo maalumu, au kumweka mhusika kizuizini. Hata hivyo, matumizi haya ya nguvu hayapaswi kufikia hatua ya kusababisha majeraha, ulemavu wa kudumu, au kupelekea ulipaji wa fidia (diya) na kutekelezwa kwa hukumu ya kisasi (qisas). [47] Hukumu ya Kujeruhi na Kuua katika Utekelezaji wa Uamrishaji Mema na Ukatazaji Maovu Kwa mujibu wa msimamo mashuhuri miongoni mwa mafaqihi wa Kishia, ni marufuku kisheria kumsababishia mlegwa jeraha au kumuua katika mchakato wa kuamrisha mema na kukataza maovu, isipokuwa kwa idhinisho la Imamu au Naibu wake linalojiri kulingana na sheria za Kiislamu. [48] Baadhi ya wasomi wanaeleza kuwa katika kipindi hiki cha Ghaiba (kutokuwepo kwa Imamu), jukumu la kutoa idhini kama hiyo linamwangukia Mwanasheria mwenye sifa kamilifu (Faqih Jami' al-Sharait) tu. [49] Mwanachuoni mashuhuri wa karne ya 13 Hijiria, ajulikanaye kwa jina la Sahib al-Jawahir, anasisitiza akisema kuwa; kizuizi hiki cha kisheria ni cha lazima na kimewekwa ili kuzuia machafuko, vurugu, na ufisadi katika jamii. [50] Tofauti kati ya Kuamrisha Mema, Kukataza Maovu na Kumuongoza Asiyejua Pia tazama: Kumwongoza Mjinga Wanazuoni wa fiqhi wamefafanua na kuainisha tofauti msingi zilizopo kati ya kuamrisha mema na kukataza maovu, na kumuongoza asiyejua (irshadu al-jaahil). Kumuongoza asiyejua hufanyika pale ambapo mtu atakuwa hana maarifa kuhusu hukumu ya kisheria kuhusiana na jambo fulani, au hajui jambo linalofungamana na sheria hiyo, au labda hajui vyote viwili. Katika hali hiyo, jukumu la anayemwelekeza ni kumpatia elimu na ufafanuzi, si kumkanya kwa maana ya kukataza maovu na kuamrisha mema.
Kwa mfano, ikiwa mtu hajui kuwa kunywa pombe ni haramu, au anajua hukumu ya uharamu wa pombe lakini hajui kuwa kinywaji alichonacho kinaingia kwenye orodha ya pombe. Katika hali hiyo kumfahamisha na kumzuia katika huhesabiwa kuwa ni kumuongoza asiyejua. Hata hivyo, iwapo mtu atakuwa anajua wazi kuwa kunywa pombe ni haramu na pia anajua kuwa kinywaji kilichopo mbele yake ni pombe, basi kumzuia kwake katika hali hiyo huingia katika mlango wa kuamrisha mema na kukataza maovu. [51] Hivyo basi kitaalamu fiqhi hutenganisha kati ya kosa linalotokana na ujinga na kosa linalotokana na ukaidi wa makusudi. Katika hali ya kwanza, kipaumbele ni elimu; katika hali ya pili, kipaumbele ni utekelezaji wa jukumu la kijamii la kukataza maovu. Mada Zinazofungamana • Aya ya 104 ya Suratu Aal Imran • Aya ya 110 ya Suratu Aal Imran