Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Dhadana ya Hilfu al-Ahlaf

Kutoka wikishia


Dhadana ya Hilfu al-Ahlaf: inayojulikana pia kama Laqatu ad-Dam (Walioramba Damu) ilikuwa ni muafaka na muungano wa kikoo ulioundwa katika zama za kabla ya Uislamu miongoni mwa baadhi ya koo za Waquraish, kufuatia mvutano kuhusu umiliki na usimamizi wa nyadhifa za Kaaba iliyoko mjini Makka. Qusaiyy ibnu Kilab, babu wa nne wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), ndiye aliyepanga upya wadhifa wa uongozi wa Makka na kugawa majukumu ya Kaaba kati ya wanawe wawili: Abdu al-Dar ibnu Qusaiyy na Abdu Manaf ibnu Qusaiyy. [1] Abdu al-Dar alipewa Jukumu la kushika ufunguo wa Kaaba, uongozi wa Daru al-Nadwa (baraza la mashauriano) na ubebaji wa bendera ya vita. Ama Abd Manaf alipata jukumu la kuwanywesha maji mahujaji, kuwakaribisha na kuwahudumia mahujaji hao ndani ya msimu wa hija. [2] Baada ya kufariki kwao, kizazi cha kila upande kilianza kudai haki ya kushika nyadhifa hizo, na hivyo kuzuka kwa mzozo mkali kati yao. [3] Baadhi ya nukuu zinaeleza kuwa Qusaiyy alikuwa amempa Abdu al-Dar mamlaka yote, [4] jambo lililowafanya wana wa Abdu Manaf kupinga kuhodhiwa kwa uongozi huo na ukoo wa Abdu al-Dar. [5] Katika hali hiyo, koo za Waquraish zikagawanyika katika makundi miwili. Ukoo wa Abd Manaf, kwa kuungwa mkono na Banu Asad, Banu Zuhra, Banu Tayyim na Banu al-Harith, uliunda muafaka wa Hilfu al-Mutayyabin (Waliojipaka manukato). {Maelezo 1: Ni jina lililotokana na desturi ya kupaka mikono manukato na kupangusia juu ya Kaaba kama ishara ya kuimarisha muafaka.} [6] Kwa upande mwingine, ukoo wa Abdu al-Dar, kwa kushirikiana na Banu Makhzum, Banu Jumah, Banu Sahm na Banu Adi, uliunda muafaka wa Ahlaf au Laqat ad-Dam, (mshikamano kwa kula kiapo cha kuramba damu) {Maelezo 2: Nao, kwa kuchinja mnyama (ng’ombe) na kupaka mikono yao damu ya mnyama huyo kisha kuiramba, walidhihirisha uaminifu na mshikamano wao juu ya muafaka wao.}. [7] Hatimaye, kwa juhudi za wapatanishi, suluhu ilifikiwa: jukumu la kuwanywesha na kuwahudumia mahujaji lilibaki mikononi mwa ukoo wa Abdu Manaf, huku ufunguo wa Kaaba na ubebaji wa bendera ya vita ukakabidhiwa mikononi mwa ukoo wa Abdu al-Dar. [8] Mapatano hayo yalizuia kuzuka kwa vita vya kikoo na yakadumu hadi kuibuka kwa Uislamu, yakibaki kuwa mojawapo ya mifano ya mapatano ya kisiasa na kijamii katika jamii ya Makka ya kabla ya Uislamu. [9]