Nenda kwa yaliyomo

Mkopo:Dawa za kulevya

Kutoka wikishia

Dawa za kulevya (Madawa ya Kulevya): ni vitu vyenye asili ya kuchangamsha (musisimu), kusababisha njozi (hisia ongo akilini zenye kuvuruga fahamu), au kuleta ulegevu wa mwili ambavyo pia huleta madhara ya kimwili na kiakili (kisaikolojia). Sifa kuu ya vitu hivi ni uwezo wake wa kusababisha uraibu na utegemezi (usehelevu) baada ya kutumiwa kwa mara chache tu. Kitaalamu, vitu hivi hufafanuliwa kwa maana ya kitu chochote kile kinacholeta hali ya uchangamfu usio wa kawaida au udhaifu mkubwa katika viungo vya mwili. Mafaqihi na wanazuoni wa Kiislamu wamefikia makubaliano ya pamoja (ittiifaq) kuwa ni haramu kutumia ya aina zote zile za madawa ya kulevya. Uamuzi huu umefikiwa kulingana na miongozo ulioibuliwa katika vyanzo vikuu vinne: Aya za Qur’ani, Hadithi, Aql (Mantiki/Akili) na Qaidah laa-Dharar (Kanuni /Kaida ya Kutodhuru). Watafiti wanabainisha kuwa nukta kuu ya makutano (kiunganishi) kati ya vileo (vinywaji vya kulevya) na dawa za kulevya ni kupotea kwa fahamu na utambuzi (mwamko wa akili). Ingawa zote mbili husababisha uharibifu wa akili, ulegevu wa viungo, na kupelekea mawazo maovu yanayochochea uhalifu, ila kuna tofauti ya kisheria katika hukumu zake. Mafaqihi wengi hawaoni dawa za kulevya kuwa ni "ulevi" kwa mtazamo wa kimila na kijamii (urfi). Hivyo basi mafaqihi wengi wa Kishia hawawahukumu watumiaji wa madawa ya kulevya kupitia adhabu zilizowekwa kwa ajili ya mnywa pombe (haddi), bali huhukumu kwa adhabu ya ta’azir (adhabu zinazotolewa kwa mujibu wa mwongozo wa hakimu au serikali, kwa ajili ya makosa yasio na sheria (adhabu) maalumu ndani ya Uislamu).

Wanazuoni wametoa hoja mbalimbali katika kuharamisha biashara na usambazaji wa dawa hizi. Baadhi yao wamesema kwamba; Biashara hii ni haramu kwa sababu haina faida yoyote ya halali au ya kimantiki (uqlai) kwa binadamu.  Wengine wanasema kwamba; haramu wa biashara hii utokana na ukubwa wa madhara wanayosababishwa madawa haya. Kutokana madhara makubwa ya madawa haya, baadhi ya mafaqihi wametoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa wasafirishaji wakubwa wa dawa za kulevya huku wakiwapa sifa ya"Mufsid fi al-Ardhi" (waharibifu wa ulimwengu). 

Ufafanuzi wa Dhana na Nafasi ya Madawa za Kulevya Dawa za kulevya (madawa ya kulevya) hufafanuliwa kitalaalamu kama vitu vyenye huzalisha hali ya uchangamfu na bashasha isiyo ya kawaida kwa mtumiaji, hali ambayo baada ya muda mfupi tu hupelekea mhusika kupata uraibu na utegemezi wa kudumu wa kutumia vitu hivyo. [1] Vilevile, kwa mtazamo wa kisheria na kitiba, kitu chochote kile ambayo kinachopelekea ulegevu na udhaifu mkubwa na wa dhahiri katika mwili wa binadamu hutambuliwa kama dawa ya kulevya. [2] Katika mapokezi ya Hadithi mbalimbali, dawa za kulevya hazikutajwa kwa jina moja la jumla kama ilivyo katika zama za hivi sasa, bali zilitajwa kupitia majina kwa majina tofauti. Baadhi ya majina hayo ni pamoja na "banji" (bangi/kanja), "muftir" (mada ilegezayo/idhoofishayo), "makhadir" (mada ya ganzi/kulevya), na "afyuni" (opium). [3] Katika vyanzo mbalimbali vya sheria ya fiqhi (vitabu vya fiqhi), hakuna mlango mmoja uliotengwa ambao ni mahususi kwa ajili ya kujadili madawa ya kulevya kama mada moja inayojitegemea. Badala yake, kutokana na unyeti na athari zake, hukumu zinazohusiana na mada hii zimeelezwa kwa kina ndani ya milango mbalimbali ya kisheria kulingana na muktadha wa matumizi au athari zake. Milango yenye kuzingumzia suala hili katika vita hivyo ni pamaja na; Mlango unajadili adhabu za Kisheria (Hudud wa Ta’azirat), [4] Sheria za Usafi na Unajisi (Tahara wa Najaasaat), [5] Ibada ya Sala (Salat), [6] Sheria za Talaka (Talaq), [7] Uhalifu na Usalama wa Umma (Muharabah), [8] Fidia ya Majeraha na Vifo (Diyaat) [9] na Mlango wa Kanuni za Vyakula na Vinywaji. [10] Mfanano Kati ya Madawa ya Kulevya na Vileo Mwanachuoni Muhammad Baqir al-Sadr (aliyefariki 1980 Miladia), katika kitabu chake Bahuth fi Sharhi al-Urwati al-Wuthqa, anabainisha akisema kwamba, kuna mambo muhimu yanayounganisha dawa za kulevya na vinywaji mbalimbali vya kulevya (vileo). Ingawa kisheria zinaweza kutofautiana katika baadhi ya hukumu zake, ila kiini cha viwili hivi kinafanana katika nyanja zifuatazo: 1. Kupotea kwa Utambuzi (Mwamko wa Akili): Vyote viwli vina sifa ya kuondoa uwezo wa mtu wa kujitambua na kufahamu mazingira yake. [11] 2. Uharibifu wa Akili na Ulegevu wa Mwili: Vyote viwili husababisha ufisadi na kudhoofika kwa akili, huku zikiacha hali ya ulegevu, udhaifu, na upotevu wa nguvu katika viungo vya mwili. 3. Uraibu na Utegemezi: Matumizi ya vitu viwili hivi hupelekea mtumiaji kuwa na utegemezi wa kudumu (uraibu). 4. Kuchochea Mawazo Maovu na Uhalifu: Moja ya athari hatari zaidi ni kuwa vyote viwili huibua mawazo machafu na ya kifisadi ndani ya nafsi ya mtumiaji. Mawazo haya mara nyingi hupelekea mtu kutenda jinai na uhalifu mbalimbali katika jamii. 5. [12] Madhara ya Kiafya: Vyote viwili vina athari za moja kwa moja na zenye sumu kwa afya ya mwili na roho ya mtumiaji, zikiathiri mifumo muhimu ya maisha. [13] Ushahidi na Nyaraka za Kisheria Zinazoharamisha Matumizi ya Dawa za Kulevya Ushahidi wa Hadithi za Mtume (s.a.w.w) Bwana Mtume (s.a.w.w) amesema: Fahamuni kuwa kila kileo na kila chenye kulevya (makhadir/kiondoacho mwamko wa akili) ni haramu. (Aidha fahamuni kwamba) chochote kile ambacho wingi wake unalevya, basi hata uchache wake pia ni haramu; na chochote kile kinachovuruga akili, kuchafua, au kuondoa akili ni haramu. [14] Wanazuoni wa sheria ya Kiislamu (mafaqihi) wakitegemea vyanzo vikuu vya sheria, wametoa hoja mbalimbali ili kuthibitish uharamu wa matumizi ya dawa za kulevya. Hoja hizo zimegawanyika katika nyanja tatu kuu: 1. Ushahidi wa Qur'ani Tukufu Mafaqihi wakuu wametumia Aya mbalimbali kama kigezo cha uharamu wa mutumizi ya madawa ya kulevya: • Hoja ya Kujipeleka Kwenye Maangamizi (Tahluka): Ayatullahi Nasir Makarim Shirazi anabainisha kuwa matumizi ya madawa ya kulevya ni moja ya mifano dhahiri ya binadamu kujiingiza katika mtego wa maangamizi, jambo ambalo limekatazwa waziwazi na Qur'ani kupitia Aya isemayo: “وَ لَا تُلْقُوا بِأَیدِیکمْ إِلَی التَّهْلُکةِ” (Wala msijitupe kwa mikono yenu katika maangamizi”. [15] • Hoja ya Uharibifu wa Mali na Utu: Mtafiti wa masuala ya kifiqhi Muhammad Jawad Mehri anafafanua hoja hii akieleza kwamba, biashara na utumiaji wa madawa ya kulevya ni aina ya "kula mali kwa njia ya batili" (akl al-mal bi al-batil). Mtafiti huyu, akitumia Aya inayokataza kujitumbukiza katika maangamizi (Aya ya 195 ya Suratu al-Baqara), Aya inazohusiana na biashara (Aya ya 29 ya Surat an-Nisa), upotezaji mali (Aya ya 27 ya Suratu al-Isra), na Aya inayoharamisha vitu vichafu na viovu (Aya ya 157 ya Suratu al-A'raf), anahitimisha akisema: “Kwa kuwa dawa za kulevya ni mada duni, zenye madhara, chafu, na zenye kufuta uwezo wa akili; hivyo basi ni haramu kuzalisha pamoja na kutumia dawa hizo. [16] 2. Ushahidi wa Hadithi (Riwaya) na Changamoto za Upokezi Yake Katika mchakato wa kuharamisha madawa ya kulevya, baadhi ya mafaqihi wanategemea maudhui ya hadithi zinazotoa huku usawa kati ya kileo na madawa ya kulevya. Miongoni mwa Hadithi hizo ni ile isemayo: "Kila kileo ni haramu na kila kitu chenye kulevya (kipumbazicho akili) ni haramu". [Maelezo 1: ألا إنَّ کلَّ مُسکرٍ حَرامٌ، و کلَّ مُخَدِّرٍ حَرامٌ، و ما أسکرَ کثیرهُ حَرامٌ قَلیلُهُ، و ما خَمَّرَ العَقلَ فَهُوَ حَرامٌ ؛ Al-Kafi, cha Kulaini, juz.6. uk. 408. Toleo la 1407 Hijiria] Aidha wameweza kufikia uharamu huo kwa kutumia kanuni isemayo; kitu chochote kile chenye matokeo sawa na ya vileo (kupoteza akili / kupumbaza akili) ni chenye hukumu sawa na vileo. [Maelezo 2: إنَّ اللّه َ عز و جل لَم یحَرِّمِ الخَمرَ لاِسمِها، ولکنَّهُ حَرَّمَها لِعاقِبَتِها ؛ فَما کانَ عاقِبَتُهُ عاقِبَةَ الخَمرِ فَهُوَ خَمرٌ ؛ Al-Kafi, cha Kulaini, juz.6. uk. 412. Toleo la 1407 Hijiria] [17] • Changamoto Dhidi ya Hoja za Hadithi: Mwanachuoni aitwaye Musawi Ardebili anatoa changamoto ya kitaalamu dhidi ya Hadithi zilizotumika kama hoja na ithimati katika uharamishaji wa matumizi ya madawa ya kulevya. Akibainisha changamoto hiyo anasema kuwa, Riwaya (Hadithi) zilizopo katika vyanzo vya Hadithi ambazo hutumiwa kama ushahidi wa moja kwa moja wa uharamu wa madawa ya kulevya, si Hadithi sahihi kwani zina mapungufu katika mnyororo wa wapokezi (sanad). Kwa msingi huo, haziwezi kuzitegemea hadithi hizo pekee na kuzitumia kama ithibati msingi ya kisheria katika kuthibitisha hoja fulani. [18] 3. Ushahidi wa Kiakili na Mantiki (Aql) Mwanachuoni mashuhuri Sayyid Muhammad Baqir al-Sadr anajenga hoja isemayo kwamba, uharamu wa madawa ya kulevya unaweza kugundulika kupitia akili (aql) bila hata kuhitaji nukuu ya moja kwa moja itokayo katika vyanzo vya sheria. [19] Akithibitisha nadharia hiyo, anatumia kanuni ya mlinganisho (analojia) akisema: Ikiwa akili inatambua kuwa vileo ni haramu kwa sababu vinapoteza utambuzi (welewa) na kuharibu akili, basi kwa mantiki hiyo hiyo dawa za kulevya—ambazo zina athari zilezile za kupoteza fahamu na uwezo wa kufikiri—nazo zitakuwa ni haramu. [20]

Je, Uharamu wa Madawa ya Kulevya Unatokana na Madhara Yaliomo Ndani yake? Wanazuoni wengi wa Kiislamu wanakubali kuwa sababu ya msingi ya uharamu wa dawa za kulevya ni madhara yake makubwa kwa mtu binafsi na jamii. Ingawa kuna tofauti kidogo katika namna wanavyojenga hoja, kiini kinabaki kuwa ni ulinzi wa uhai na akili. 1. Mtazamo wa Ayatullah Nasir Makarim Shirazi Ayatullah Makarim Shirazi anaharamisha madawa ya kulevya kwa kutegemea kanuni ya kifiqhi iitwayo "La-Dharar" (Kutodhuru). Katika kufafanua mtazamo wake anasema: “Ingawa mara nyingi kanuni hii hutumika kuzuia kumdhuru mtu mwingine, ila pia inajumuisha kujidhuru nafsi yako mwenyewe. Kwa vile imethibitika kuwa madawa ya kulevya yanaleta madhara ya wazi kabisa kwa mtumiaji wake pamoja na watu wanaomzunguka, hivyo basi ni haramu kutumia aina kama hiyo ya madawa”. [21] 2. Mtazamo wa Sayyid Muhammad Baqir al-Sadr Kwa mtazamo wa Sayyid Muhammad Baqir al-Sadr ni kwamba; kuna utofauti wa kisheria kati ya vileo na madawa ya kulevya. Kwa mujibu wa mtazamo wake, sababu ya uharamu wa kunywa pombe ni sifa yake ya kulevya (muskir), ilhali sababu kuu ya uharamu wa kutumia madawa ya kulevya ni madhara na hasara inayotokana na madawa hayo. [22] 3. Mtazamo wa Ayatullahi Khui Baadhi ya mafaqihi akiwemo Ayatullahi Khui, wanafananisha madawa ya kulevya na sumu. Wao hujenga hoja yao kwa kutegemea msingi usemao kwamba; ni haramu kwa mtu fulani kutumia chochote chenye madhara kwenye mwili wa mwanadamu, kama vile sumu (iwe ni kiasi kidogo au kikubwa, ngumu au ya majimaji). [23] [24] Wanazuoni hawa -isipokuwa Ayatullahi Khui- wamehalalisha kutumia kiwango kidogo cha madawa (kama vile Afyuni), iwapo kiwango hicho haklitapelekea kwa mtumija wake. Ila ikithibiti tu kwamba utumiaji huo utapelekea madhara ndani yake, jambo hilo litamharamikia mtumiaji huyo. [25] Kwa upande wa Ayatullah Khui, yeye anaamini kuwa utumiaji wa madawa ya kulevya ni sawa na utumiaji wa sumu. Hii ni kwa sababu ya kwamba, utumiaji wa madawa ya kulenya huhatarisha usalama wa afya ya kimwili na kisaikolojia. Hivyo basi yeye ameharamisha moja kwa moja utumiaji wa madawa hayo iwe ni kwa kiwango kidogo au kikubwa. [26] 4. Mitazamo ya Imam Khomeini na Ayatullah Khamenei Imam Khomeini na Ayatullahi Khamenei wameelekezamoja kwa moja jicho lao kwenye maafa na madhara yanayotokana na madawa haya. Hivyo basi wao wameharamisha dawa za kulevya kutokana na madhara binafsi na ya kijamii yanayopatikana ndani yake, kwani uuzaji, usafirishaji, na utumiaji wake unahatarisha mfumo mzima wa jamii. [27] [28] Kigezo na Kiwango cha Madhara ya Madawa ya Kulevya Kuna mjadala kuhusu kiasi gani cha matumizi kinaingia katika hukumu ya haramu: Wanazuoni hawakuharamisha matumizi ya mara moja au mbili ya madawa ya kulevya. Kwa kuwa kigezo cha uharamu wa madawa hayo ni uraibu unaosababishwa na matumizi ya mara kwa mara. [29] Nadharia hii ndiyo iliyowafanya Mafaqihi kama Mirza Jawad Tabrizi, [30] Bahjat, [31] na Fadhil Lankarani [32] wajuzishe baadhi ya hatua za matumizi ya vitu vilivyomo ndani ya orodha ya madawa ya kulevya. Kulingana na mtazamo wa wanazuoni hawa, kigezo cha uharamu ni uraibu wa madawa haya, na sio matumizi ya kiwango cha chini. Hii ni kwa sababu wao wanaamini kwamba, matumizi makubwa yake makubwa ndiyo yaletayo madhara ya uraibu kwa mwanadamu, na hicho ndicho kilichoharamisha na sheria. Hili ndilo lililopelekea wanazuoni kuamini kwamba; Ikiwa mraibu hawezi kuacha ghafla matumizi yake bila kujihatarishia maisha, sheria ya Kiislamu humruhusu kuendelea na matumizi ya kiasi kidogo kwa ajili ya kuhifadhi uhai wake. [33] Adhabu ya Utumiaji wa Dawa za Kulevya Kuna mitazamo tofauti miongoni mwa mafaqihi wa Shia Imamiyya juu ya suala la kwamba, je madawa ya kulevya ni sehemu ya vileo, na kama je hukumu za kijinai za vileo zinazihusu dawa hizo au la. Kilichobainishwa katika vitabu vya kisheria (kifiqhi) ni kwamba hakuna ithibati za kutosha za kuweza kuyahusisha madawa ya kulevya na vileo vyengine, na jambo hili ni suala lenye hitilafu miongoni mwa wanazuoni mbalimbali. Kwa mtazamo na welewa (muono) wa kimila (kijamii), wengi wa mafaqihi hawazichukulii dawa za kulevya kama ni moja ya kileo miongoni mwa vileo mbalimbali vinavyotambuliwa na jamii. Wala hakuna mwanazuoni anayebebesha na kuendesha hukumu mbalimbali za kileo juu ya madawa ya kulevya. [34] Hii ndiyo sababu ya wao kuyahisabu makosa ya utumiaji wa madawa ya kulevya miongoni mwa makosa ya ta’azir (adhabu zinazotolewa kwa hiari ya hakimu au sheria za nchi, ambayo hayana hukumu maalumu kwa mujibu wa sheria za awali za Kiislamu). [35] Mkabili wa kundi hili, baadhi ya mafaqihi wengine wanaona kuwa sababu ya uharamu wa utumiaji wa dawa za kulevya ni asili (sifa) yake ya kulevya. [36] Wao wanaamini kuwa kigezo cha kutoa adhabu ya haddi (adhabu maalum iliyowekwa na sheria ya Kiislamu) kwa dawa za kulevya ni uwezo wake wa kulevya. Kwa mfano, Allamah Hilli, faqihi na mwanatheolojia wa Kishia wa karne ya nane Hijiria, katika kitabu cha Qawa’id al-Ahkam, [37] na Imamu Khomeini, katika kitabu cha Tahrir al-Wasilah, [38] wanaamini kuwa; vileo vya aina yoyote ile—kiwe ni kigumu au cha majimaji—vyote kwa pamoja vinahusishwa na hukumu ya pombe (khamr), kama ilivyo hashishi (bangi). Shahid al-Awwal, mmoja wa mafaqihi wa Kishia wa karne ya nane Hijiria, anaashiria kuwepo kwa mitazamo miwili tofauti ya kitaalamu juu ya sababu ya uharamu wa hashishi pamoja na matokeo ya kisheria yanayojiri kutokana na utumiaji wake. Akifafanua mitazamo hiyo anasema; ikiwa uharamu wake utakuwa ni kwa sababu ya kulevya kwake, basi hukumu ya matumizi yake itakuwa ni adhabu ya haddi (bakora 80 kama ilivyo kwa mwenye kunywa pombe); vinginevyo, ikiwa ni kwa sababu ya kuleta ufisadi (yaani kufisidi na kuharibu akili), basi huku ya matumizi yake itakuwa ni adhabu ya ta’zir. [39] Hukumu ya Uzalishaji, Usafirishaji, na Ufanyaji Biashara ya Dawa za Kulevya Kuna hitilafu miongoni mwa mafaqihi wa Shia Imamiyya kuhusu hukumu ya vitu vyenye kulevya vilivyo katika hali ya ugumu (solid) kama vile bangi. Hitilafu hii inahusiana na usafi (tahara) na unajisi (najasa) wa vitu hivyo, na si katika uhalali wa matumizi yake, kwani wanazuoni wamewafikiana juu ya uharamu wa matumizi ya vitu hivi. Kundi moja la mafaqihi linaamini kuwa mada hizi ni safi (tahir), hata kama zitachanganywa na kitu kingine hadi kuwa katika hali ya kimiminika, bado zinabaki kuwa ni safi. [40] Mkabali wa kundi hili, ni kundi la mafaqihi wanoamini kuwa kila kileo ni najisi, bila kujali kama ni kigumu au kimiminika. [41] 1. Kigezo cha Allamah Hilli: Allamah Hilli, faqihi na mwanatheolojia mashuhuri wa Kishia wa karne ya nane Hijiria, anaamini kuwa kigezo kikuu cha uharamu wa ununuzi na uuzaji wa dawa za kulevya ni uhusishwaji wa mada hizi na vileo (muskirat). Kwa mtazamo wake, kwa kuwa mada hizi zina sifa ya kulevya, basi zinaingia katika hukumu moja na pombe katika nyanja za biashara. [42] 2. Mtazamo wa Wengi wa Mafaqihi: Tofauti na Allamah Hilli, mafaqihi wengi zaidi wameweka kigezo cha uharamu wa usafirishaji na miamala ya dawa za kulevya katika kukosekana kwa manufaa ya halali na yenye tija zithaminikazo mbele ya wenye akili (uqlai), pamoja na kuwepo kwa dhamira ya kupata manufaa ya haramu ndani yake. Wanazuoni hawa wamebainisha kuwa: • Ikiwa shughuli hizi (za kibiashara) zitafanywa kwa ajili ya matumizi ya halali, ikiwa ni pamoja na matumizi ya kitiba (matibabu) na mambo mengine yenye mantiki ya kiakili, basi shughuli hizo zinajuzu na zinaruhusiwa kisheria. Ila ikiwa ni kwa malengo yasio halali basi shughuli hizo zitakuwa ni haramu moja kwa moja. [43] Miongoni mwa mifano ya fatwa hii: ni fatwa ya Sayyid Ali Khamenei isemayo: • Utumiaji wa dawa za kulevya, ununuzi, uuzaji, usafirishaji, na uhifadhi wake ni haramu. Sababu kuu ya uharamu huu ni madhara ya kibinafsi na ya kijamii yanayotokana kutokana na mada hizo. Na wala hakuna ruhusa ya kutumia mada hizi ila tu katika dharura ya matibabu ya ugonjwa, na hiyo ni kwa sharti la mwongozo wa daktari bingwa na mwaminifu. Katika mazingira hayo, matumizi yake yanaruhusiwa kwa kiwango cha dharura tu, jambo ambalo limeruhusiwa kisheria. [45] Kwa mujibu wa fatwa za Ayatullahi Nasir Makarim Shirazi, ni haramu kutumia opiamu na aina nyingine za dawa za kulevya. Pia kwa mujibu wa fatwa zake, ni haramu kufanya biashara ya madawa ya kulevya pamoja na kushiriki katika mikusanyiko inayohusisha matumizi ya dawa hizo, kwani jambo hilo ni miongoni mwa madhambi makubwa ndani ya sheria za Kiislamu. Aidha, fatwa zake zinaharamisha aina yoyote ya msaada unaohusiana na kilimo, uuzaji, usafirishaji au matumizi ya dawa hizo. [46] Kwa mtazamo wake, ni haramu kutoa mchango wa namna yoyote ile katika suala hili, iwe ni katika uzalishaji, uandaaji, usafirishaji au usambazaji. Na yeyote atakayeshiriki moja ya vitendo huwajibika kupata adhabu ya Mungu; vivyo hivyo, mapato yote yatokanayo na shughuli hizo ni haramu na hayana uhalali wa kisheria ndani ya Uislamu. [47] Baadhi ya wanazuoni, kama vile Mirza Jawad Tabrizi (aliyefariki: 1385 SH/2006), wanaamini kuwa kigezo cha uharamu wa dawa za kulevya kipo katika kuenea na kushamiri kwa ufisadi pamoja na uraibu ndani ya jamii. Kwa mujibu wa mtazamo huu, uharamu wake hautokani tu na madhara ya kibinafsi, bali unalenga kuzuia mmomonyoko wa kijamii unaosababishwa na kusambaa kwa uraibu. Kundi jingine la mafaqihi, akiwemo Imamu Khomeini na Sayyid Kadhim Ha’iri (aliyezaliwa: 1317 SH/1938), wameweka kigezo cha uharamu katika uasi dhidi ya taratibu na sheria za serikali ya Kiislamu. Katika mantiki hii ya kisheria, pale serikali ya Kiislamu inapoweka sheria fulani kwa ajili ya maslahi ya umma, kama vile sheria ya kuzuia dawa za kulevya, kupinga sheria hizo kunachukuliwa kuwa ni haramu mbele ya sheria. Uharamu hapa unafungamanishwa na wajibu wa kidini wa kutii kanuni za mfumo wa uongozi wa Kiislamu unaolinda jamii. [48] Je, Wasafirishaji wa Dawa za Kulevya ni Mufisidi katika Ardhi? Dhana ya "Mufsidu fi al-Ardhi" (Mfisadi katika Ardhi) ni mojawapo ya mada nzito katika sheria za Kiislamu, inayorejelea mtu anayefanya uharibifu mkubwa unaotishia usalama na maadili ya jamii. Baadhi ya mafaqihi wanawachukulia wasafirishaji wa dawa za kulevya na wale wanaofanya jitihada kubwa za kuanzisha vituo vya ufuska kuwa ni mifano kamili ya dhana ya "Mufsidu fi al-Ard" (kwa Kiswahili: Mfisadi au Fisadi katika Ardhi). Kwa mfano, Nasir Makarim Shirazi akifafanua dhana ya mfisadi katika ardhi anasema: "Mfisadi katika ardhi ni mtu anayekuwa chanzo cha ufisadi ulienea katika mazingira fulani; hata kama atafanya hivyo bila kutumia silaha; kama vile wasafirishaji wa dawa za kulevya na wale wanaounda vituo vya ufuska kwa kiwango kikubwa. [49] Katika muktadha wa kisheria wa kuhusisha makosa ya dawa za kulevya na makosa ya ufisadi katika ardhi, Imam Khomeini anabainisha kuwa kigezo cha "ufisadi katika ardhi" hufikiwa pale usambazaji wa mada hizo unapoleta janga la uraibu mkubwa kwa umma, huku kukiwa na nia ovu au elimu ya awali juu ya athari zake. [50] Katika mawasiliano yake rasmi na Mkuu wa Diwani Kuu ya Nchi, Sayyid Abdul-Karim Musawi Ardebili (1925–2016 AD), kuhusu uainishaji wa adhabu ya kifo kwa wahalifu hao, Imamu Khomeini alielekeza matumizi ya ijtihadi ya Hussein-Ali Montazeri (1301–1388 SH) katika utekelezaji wa huku hizo. Msimamo wa Montadhari unaruhusu adhabu ya kifo kwa mafisidi, lakini unaweka zuio la adhabu hiyo endapo kutakuwa na utata na shaka juu ya kuthibiti sifa ya mfisadi kwa mhusika wake. Hii ni kwa mujibu wa kanuni ya kifiqhi ya "Ihtiyat fi al-Dima" (Tahadhari katika Damu) [53] Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kupitia vifungu vya 6 na 9 vya Sheria ya Kupambana na Dawa za Kulevya iliyopitishwa mwaka 1988 AD, mtunga-sheria aliwapa hadhi ya 'Mufisidina fil Ardhi' (Mharibifu mkuu katika nchi) wahalifu wote wa dawa za kulevya ambao shehena zao zinafikia kiwango maalum cha kisheria. Hata hivyo, baada ya kipindi cha mabadiliko ya hadhi hiyo ('Mufisidi katika Ardhi) katika kifungu cha 6 cha sheria hiyo mnamo mwaka 1997 AD, mtunga-sheria alirejea tena mwaka 2017 AD na kufanya mabadiliko mapya kwa kuongeza Kifungu cha 45. Kifungu hicho kiliainisha bayana vigezo (vya masadiqi) vinavyomfanya mtenda-jinai wa dawa za kulevya kuhesabiwa kuwa ni miongoni mwa mafisadi katika ardhi. [54]