Kuvunja Ibrahim masanamu

Kutoka wikishia

Kuvunja Masanamu Ibrahim (Kiarabu: تحطيم إبراهيم للأصنام) kunaashiria tukio la Nabii Ibrahim (a.s) kuvunja masanamu ya washirikina. Mkasa huu umetajwa na kuelezwa katika Qur'ani katika Sura ya Anbiya na Saffat. Kwa mujibu wake ni kuwa, siku moja watu waliondoka na kwenda nje ya mji. Nabii Ibrahim akaenda katika jumba la masanamu na akayavunja masanamu yote isipokuwa sanamu kubwa kuliko yote. Baada ya watu kurejea na kumuuliza sababu ya kuvunjwa masanamu. Ibrahim akasema kwa kinaya kwamba aliyefanya hilo ni sanamu mkubwa na akasema, yaulizwe masanamu mengine.

Ibrahim alisema hivyo akiwa na nia ya kuwatanahabahisha watu ili wazinduke kuhusiana na uwezo wa masanamu hayo. Wafasiri wanasema kuwa, nia ya Ibrahim ilikuwa ni kuonyesha kwamba, masanamu hayana uwezo wa kuzungumza wala hayana uwezo wa kumdhuru wala kumnufaisha mtu, na kwa msingi huo hayastahiki kuabudiwa. Kadhalikka wanasema kuwa, lengo la Ibrahim halikuwa kuvunja tu masanamu ili kitendo chake hicho kihesabiwe kuwa ni kuvunjia heshima itikadi za wengine, la hasha! bali akiwa katika daraja ya Utume, Nabii Ibrahim (a.s) kupitia hili alitaka kupambana na utamaduni wa kuabudu masanamu.

Kisa cha Kuvunjwa Masanamu

Kisa cha kuvunjwa masanamu yaliyovunjwa na Nabii Ibrahim (a.s) kimesimuliwa na kuzungumziwa katika Surat al-Anbiya (Aya ya 52-70) na Surat Saffat (Aya ya 89-98). Mkasa huu umesimuliwa namna hii katika Surat al-Anbiya:

Siku moja watu waityoka na kwenda nje ya mji, Ibrahim akayavunja masanamu yote isipokuwa kubwa lao. Wakati waliporejea wakakutana masanamu yao yamevunjwa. Kutokana na kuwa huko nyuma Ibrahim alikuwa akiyasema kwa ubaya masanamu hayo ambayo ni miungu wa washirikina, walimuendea na kumuuliza, je wewe ndiye uliyefanya hivi kwa miungu wetu? Ibrahim akajibu: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Kwa swali hili, wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu; pamoja na hayo wakawasha moto kwa ajili ya kumuadhibu Ibrahim na kisha wakamtupia ndani ya moto; hata hivyo kwa amri ya Mwenyezi Mungu moto ule ukawa baridi na usiounguza. [2]

Baadhi ya wafasiri wamesema, kufuatia tukio na mkasa huu kwamba, idadi kadhaa ya watu walijitokeza na kumuamini Ibrahim na mafundisho aliyokuja nayo. [3]

Lengo la Ibrahim la Kuvunja Masanamu; Kuthibitisha Tawhidi

Sababu ya kuvunja masanamu na kunasibisha kitendo hicho na sanamu kubwa kuliko yote imetambuliwa kuwa, Ibrahim alilenga kupitia hatua hii kufanya mdahalo na waabudu masanamu na kubatilisha uungu wa masanamu na kupitia kudhalilishwa na kudunishwa miungu wao, watu wazinduke na kufahamu kwamba, masanamu hayo hayastahiki kuabudiwa kwani hayawezi kumnufainisha mtu wala kumdhuru na hata hayawezi kujilinda. [4]

Wamebainisha hoja ya Nabii Ibrahim namna hii kwamba, vipi kitu ambacho hakidhuru wala kunufaisha kinaabudiwa? [5] Allama Tabatabai anasema kuwa, Ibrahim al-Khalil (a.s) alikinasibisha kitendo cha kuvunjwa masanamu na sanamu kubwa zaidi ili kwa njia hiyo watu wakiri wenyewe kwamba, masanamu hayaongei. [6] Ameandika: Jambo la lazima la kutoweza kuzungumza masanamu ni kuwa, hayana nguvu wala elimu yoyote na kwa msingi huo hayana manufaa wala madhara yoyote. Kwa muktadha huo, kuyaabudu ni jambo lisilofaa, kwani ibada ima ni matumaini ya kupata kheri au woga wa shari, na kwa masanamu hakuna matumaini ya kheri wala woga wa shari. [7] Imekuja katika Tafsiri ya Kashif kwamba: Wakati masanamu hayana hata uwezo wa kujilinda na kujitetea, vipi yanaweza kuzuia mambo mabaya yasiwapate na kuwakumba watu wengine. Kwa maana kwamba, vipi yanaweza kuwalinda wengine wasimbukwe na mambo mabaya ilihali yenyewe hayana hata uwezo wa kujilinda na kujitetea? [8]

Murtadha Mutahhari anaamini kuwa, Ibrahim alinasibisha uvunjaji masanamu kwa sanamu kubwa lao kwa ishara kwamba, kulizuka ugomvi baina ya masanamu hayo, ili kwa njia hiyo aweze kuamsha fitra ya ndani ya watu; kwani kifitra na kimaumbile watu wanadiriki kwamba, haiwezekani vitu vikapigana. [9]

Je, Ibrahim Alisema Uongo?

Imekuja katika simulizi ya Qur’an kuhusiana na Ibrahim kuvunja masanamu kwamba, wakati walipotaka kutoka nje ya mji, Ibrahim alisema yeye ni mgonjwa ili asifuatane nao. [10] Kadhalika wakati alipoulizwa ni nani aliyevunja masanamu haya, alijibu ni sanamu kubwa. [11] Mambo haya mawili yamewafanya wafasiri wawe na mjadala wa kwamba, je, Ibrahim alisema kweli au alisema uongo wa maslahi au alifanya Tauriyah (alificha makusudio na kudhihirisha kitu kingine):

Wafasiri Waislamu wanaamini kuwa, Ibrahim hakusema uongo kuhusiana na kuwa yu mgonjwa; [12] lakini kumetolewa uwezekano na ufafanuzi tofauti kuhusiana na hili ambao ni: Tabarsi na Allama Tabatabai wanasema kuwa: Ibrahim alikuwa akitambua kuwa, ataumwa muda si mrefu. Hivyo alisema kweli. [13] Alusi mfasiri wa Qur’ani wa Kisuni anaamini kuwa, kwa kuwa kila mtu kuna siku ataumwa, Ibrahim alisema anaumwa na makusudio yake yalikuwa kwamba, ataumwa. Hivyo basi, Ibrahim alificha makusudio yenyewe na kubainisha maneno yake kwa namma ambayo washirikina wakadhani kuwa, hivi sasa yu mgonjwa. [14] Uwezekano mwingine uliozungumziwa ni kwamba, makusudio yake kwa hakika yalikuwa kwamba, moyo wake ni mgonjwa kunako ukafiri wao; lakini alificha makusudio na kuzungumza kwa namna ambayo washirikina walidhani kwamba, mwili wake unaugua. [15]

Kadhalika wamesema: Hii kwamba, Ibrahim amekinasibisha kitendo cha kuvunjwa masanamu na sanamu kubwa hakusema uongo; kwani kwa kuzingatia ishara, hakukusudia kusema kwa dhati kupitia maneno yake hayo; bali alizungumza kwa kinaya na ishara ili kupitia kauli yake hiyo aonyeshe na kuthibitisha juu ya kutokuwa sahihi kuabudu masanamu. [16] Kuzungumza kwa kinaya ni jambo lililozoeleka katika midahalo. [17] Baadhi ya watu pia wamejaalia uwezekano huu kwamba, Ibrahim alizungumza maneno hayo kwa senyenti yenye sharti na alisema, kama yatazungumza, basi yatakuwa yamefanya kitendo hiki. [18] Kimsingi ni kuwa, Ibrahim alizungumza maneno yake na kuweka sharti la muhali, ili athibitishe kubatilika madai yao ya kuabudu masanamu. [19]

Kuvunja Masanamu Ibrahim na Uhuru wa Itikadi

Baadhi ya watafiti wamedai kwamba, hatua ya Ibrahim (a.s) ya kuvunja masanamu ya washirikina ilikuwa ni kuvunjia heshima matukufu ya wengine. Kwa msingi huo, Waislamu wanaweza kushikamana na kitendo hicho na hivyo kuangamiza athari za kale za washirikina. [20] Katika kujibu madai haya imeelezwa kuwa: Mali na roho za watu wote ni zenye kuheshimiwa na haiwezekani kuvunja masanamu ya wengine ambayo yanahesabiwa kuwa ni mali yao. Ibrahim alifanya hilo akiwa katika nafasi na cheo cha Utume na katika jukumu lake la kufikisha risala yake na watu wengine hawapaswi kuhujumu mali za wengine. [21] Baadhi ya wengine pia wamesema: Uhuru wa itikadi na dini ni katika itikadi za zama za leo na haiwezekani kulinganisha na kiwango cha zama za huko nyuma na matukio yake. [22]

Kwa msingi huo, wafasiri wanasema, kitendo cha Ibrahim cha kuvunja masanamu kililenga kubatilisha uungu wao na lengo lake lilikuwa ni kupambana na utamaduni wa kuabudu masanamu na sio kuvunja tu manasamu. [23]