Kujiona (Kiarabu: العجب) ni miongoni mwa tabia mbaya za kimaadili. Kujiona maana yake ni mtu kufurahishwa na amali na matendo yake mema na kuyakuza, kwa sura ambayo mja ahisi na kujua kwamba hivyo vinatokana na yeye (au uhodari wake) na sio kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Katika elimu ya maadili (akhlaq), mambo kama madaraka, uzuri na ujamali, nasaba na wingi wa watoto ni miongoni mwa sababu za kujiona pia, na ni chimbuko la kubatilika amali njema. Kiburi na kuharibika kwa akili inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa athari na natija zake.

Wataalamu wa masuala ya maadili, wanaona kwamba; kujiona kunatokana na ujinga na wanaamini kuwa kujiona kunaweza kutibika na kuondolewa kwa kuwa na ufahamu na maarifa (sahihi). Hali kadhalika wanaamini kwamba, ubaya huu wa kimaadili ni lazima utibiwe na kumalizwa kwa njia ya kuondoa sababu na mizizi yake.

Maana ya kujiona

Kujiona ina maana ya (mtu) kujikuza, kujikweza na kuwa na furaha kutokana na matendo yake mema kwa sharti ya kwamba mtu asahau kumnasibisha Mwenyezi Mungu katika matendo hayo. Naye aone kwamba matendo hayo mema yanatokana yeye (uwezo na uhodari wake) na asiwe na hofu ya kubatilika na kuharibika kwa matendo yake hayo [1]. Hata hivyo Mulla Ahmad Naraqi ametaja kwamba, kujiona ni mtu kujikweza na kujiona kwamba ni mkamilifu [2].

Uhusiano wa kiburi na ufakhari

Kujiona ina maana ya karibu mno na kiburi, tofauti baina ya haya matendo mawili ni kwamba; katika hali ya kujiona, mtu hajilinganishi na watu wengine lakini katika hali ya kiburi mtu hujilinganisha na wengine na kujiona bora na wa juu zaidi ya wengine [3]. Kuhusiana na utofauti baina ya kujiona na kujifakharisha inaelezwa kwamba, kujiona ni kukuza amali na matendo mema na kumfanyia masimbulizi Mwenyezi Mungu kwa njia ya kufanya baadhi ya matendo na ibada. Ama katika hali ya kujifakharisha pamoja na hayo, ni kwamba mwanadamu anajiona ni mwenye kustahiki haki (daima) ambapo kutokana na hali hiyo, anakuwa hana hofu wala woga [4].

Chimbuko

Wataalamu wa elimu ya maadili wamebainisha chimbuko, sababu na misukumo mbali mbali inayopelekea (mtu kuwa) na tabia (mbaya) ya kujiona. Feidh Kashani katika kitabu cha Al- Mahajjatul- Baydha anasema kwa kubainisha kwamba; ujamali na uzuri, nguvu na uwezo, ujanja na akili, nasaba na familia, kuwa katika ukoo wa kifalme na wenye nguvu (kisiasa, kifedha), wingi wa watoto, mali na utajiri, kuwa mwenye fikra na tafakari, ni miongoni mwa sababu za kujiona [5]. Wataalamu hao wa masuala ya kimaadili na tabia katika kuweka wazi zaidi maana ya kujiona, wametumia Aya tukufu za Qur’an zifuatazo: وَ یوْمَ حُنَین اذْ اعْجَبَتْکمْ کثْرتُکمْ: [6]

Na siku ya Hunayni ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, Aya ya 2 ya Suratul- Hashr na katika Aya ya 104 ya Surat al-Kahf ya kwamba Aya hizi zina uhusiano na zimetaja maudhui ya kujiona [7]. Naraqi amesema kwamba; hakika kujiona katika ibada, kunapingana na falsafa ya wale ambao wanadhihirisha udhalili na unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Matokeo

Natija na athari za kujiona zimebainishwa katika riwaya kama ifuatavyo:

  • Kuharibu amali na maetendo mema (ya mja). Mtume Muhammad (s.a.w.w) amepokelewa akisema kwamba: (Hakika tabia ya) kujiona inaharibu na kubatilisha matendo mema ya mwanadamu ya miaka 70 [9].Hali kadhalika kuna hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Imam Swadiq (a.s) ambayo inasema kwamba:

Watu wawili waliingia msikitini, ama wakati walipokuwa wakitoka kutoka msikitini! Mtu fasiki na muovu akawa mwenye kuabudu na mtu wenye kuabudu akawa ameshakua muovu. Hiyo ni kwa sababu mtu mwenye kuabudu alipokuwa msikitini alifikwa na hali ya kujiona na akawa anavutiwa na ibada yake. Ama mtu muovu (alipokuwa mskitini) alikuwa hatika fikra ya kufanya toba na alikuwa akifanya Istighfari (akiomba msamaha) [10].

  • Kiburi; (yaani kuwa na takaburi); kujiona ni miongoni mwa sababu za kuwa na kiburi [11].
  • Kusahau au kudumisha madhambi.
  • Kukuza matendo mema, kukuza ibada na kumfanyia Mwenyezi Mungu masimbulizi [12].

Katika riwaya imekuja na kubainishwa kwamba; kuharibika kwa akili [13] na hekima [14], Kuangamia [15] kuwa mpweke [16], ni miongoni mwa matokeo na athari za kujiona. Hali kadhalika imetajwa kwamba: Kujiona ni kizuizi cha kutokuongezeka maarifa na elimu kwa mtu [17], na pia ni kizingiti cha mtu kutofikia ukamilifu mbali mbali unaotakikana [18]. Kwa mujibu wa hadithi ambayo imetajwa katika Nahjul- Balagha ni kwamba: Dhambi ambayo inamuhuzunisha mwanadamu (mtendaji wake) au kumfanya ajutie na kuomba msamaha ni bora zaidi kuliko amali na matendo mema ambayo yanamfanya awe na hali ya kujiona. [19]

Tiba

Feidh Kashani anatambua kwamba kujiona ni maradhi (ya nafsi) ambayo sababu yake ni ujinga na kutokujua. Mwanazuoni huyu anaamini kwamba kila maradhi yanaweza kutibika kwa njia ya (kutumia) dhidi yake, hivyo anaitakidi kwamba kujiona pia kunaweza kutibika kwa kuwa na elimu (ufahamu) na maarifa [20]. Feidh kashani na baadhi ya wengine miongoni mwa maulamaa wa masala ya akhlaq na elimu ya maadili wanaamini kwamba, ili kutibu na kuonda tabia mbaya ya kujiona, inatakikana kuchunguza na kuzingatia sababu na mizizi yake. Ikiwa sababu na chanzo (mtu) kujiona ni moja katika neema za Mwenyezi Mungu kama vile ujamali, nguvu (uwezo) na wingi wa watoto, binadamu katika nukta hii anatakiwa azinduke na kujua kwamba: Mwenyezi Mungu (ndiye) ambaye amempa nguvu na uwezo huo, (hivyo basi) katika sekunde moja ya kufumba jicho na kufumbua anaweza kumnyang'anya. (Mwenye neema na kujiona)! Achukue mafunzo na mazingatio katika historia, kwa watu ambao historia inaonyesha kwamba walikuwa na neema kama hizo, na hawakuzitumia katika njia sahihi. (Naye mwenyezi Mungu aliwafaya kuwa somo na mazingatio kwa kuwanyang'anya neema hizo au kuwaadhibu kutokana na ya matumizi yao mabaya). Kwa mfano: Ikiwa kujiona kwa mtu kunatokana na nguvu na uwezo alio nao, basi na atizame na kuzingatia ukubwa na uwezo wa Mwenyezi Mungu na pia atizame na kutafakari katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu (na hasa) jinsi alivyo muumba mwanadamu! Afahamu ameumbwa kutokana na nini. Hali kadhalika ikiwa kujiona kwake kunasababishwa na kuwa mwenye fikra, tiba yake ni kwamba daima awe ni mwenye kuyatuhumu maoni yake, isipokuwa pale tu atakapokuwa na dalili isiyo na shaka kutoka katika Qur’an au hadithi ambayo itatoa ushahidi wa mazungumzo na maoni yake. Hali kadhalika (ili kujitibu kutokana kujiona mtu anatakiwa) ashauriane na watu wenye ujuzi na elimu katika uwanja huu. [21]. Kwa mujibu wa wasia wa Imam Muhammad Baqir (a.s) kwa Jabir bin Yazid Ju’fi ni kwamba: Kwa kuitambua nafsi, inapasa kufunga njia ya kujiona [22]. (Yani ili afunge mlango wa kujiona anapaswa kuijua nafsi yake).

Rejea

Vyanzo