Khasifun-Na'al (Lakabu)

Khasifu Al-Na’al (Kiarabu: خاصِفُ النَّعْل) (Mkarabati Viatu au Mfungafunga Viatu), ni moja ya lakabu za Imam Ali (a.s), ambaye ni Imamu wa kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ulimwenguni. [1] Lakabu hii imetokana na Hadithi inazojulikana kwa jina la Hadithi ya Khasifun-Na’al, ambayo kwa mujibu wake; Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndiye aliyemwita Imamu Ali (a.s) kwa jina hili, jina ambalo alipewa pale alikuwa akirekebisha na kufungafunga au kutia viraka viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w). [2]
Neno khasafa linamaanisha kukusanya au kuunganisha pamoja vitu fulani. [3] Na yule mtu anayekusanya vipande vya viatu na kuvirekebisha ili viungane na kurejea katika hali yake ya awali, huitwa Khasifun-Na’al. [4] Kile kitendo cha Imamu Ali (a.s) cha kurekebisha na kutia viraka viatu vya bwana Mtume (s.a.w.w), kimeonekana kuwa ni miongoni mwa ishara za unyenyekevu wake, [5] na ni kielelezo kinachoashiria hali ya maisha ya kawaida aliyokuwa akiishi Imamu Ali (a.s). [6]
Kila moja miongoni mwa Hadithi za bwana Mtume (s.a.w.w), zinazomtaja Imam Ali (a.s) kwa lakabu ya Khasifun-Na’l, zinaonekana kumsifu Imamu Ali (a.s) kwa mbalimbali. Miongoni mwa sifa zake (a.s) alizosifiwa ndani ya Hadithi hizo, ni pamoja na sifa ya uongozi wake (Uimamu) na ukhalifa wake, pamoja na vita alivyopigana dhidi ya washirikina na madhalimu mbali mbali. [7] Hadithi hizi zinapatikana katika vyanzo vya awali vya hadithi za upande wa madhehebu ya Kishia, vikiwemo vitabu vinavyojulikana kwa jina la Al-Kutub Al-Arba’a. [8] Pia Hadithi hizi zinapatika katika vitabu maarufu vya Hadithi za upande wa madhehebu ya Kisunni, kama vile; Sihah Al-Sitta, [9] Musnad bin Hanbal, [10] na Sunan Annasaai. [11] Wanazuoni wa Hadithi kutoka madhehebu ya Kishia pamoja na Kisunni, wanakubalia na usahihi wa baadhi ya Hadithi hizi na huzizingatia Hadithi hizo kuwa ni miongoni mwa Hadithi zenye kuaminika. [12] Baadhi ya wanazuoni wa madhehebu ya Shia, kama vile; Sharafuddin na Kaashifu Al-Ghita, wanasema kuwa: Hadithi hizi ni zenye sifa ya mapokezi yenye kiwango cha mutawatir (yaani, zimepokewa kwa wingi kupitia matabaka mbali mbali ya wapokezi wa Hadithi). [13]
Moja ya hadithi hizo, ambayo ianpatikana katika vitabu vya Hadithi za Kishia pamoja na Kisunni, ambayo inaeleza ya kwamba; Bwana Mtume (s.a.w.w) alimwita Imamu Ali (a.s) kwa lakabu ya Khasifun-Na’l, ni ile Hadithi iliyokuja ikisema kwamba: Pale bwana Mtume (s.a.w.w) alipokuwa katika mkusanyiko wa masahaba zake, alisema: «إِنَّ مِنْکمْ مَنْ یقَاتِلُ عَلَی تَأْوِیلِ هَذَا الْقُرْآنِ کمَا قَاتَلْتُ عَلَی تَنْزِیله ; Hakika miongoni mwenu, kuna mmoja atakayepigana kwa ajili ya kufasiri Qur’ani hii (kwa ajili ya kufikisha tafsiri sahihi ya Qur’ani), kama nilivyopigana kwa ajili ya kushushwa kwake (kwa ajili ya kuufikisha ujumbe ulioshushwa na Qur’ani)». Baadhi ya waliokuwepo wakamuuliza kama jee wao ndio mtu huyo aliyetajwa na bwana Mtume (s.a.w.w). Baada ya bwana Mtume (s.a.w.w) kwapa jawabu hasi juu ya swali lao, aliwatambulisha mtu huyo kwao, akiwaambia kuwa; Mtu huyo ni yule aliyekuwa akimshonea au akimtilia viraka viatu vyake (s.a.w.w). Wakati huo, Imam Ali (a.s) alikuwa akiungaunga viatu vya bwana Mtume (a.s). [14]