Khasais al-Nabi (s.a.w.w)

Kutoka wikishia

Makala hii inahausiana na maana na mafuhumu ya Khasais al-Nabi (Sifa na mambo maalumu ya Mtume) Ili kuona orodha ya vitabu vya Sifa maalumu za Mtume (s.a.w.w) soma Makala ya Khasais al-Nabi (vitabu)

Khasais al-Nabi au Ikhtisasat al-Nabi inaashiria sifa maalum na huuumu maalumu zinazomhusu Mtume Muhammad (s.a.w.w), sifa ambazo zinamtofautisha yeye na Waislamu pamoja na Mitume wengine.

Katika fikihi Khasais al-Nabi inaelezwa kuwa ni sifa na mambo maalumu ya Mtume au hukumu zinazomhusu tu Mtume. Hata hivyo neno hili katika matumizi jumla linarejea kwa sifa zote ambazo zinamhusu Bwana Mtume tu na mafundisho yake.

Sifa na mambo maalumu yanayomhusu Mtume yamegawanywa katika katika anuani nne ambazo ni mubaha, haramu, wajibu na karamaat (sifa, mambo na hukumu ambazo watu wanapaswa kuzingucha kuhusiana na Mtume). Baadhi ya sifa na mambo maalumu ya Mtume ni, kuruhusiwa kuoa zaidi ya wake wanne wa ndoa ya daima, kuwa wajibu kwake Sala ya usiku, kuharamishiwa kupokea sadaka, kuharamishwa kunyanyua sauti juu ya sauti ya Mtume, kuharamishwa kuoa wake za Mtume na kuwa kwake ni Mtume wa mwisho yaani hitimisho la Utume.

Utambuzi wa maana

Katika fiqhi, Khasais al-Nabi (sifa na mambo maalumu ya Mtume (saww) huelezwa zile sheria ambazo zimetungwa kwa ajili ya Mtume tu [1] na hivyo kuwa sababu ya kumtofautisha yeye na Umma wake. [2] Hata hivyo neno hili katika matumizi jumla linarejea kwa sifa zote ambazo zinamhusu Bwana Mtume na kumtofautisha yeye Waislamu pamoja na Mitume wengine. [3] Khasais ni wingi wa neno Khasisah ambalo lina maana ya sifa maalumu ambazo zinamtofautisha mtu na wengine. [4]


Kukithiri sifa

Katika vyanzo vya Kiislamu kumetajwa sifa nyingi na mambo mengine ambayo ni maalumu kwa Mtume (s.a.w.w). Kwa mfano katika kitabu cha al-Khasais al-Kubra kilichoandikwa na Suyuti, kumetengwa takribani milango 570 kwa ajili ya maudhui hii. [5] Hata hivyo, Muhaqqiq Karaki anasema kuwa, ilikuwa ni ada na mazoea ya mafakihi kuzungumzia sifa na mambo maalumu ya Mtume katika katika vitabu vya fikihi katika maudhui ya nikaha; kwa sababu akthari ya sifa na mambo yake maalumu yanahusiana na mada ya ndoa. [6] Hata hivyo, wingi wa sifa maalumu zilizonukuliwa kutoka kwa Mtume kumewafanya Maulamaa wa Kiislamu hususan wanazuoni wa Kisuni kuandika athari za kujitegemea kuhusiana na maudhui hii. Kitabu " al-Khasais al-Kubra cha Sheikh Jalal al-Din Syuti (aliaga dunia 911 Hijria) mwanazuoni na msomi wa Kisuni na Khasaid al-Nabi cha Ahmad bin Muhammad bin Daul Qummi alimu na mwanazuoni wa Kishia (aliaga dunia 350 Hijria) [7] ni miongoni mwa athari hizo. Kadhalika angali: Khasaid al-Nabi (vitabu).

Mgawanyo

Katika fikihi sifa, hukumu na mambo maalumu tu kwa Mtume yamegawanywa na kuwekwa katika anuani nne za Mubaha, wajibu, haramu na karamaat (sifa, mambo na hukumu ambazo watu wanapaswa kuzingucha kuhusiana na Mtume). [8] Katika baadhi ya vyanzo mambo ya haramu na ya wajibu yametajwa kwa anuani ya taghlidhat na mambo ya muhaba yametajwa kuwa ni takhfifat. [9]

Mambo ya mubaha

Baadhi ya mambo ya mubaha (ruhusa) ya Mtume ni:

. Kuoa zaidi ya wake wanne kwa ndoa ya daima. [10]

. Nikaha kwa hibah (Mwanamke mwenyewe kujitoa bure kwa Mtume). [11]

. Kufunga nikaha katika hali ya ihramu. [12]

. Kutochunga ugawaji wa siku za kulala baina ya wake zake [13]. Haki ya kugawa siku ni hukumu ya kisheria ambayo kwa mujibu wake, kila mwenye mke zaidi ya mmoja ni wajibu kwake kuitekeleza nayo ni kugawa siku za kulala kwa wake zake. [14]

. Kuingia Makka bila ya vazi la ihramu. [15]

. Saumu ya Wisal, [16] (nayo ni kufunga Saumu siku moja bila ya kufuturu na kuunganisha na siku ya pili au kuendelea na Saumu mpaka wakati wa kula daku. [17]

. Kupigana vita katika Haram ya Makka wakati wa Fat'h Makka. [18]

. Kuoa bila ya mwafaka wa Walii wa mke na ushahidi wa mashahidi. [19]

. Kutumia uturi katika hali ya Ihramu. [20]

. Kutumia vyakula na vinywaji vya Waislamu kwa ajili ya kuokoa roho yake kwa kutegemea Aya ya: Nabii ni bora zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. [21]

Mambo ya haramu

Kwa mujibu wa vyanzo vya Shia na Sunni, baadhi ya mambo ambayo ni haramu kwa Mtume tu ni:

. Kuoa makanizi na Ahlul-Kitab kwa tamko la aqd. [22]

. Kubadilisha au kuongeza wake baada ya kushuka Aya ya 52 ya Surat al-Ahzab, [23] ambayo inasema:

Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala kuwabadilisha kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza; isipo kuwa yule uliye mmiliki kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu.

. Zaka na sadaka kwake na Aali zake. [24]

. Kuandika. [25]

. Kutunga mashairi [26] na kufundisha hilo. [27]

. Kuvua vazi la vita au kuweka kando zana za vita kabla ya kukutana na adui. [28]

. Kuashiria kwa jicho katika mambo ya mubaha kama vile kutoa amri kwa ishara ya jicho. [29]

Mambo ya wajibu

Kwa mujibu wa vyanzo vya Shia na Sunni, baadhi ya mambo ya wajibu ambayo ni makhsusi na maalumu tu kwa Bwana Mtume (s.a.w.w) ni:

. Kupiga mswaki. [30]

. Kusali Sala ya Witr. [31]

. Kuchinja. [32]

. Tahajjud (kuamka usiku kwa ajili ya kusali Sala ya usiku). [33]

. Kutaka ushauri katika mambo [35]. Kwa mujibu wa Abul Hassan Mawardi mmoja wa mafakihi wa Ahlu-Sunna (aliaga dunia 450 Hijria) ni kwamba, kkuhusiana na kuwa ni mambo gani ambayo Mtume anapaswa kuomba ushauri kuna hitilafu.

Baadhi wanasema kuwa, hilo ni makhsusi katika vita na kumshinda adui. Baadhi ya wengine wanasema kuwa, kuomba ushauri huko kunahusiana na masuuala ya kidunia na kidini na kwa mtazamop wa baadhi, hilo linahusiana tu na masuala ya kidini ili watu wajue sababu ya hukumu na mbinu za ijtihad. [36]

Karamaat

Makusudio ya karamat ni sifa zingine maalumu za Mtume na hukumu ambazo Waislamu wanapaswa kuzichunga kuhusiana na Mtume tu. Baadhi ya karamaat hizo ni:

1. Kupewa wake za Mtume lakabu ya Amirul-Muumina. [37]

2. Haramu kuwaoa wake za Mtume baada ya kuaga kwake dunia. [38]

3. Kutonyanyua sauti juu ya sauti ya Mtume (s.a.w.w). [39]

4. Kutoruhusiwa kuondoka katika kikao ambacho Mtume yupo bila ya idhini na ruhusa yake. [40]

5. Kuruhusiwa anayeswali kumsalimia Mtume: Kufanya hivyo hakubatilishi Sala. [41]

6. Kipaumbele cha kulinda na kuhifadhi uhai wa Mtume kwa waumini (kama mtu amekusudia kumuua Mtume, Waislamu waliopo wanapaswa kuwa tayari kujitolea maisha yao ili kumuokoa Mtume. [42]

7. Kuwafanya maadui waingiwe na hofu kuhusu Mtume. [43]

8. Kuwa Mtume wa mwisho. [44]

9. Qur’ani kuwa ni ya milele.


Hekima ya sifa na mambo ambayo ni maalumu kwa Mtume (s.a.w.w)

Baadhi ya Maulamaa wa Kiislamu wamebainisha baadhi ya hekima kuhusiana na uwepo wa hukumu, sifa na mambo maalumu kwa ajili ya Mtume ambapo miongoni mwazo ni: Hekima ya mambo ya wajibu ambayo ni makhsusi kwa Mtume ni kwa ajili ya kuongeza daraja yake ya kimaanawi [46] na hekima ya mambo ya haramu ni kumtakasa yeye na mambo hayo. [47] Kadhalika hekima ya mambo ya mubaha ni kuongeza mamlaka ya Mtume na hekima ya karamaat (sifa, mambo na hukumu ambazo watu wanapaswa kuzingucha kuhusiana na Mtume) ni kumfanya azingatie daraja yake. [48]