Nenda kwa yaliyomo

Istikhara

Kutoka wikishia

Istikhara (Kiarabu: الاستخارة)ni kuomba kheri na kukabidhi uchaguzi wa jambo kwa Mwenyezi Mungu wakati inapotokea kwamba, mtu ameingiwa na shaka juu ya jambo fulani na kheri na shari ya jambo hilo hawezi kuainisha kwa kushauriana na watu. Kwa maneno mengine ni kwamba, istikhara ni kuomba muongozo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuhusiana na jambo fulani ambalo mtu amekwama na kuingiwa na shaka kwamba, alifanye au asilifanye. Istikhara inaweza kufanywa kwa sura na namna tofauti kama vile kufanya isitikhara kwa Sala, dua, kwa kutumia Qur’an, tasbihi na karatasi. Maulamaa wa dini wamejuzisha kisheria suala la kufanya istikhara wakitumia hadithi mbalimbali. Shekhe Abbas Qomi, amebainisha katika kitabu chake cha Mafatihul-Jinan baadhi ya aina na mbinu za kufanya istikhara. Hata hivyo kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kila jambo lina adabu zake na istikhara pia ina adabu zake. Miongoni mwa adabu za kufanya istikhara ni: Kusoma sura miongoni mwa sura za Qur’ani, kumswalia Mtume (saww) na Ahlul-Bayt wake, na kusoma dhikri maalumu.

Allama Majlisi anasema, asili ni kwamba, kila mtu afanye istikhara yeye mwenyewe; licha ya kuwa baadhi ya wanazuoni wa dini wanaamini kwamba, inajuzu pia mtu kuwarejea wengine kwa ajili ya kufanya istikhara, kwa maana kwamba, afanyiwe istikhara na mtu mwingine, kama ambavyo hii leo aghalabu istikhara inafanyika kwa njia hii. Kumenukuliwa istikhara mashuhuri za wanazuoni wa dini na wengine; ikiwemo istikhara ya Sheikh Abdul-Karim Hairi, mwasisi wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qom, Iran kwa ajili ya kwenda kuishi Qom na istikhara ya Muhammad Ali Shah kwa ajili ya kufunga makao ya Majlisi ya Ushauri (Bunge). Shekhe Abbas Qomi, amebainisha katika kitabu chake cha Mafatihul-Jinan baadhi ya mitindo na namna ya kufanya istikhara. [1]

Utambuzi wa maana

Istikhara katika lugha ina maana ya kutafuta kheri. [2] Katika istilahi, istikhara ina maana ya kutafuta kheri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. [3] Sahib al-Jawahir, fakihi wa Kishia wa karne ya 13 Hijria anasema: Istikhara ina maana mbili:

1. Kumuomba Mwenyezi Mungu akuweke katika jambo la kheri ambalo umekusudia kulifanya. Yaani akupe muongozo wa kufanya jambo lenye kheri.

2. Kumuomba Mwenyezi Mungu akupe tawfiki ya kuchagua jambo na yumkini tawfiki hii ikapatikana kwa istikhara au kwa kushauriana na mtu. [4]

Istikhara kwa Sala Kufanya istikhara kwa Sala ni kwa namna hii: Mwenye kutaka kufanya istikhara kwa kwa kutumia Sala, anapaswa kuswali rakaa mbili na baada ya kukamilisha Sala asujudu na kusema:

أستخير الله في جميع أموري خيرة في عافية

Kisha baada ya dua hiyo, kila ambacho Mwenyezi Mungu atakitia katika moyo wake, basi akifanye hicho hicho. [5]

Istikhara kwa Qur’an

Kuna aina mbalimbali za kufanya istikhara kwa Q’ran [6] na miongoni mwazo ni: • Kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ja’afar Sadiq (as) ni kwamba, moja ya aina za kufanya istikhara kwa Qur’an ni kwamba, kila mara mtu anapokumbwa na utata na hali ya kusitasita na kushindwa kuamua kuhusiana na kufanya au kuacha kufanya jambo fulani, basi atakapokuwa amejiandaa kwa ajili ya Sala, afungue Qur’an na akifanyie kazi kitu cha kwanza atakachokiona baada ya kufungua msahafu. [7] • Sayyid Ibn Tawus amenukuu kutoka kwa Bwana Mtume (saww) ya kwamba: Wakati unapotaka kufanya istikhara kwa kutumia Qur’an, soma Surat al-Ikhlas (Qul-huwallah) mara tatu, mswalie Mtume mara 3 na kisha soma dua hii:

قُلْ اللَّهُمَّ إِنِّی تَفَأَّلْتُ بِکِتَابِکَ وَ تَوَکَّلْتُ عَلَيْکَ فَأَرِنِی مِنْ کِتَابِکَ مَا هُوَ الْمَکْتُومُ مِنْ سِرِّکَ الْمَکْنُونِ فِی غَیْبِک.

Kisha baada ya dua hiyo, afungue msahafu na achukue jibu la istikhara yake kwa kuangalia mstari wa kwanza wa ukurasa wa kwanza. [8] • Kwa mujibu wa baadhi ya nukuu, baada ya kufungua msahafu, afungue kurasa saba au nane na achukue jibu la istikhara yake katika ukurasa wa saba au wa nane. [9]

Istikhara kwa kutumia karatasi

Katika kufanya istikhara kwa kutumia karatasi anachotakiwa kukifanya mtu ni kuandika maneno mawili ya “fanya” na usifanye” katika karatasi mbili tofauti na badala ya kufanya adabu maalumu, anachotakiwa hapa ni kuchagua moja ya vijikaratasi alivyoandika na kisha kufanyia kazi kile kilichoandikwa ndani yake. [10] Ibn Idris Hilli amezitambua hadithi zinazoashiria kufanya istikhara kwa kutumia karatasi kwamba, hazina itibari.; [11] lakini Shahid al-Awwal amepinga mtazamo wake huo akitoa hoja kwamba, istikhara kwa kutumia karatasi ilikuwa mashuhuri kwa Maimamu (as). [12]

Istikhara kwa kutumia tasbihi

Kuna aina tofauti za kufanya istikhara kwa kutumia tasbihi.

• Shahid al-Awwal amesema katika kitabu cha Dhikraa kwamba, baada ya kusoma moja kati ya sura za Hamd (kwa akali mara tatu na kama haijawezekana basi japo mara mopja) na Surat al-Qadr mara 10 na vilevile kusoma dua makhsusi, utachukua tasbihi na kutenganisha sehemu fulani ya tasbihi na kisha kuanza kuzihesabu mbili mbili, kama ya mwisho itakayobakia ni idadi mbili basi jambo ulilokusudia kulifanya unaweza kulifanya, lakini kama idadi iliyobakia ni moja, basi utaliacha hilo, au kinyume chake. [13]

• Aina nyingine ya kufanya istikhara kwa kutumia tasbihi imenukuliwa katika kitabu cha Mafatihul-Jinan kutoka kwa Sahib al-Jawahir ambayo ilikuwa mashuhuri katika zama zake. Aina hii ya istikhara ni kwamba, baada ya kusoma Qur’an na dua, chukua sehemu ya tasbihi na punguza nane nane na kama itabakia moja basi jibu lake ni nzuri kawaida na kama zitabakia mbili, hapa kuna katazo moja, yaani ulilokusudia usilifanye na kama zitabakia tatu, kufanya jambo ulilokusudia na kuliacha ni sawa (hakuna tofauti) na kama zitabakia nne kuna makatazo mawili na kama zitabakia tano baadhi wamesema, kuna ugumu na taabu ndani yake na baadhi wamesema, kuna lawama ndani yake na kama zitabakia sita jibu lake ni zuri sana, ni ni lazima kuharakisha kulifanya lile alilokusudia mtu, na kama zitabakia saba hekima yake ni kama pale zilipobakia tano na kama zimebakia nane kuna makatazo manne. [14] Baada ya Sahib al-Jawahir kunukuu istikhara hii amebainisha wazi kwamba: Sijaona wala kupata msingi na tawi la istikhara hii katika vitabu vya kale na vipya kama ambavyo baadhi ya walimu wetu waliotabahari wamelizungumzia pia jambo hili. [15]

Uhalali wa istikhara

Kabla ya Uislamu, aina fulani ya istikhara iliyojulikana kwa la istisqam bil-Azlam (kupiga ramli) ilikuwa imeenea, [16] ambayo ilikuwa ikifanyika kwa mshale na upinde. Sheikh Mahmoud Shaltut, msomi na mwanazuoni wa Kisuni akitumia Aya ya 3 ya Surat al-Maidah ambapo ndani yake kumeharamisha kupiga ramli, ameitambua Aya hii kama misdaqi na mfano wa kuharamishwa istikhara na kukitaja kitendo hiki kuwa sio halali; [17] hata hivyo Ayatullah Safi Golpaygani mmoja wa Marajii Taqlidi wa Kishia anasema kuwa, kuna tofauti baina ya istikhara na kupiga ramli na hivyo anapinga rai na matzamo wa Sheikh Shaltut, [18] na anaeleza kwamba, kufanya istikhara ni mustahabu kwa mujibu wa hadithi mbalimbali. [19]

Adabu na masharti

Kuhusiana na istikhara kumebainisha adabu na masharti na baadhi ya masharti hayo ni:

• Kuwa mubaha jambo ambalo linafanyiwa istikhara: Istikhara ni kwa ajili ya kuondoa shaka na hali ya kusitasita katika mambo ya mubaha na sio katika mambo ya kheri. [20]

• Kujifanyia istikhara: Allama Majlisi anasema, hakuna hadithi inayoonyesha kwamba, mtu anaweza kufanya istikhara kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa mukatadha huo ni bora kila mtu akafanya mwenyewe istikhara. [21] Hata hivyo Sayyid Ibn Tawus amenukuliwa kwamba, yeye alikuwa akiamini kwamba, inajuzu kumfanyia istikhara mtu. [22]

• Istikhara baada ya ushauri: Ina maana kwamba, kabla ya kufanya istikhara mtu anapaswa kutafuta ushauri wa jambo husika na kama hakupata natija katika ushauri, basi hapo anaweza kufanya istikhara.

• Sehemu ya istikhara: Kwa mujibu wa Shahid al-Awwal anasena, ni bora istikhara ya dua ikafanyika msikitini au katika haram (maeneo matakatifu). [23]. Katika baadhi ya hadithi limekuja suala la kufanya istikhara katika haram ya Imam Hussein (as). [24]

• Wakati: Feydh Kashani amesema katika kitabu chake cha Taqwim al-Muhsinin kwamba: Ili kufanya istikhara kwa kutumia Qur’an kumenukuliwa katika kila siku katika wiki kwamba, kuna saa fulani; lakini inaelezwa kwamba, saa zilizotajwa ni mashuhuri baina ya watu wenye imani na hazijatajwa katika hadithi. [25] Sahib al-Jawahir anasema, hakuna wakati maalumu uliotajwa kwa ajili ya kufanya istikhara ya Sala. [26] Hata hivyo kuhusiana na istikhara kwa kutumia Qur’an imenukuliwa kwamba, ifanyike katika wakati wa Sala. [27]

• Kuifanyia kazi istikhara: Kufanyia kazi istikhara hakuna ulazima wa kisheria, lakini ni bora mtu baada ya kupata jibu la istikhara akalifanyia kazi. [28]

• Kusoma dua makhsusi, [29] kusoma baadhi ya sura za Qur’ani, [30] na kumswalia Mtume (saww) na aali zake watoharifu (as) nazo ni katika adabu zinasisitizwa kutekelezwa kabla ya kufanya istikhara.

== Istikhara mashuhuri

Baadhi ya istikhara mashuhuri ni:

• Istikhara ya Muhammad Ali Qajar: Mtawala huyu wa zamani wa Iran alikuwa akifanya istikhara katika mambo mbalimbali kama vile kufunga Majsli ya Ushauri (Bunge la taifa) mwaka 1287 Hijria Shamsia na alipokuwa akitaka kuwapeleka uhamishoni baadhi ya watu na kadhalika. [31]

• Istiklhara ya Naser al-Din Shah Qajar ya kukubali mamlaka ya Iran kwa Herat: [32] Mwaka 1296 Hijria, serikali ya uingereza ilichukua uamuzi wa kuirejesha mamlaka ya Herat kwa Iran kwa muda usiojulikana. Baada ya Naser al-Din Shah kufanya mashauriano mengi aliamua kufanya istikhara. [33]

• Istikhara ya Sheikh Abdul-Karim Hairi Yazdi kwa ajili ya kuishi Qom: Ayatullah Hairi mwasisi wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qom, Iran, mwaka 1340 Hijria alikwenda katika mji wa Qom. Katika safari hiyo idadi kadhaa ya Maulamaa na wakazi wa Qom walimtaka abakie na kuishi katika mji huo. Awali Sheikh Hairi alikumbwa na hali ya kusitasita na utatanishi na kutojua akubali au akatae. Baada ya Maulama kumsisitizia sana aliamua kufanya istikhara na hivyo akabakia na kuishi katika mji huo. [34]

Hukumu ya kisheria ya kufanyia kazi jibu la istikhara

Kwa mujibu wa nadharia na mtazamo wa mafakihi, sio wajibu kufanyia kazi natija na matokeo ya istikhara na kupingana na majibu hayo pia kisheria sio jambo la haramu, ingawa ni bora kutopingana na matokeo ya istikhara. [35] Kwa mtazamo wa Ayatullah Shubairi Zanjani ni kwamba, kwa kuzingatia kwamba, kupingana na matokeo ya istikhara kuna uwezekano wa kutokea madhara basi ni bora kutopingana nayo. [36]


Kumeandika vitabu mbalimbali kuhusiana na istikhara. Kitabu cha kwanza katika uga huu ni cha al-Ayyashi na vilevile kitabu cha Zubairi al-Shafi'i. Kuna vitabu vingine pia vilivyoandika katika uwanja huu kama vile:

• Fat’hu al-Abwab Baina Dhawi al-Bab wa Baina Rabbi al-Arbab Fil Istikharaat, mwandishi Sayyid bin Tawus (aliaga dunia 664 Hijria): Katika kitabu hiki ambacho kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu, kumebainishwa uhalai wa istikhara na aina zake mbalimbali.

• Irshad al-Mustabsirin fil istikharaat, mwandishi: Sayyid Abdallah Shubbar.

• Istikhareh ba Qur’ani, mwandishi: Sheikh Bahai.

• Istikharname, mwandishi: Abdul-Hussein Lari.

• Mafatihul-Ghaib dar adab istikhara, mwandishi: Muhammad Baqir Majlisi

• Mafatihul-Ghaib fil istikhara wal istishara, mwandishi: Kaf’ami.

Rejea

Vyanzo