Hubbu al watan mina al iman
Hubbu Al-Watan Mina Al-Imaan (Kiarabu: حُبّ الوطن من الإيمان), yaani «Kupenda nchi ni sehemu ya imani». Ni msemo maarufu unaohusishwa na maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Hata hivyo, kwa mujibu wa watafiti mbali mbali kama Ayatullahi Makarim Shirazi, msemo huu haupatikani katika vyanzo asili vya Hadithi vya upande wa madhehebu yaShia, pia baadhi ya wanazuoni wameuhisabu msemo huu kuwa ni wa kutungwa na wala hauhusiani na kauli za bwana Mtume (s.a.w.w). Abul Futuh Razi, mfasiri wa Qur’an wa karne ya sita, katika tafsiri yake ya Rawdh al-Jinan, ananukuu msemo huu akimhusisha na Mtume Muhammad (s.a.w.w) na msemo huu, yeye katika maelezo yake alisema kuwa; bwana Mtume (s.a.w.w) aliusema msemo huu alipokuwa safarini mwake akiondoka Makka kuelekea Madina. Kwa hivyo, inafikiriwa kuwa; kauli hii ya bwana Mtume (s.a.w.w) inahusiana na mji wa Makka peke yake.
Hata hivyo, kundi fulani la wanazuoni halikubaliani na uhusiano wa moja kwa moja kati ya kupenda nchi kijiografia na suala imani, kama inavyoelezwa katika msemo huu. Hivyo basi ili wanazuoni hawa waepukane na maana maarufu ya msemo huu, wao wenyewe walijaribu kutoa tafsiri mbali mbali kuhusiana na maana ya neno «nchi» lililomo katika usemi huu. Baadhi ya wanazuoni hawa wanaamini kwamba neno «nchi» linamaanisha «umma adhimu wa Kiislamu», huku baadhi yao wakilifasiri neno «nchi» kwa maana ya Pepo. Aidha, wanazuoni wengine wamejaribu kupanua zaidi maana ya «nchi» wakisema kuwa; «Nchi» ni mahali ambapo mtu hupata utulivu wa kiroho ndani yake, kwa kuzingatia maana hii, wao wanaamini kwamba; Nchi asili ya mwanadamu ni ile daraja ya juu ya kuwa karibu na Mwenye Ezi Mungu.
Nafasi na Hadhi ya Msemo Huu
Msemo usemao «حُبُّ الْوَطَنِ مِنَ الْایمانِ» ambao unamaanisha «Kupenda nchi ni sehemu ya imani», yameenea mno katika jamii ya Kiislamu ukitambulika kama ni hadithi maarufu [1] inayonasibishwa na bwana Mtume Muhammad (s.a.w.w). [2] Umaarufu wa sentensi hii miongoni mwa watu umeufanya msemo huu kuwa ni methali mashuhuri, huku waandishi na washairi mbali mbali wakionekana kuutumi katika maandishi na kazi zao mbali mbali. [3]
Uhalali msemo usemao «Kupenda Nchi ni Sehemu ya Imani» kwa Mtazamo wa Hadithi
Msemo usemao; «Kupenda Nchi ni Sehemu ya Imani» ni wenye kutiliwa shaka na wanazuoni mbalimbali wa Kiislamu kutokana na ukosefu wa msingi wake katika vyanzo vya kale vya Hadithi, hasa katika madhehebu ya Kishia. Kwa mujibu wa maelezo ya Ayatollahi Makarim Shirazi, ibara hii haionekani ndani ya vitabu vya asili vya Hadithi vya madhehebu ya Shia. [4] Mara ya kwanza kabisa msemo huu umeonekana katika tafsiri ya Kiarabu ya Marzebaan Naameh, ambacho ni kitabu cha Marzeban bin Rustam (aliyefariki mwaka wa 302 Hijria). [5] Hii inafanya kitabu cha Marzeban Naameh kuwa ndio chanzo cha kale zaidi kinachodai kuwa ibara hiyo ni Hadithi itokayo kwa bwana Mtume (s.a.w.w). [6]
Hadithi hii imetajwa na baadhi ya wanazuoni wa Kishia wa baadaye huku wakiitaja kuwa ni Hadithi mursal (Hadithi isiyo na mfululizo wa wapokezi maalumu, ila msimulizi wake halisi hajulikani). Abul Futuh Razi, mfasiri wa Kishia wa karne ya sita, katika tafsiri yake ya Rawdhu al-Jinan, anauhusisha msemo huu na bwana Mtume (s.a.w.w), akieleza kuwa; Mtume (s.a.w.w) ulitamka maneno haya wakati alipokuwa akiondoka Makka kwenda Madina. Abul Futuh Razi aliongeza akisema kuwa; Nchi iliokusudiwa na Bwana Mtume katika usemi huu nimji wa Makka. [8] Sheikh Abbas Qummi, ameutaja usemi huu katika ]kitabu chake Safinat al-Bihar, akinukuu kutoka katika utangulizi wa kitabu Amal al-Aamal, kilichoandikwa na Sheikh Hurr Amili. [9]
Wanazuoni wengine wa Kiislamu, kama vile: Ibn Arabi ameutaja usemi huu katika tafsiri yake ya Qur’ani. [10] Sayyid Muhsin Amin katika kitabu chake A'yan al-Shi'a. [11] Mirza Habibullah Khui, mshereheshaji wa Nahj al-Balagha.[12] Wanazuoni watatu hawa wote kwa pamoja wameihisabu ibara hii kama ni Hadithi maarufu, ila hakuna hata mmoja kati yao aliyetoa ushahidi wa wazi wa kuithibitisha uhalali wa Hadithi hii. Hata hivyo, baadhi ya wanazuoni, akiwemo Ayatullah Makarim Shirazi na Sayyid Jafar Shahidi, wamekuwa na shaka juu ya uhalali wa Hadithi hii, na wengine wameihisabu kuwa ni miongoni mwa Hadithi za kutungwa. [13][14]
Washairi maarufu kama vile Jalalu Al-Diin Rumi (Maulana) na Saadi pia nao wameonekana kuutumia msemo huu katika mashairi yao, wakionekana kuuhisabu msemo huu kama ni Hadithi maalumu miongoni mwa Hadithi. [15]
Imeelezwa kuwa wengi miongoni mwa wanazuoni wa Kisunni wamepinga ukanushaji wa usemi huu, unaodai kwamba usemi huu hautokani na Hadithi ya bwana Mtume, huku akitoa huja kadhaa dhidi ya madai ya waliodai madai hayo. [17]
Vielelezo Viungavyo Mkono
Kulingana na maoni ya Ayatullahi Makarem Shirazi, ni kwamba; Ingawa usemi huu haupatikani katika vyanzo vya kuaminika, ila bado kuna uwezekano wa kutaja aina mbili za ushahidi katika kuunga mkono usemi huu:
- Tukivungua kurasa za vyanzo mbali mbali vya Hadithi, tutakuta ibara kuna zinazofanana na ibara hii kutoka kwa Imam Ali (a.s), jambo ambalo linathibitisha uwepo wa ibara yenye maana kama hiyo katika vyanzo vya Hadithi. Kwa mfano, moja ya ibara yenye yanayofanana kimaana na ibara hiyo, ni ile kauli ya Imamu Ali (a.s) isemayo; «عُمِّرَتِ الْبُلْدَانُ بِحُبِ الْأَوْطَان ; Miji imeimarishwa kutoka na upendo wa nchi» [18] na «مِنْ كَرَمِ الْمَرْءِ بُكَاهُ عَلَى مَا مَضَى مِنْ زَمَانِهِ وَ حَنِينُهُ إِلَى أَوْطَانِه ; Na miongoni mwa ishara ya utu wa mtu fulani ni kilio chake kwa muda uliommalizikia na shauku yake juu ya nchi yake (au mji wake)». [19]
- Upendo wa nchi ni hisia ya kawaida inayotokana na hali halisi ya maumbile ya kutaka kulipa fadhila, jambo ambalo ni ishara ya imani na utu wa mtu fulani. [20]
Changamoto Dhidi ya Uhusiano Kati ya Imani na Upendo wa Nchi
Kauli inayosema, Upendo wa nchi ni sehemu ya imani, imeleta mjadala mkubwa kuhusu maana yake halisi na uhusiano wake na imani ya Kiislamu. Wanazuoni na watafiti mbalimbali wameonekana wakitoa maoni na tafsiri tofauti kuhusiana na msemo huu.
Hoja Zinazopinga Uhusiano wa Moja kwa Moja
Kundi moja la wanazuoni limejaribu kupinga tafsiri dhahiri au ya kilugha ya msemo huu kwa sababu zifuatazo:
- Mapenzi ya nchi si kipimo cha imani: Wao wakikosoa tafsiri dhahiri ya msemo huu, wanasema kwamba; watu wasio na imani, kama makafiri na wanafiki, pia ni miongoni mwa wanaopenda nchi zao. Hivyo basi, upendo juu ya nchi hauwezi kuwa ni alama ya imani yao.
- Imani za Wanaoishi Katika Nchi za makafiri: Ikiwa muumini atazaliwa na kuishi katika nchi ya makafiri, bila shaka atakuwa na upendo wa nchi hiyo, ila upendo huo hauwezi kuhusishwa na imani yake ya Kiislamu, kwani mazingira ya nchi hiyo hayaendani na mafundisho ya Kiislamu. [21]
Shams Tabrizi, msomi na mwanasufi wa Kiislamu, pia anapingana na maana dhahiri inayohusishwa na bwana Mtume (s.a.w.w). Yeye anaamini kwamba; Pale Bwana Mtume (s.a.w.w) alipotaja neno «nchi» katika ibara yake hiyo maarufu, hakuwa akimaanisha nchi zote duniani, bali alimaanisha mji wa Makka peke yake. Kwa mujibu wa maoni ya Tabrizi, upendo wa bwana Mtume wa kuupendo mji wa Makka haukuwa upendo wa mapenzi ya kidunia, bali ulikuwa na maana ya kiroho wenye uhusiano wa moja kwa moja na msuala ya kiimani. [22]
Tafsiri ya Wanazuoni wa Shia
Wanazuoni wa Kishia, kama vile Sayyid Jafar Murtaza na Sayyid Murtaza Askari, wakitoa tafsiri ya usemi huu, wamejaribu kufafanua maneno mawili msingi yaliomo ndani ya usemi huu, nayo ni «upendo» na «nchi». Ufafuzi wao kuhusiana na maana ya maneno mawili haya ni kama ifuatavyo:
- Upendo: Wakifafanua maana iliyokusudiwa katika matumizi ya neno upendo, wanasema kwamba; Upendo uliotajwa katika msemo huu unahusiana na malengo adhimu yanayodhamiriwa kufikiwa na dini ya Kiislamu, na hauna maana ya mapenzi ya kihisia tu.
- Nchi: Kwa mujibu wa maoni yao, neno «nchi» linawakilisha Umma mzima wa Kiislamu, na sio kwamba neno hili lina maana ya mahali pa mtu alipozaliwa au kukulia ndani yake, ambayo ni maana dhahiri ya neno hili. [23][24]
Tafsiri za Kiroho za Neno «Nchi»
Kundi la fulani la wanazuoni linaamini kwamba; Maana ya neno «nchi» hapa lina maana ya Pepo ya milele walioahidiwa wachamungu. Kwa mujibu wa mtazamo huu, Muumini ni mgeni duniani na utendaji wake wa matendo mema, unadhihirisha hamu yake ya kurudi tena mjini mwake. [25] Wanazuoni wa Kisufi, wakipanua zaidi maana ya neno «nchi», wanasema kwamba; neno nchi linamaanisha mahali ambapo mtu hupata utulivu na amani ndani yake. [26] Hivyo basi wao wanaamini kuwa; «nchi» ya kweli ni ile daraja ya juu kabisa [27] ya kuwa karibu na Mwenye Ezi Mungu. [28] Masufi na wanairfani huwakupaliani na wale wanaotafsiri neno «nchi» kwa kmaana ya «Upendo wa kupenda nchi ya dunia, na wakiamini kwamba, kufanya hivyo ni sehemu ya imani» na badala yake wamewahisabu watu kama hao, kuwa ni miongoni mwa watu wenye mioyo potufu wapendao dunia, jambo ambalo limewafanya wao kuwa vipofu na viziwi. [29]