Nenda kwa yaliyomo

Ayat Baiat al-Ridhwan

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Aya ya Bai'at al-Ridhwan)
Makala hii inahusiana na Baiat al-Ridhwan (baia ya Ridhwan). Ili kujua kuhusiana na tukio lenye jina hili angalia makala ya Baia Ridhwan.

Ayat Baiat al-Ridhwan au Aya ya Baia (Kiarabu: آية بيعة الرضوان ) (Surat Fat’h: 18) inatangaza kuhusu Mwenyezi Mungu kuwa radhi na Waumini walioshiriki katika baia ya Ridhwan. Maulamaa wa Ahlu-Sunna huitumia Aya hii kwa ajili ya kuthibitisha nadharia ya uadilifu wa masahaba; lakini wafasiri wa Kishia wanaamini kwamba, ridhaa ya Mwenyezi Mungu katika Aya hii sharti lake ni kusimama kidete na kufungamana na mkataba wa masahaba na inajumuisha tu masahaba ambao wamebakia katika utiifu wao. Kwa mujibu wa wafasiri wa Qur’an wa Kishia, Aya ya 10 Surat al-Fat’h imeshuka baada ya Aya hii na ndani ya Aya hiyo, Mwenyezi Mungu anaeleza sharti la ridhaa ya Mwenyezi Mungu kwa waumini ni kutii amri na maagizo ya Mtume (s.a.w.w) na kujiepusha na kukiuka mkataba na makubaliano.

Kwa mujibu wa Aya ya Baia al-Ridhwan Mwenyezi Mungu amewapa ujira mkubwa waumini waliojitolea ambao walimpa baia na kiapo cha utiifu Mtume (s.a.w.w) katika Baia al-Ridhwan: Ridhaa ya Mwenyezi Mungu ipo pamoja nao, Allah amewapa utulivu na ushindi wa karibu. Kadhalika katika Aya inayofuata, Mwenyezi Mungu anatoa ahadi ya waumini hao kupata ngawira nyingi ambapo kwa mujibu wa wafasiri ni ngawira zilizopatikana katika Vita vya Khaybar.

Jina na umuhimu wake

Aya ya 18 ya Surat al-Fat’h ambayo ndani yake inabainisha tukio la Baia Ridhwan inajulikana kwa jina la “Ayat Baiat al-Ridhwan”. [1] Maulamaa wa Ahlu-Sunna huitumia Aya hii kwa ajili ya kuthibitisha nadharia ya uadilifu wa masahaba wote (yaani masahaba wote ni waadilifu). [2]

Andiko na tafsiri ya Aya

لَقَدْ رَضِيَ اللهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِى قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا

Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia Waumini walipo fungamana nawe chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa Ushindi wa karibu.



Baia ya Ridhwan

Makala kuu: Baia ya Ridhwan na Sulhu ya Hudaibiyah

Baia al-Ridhwan au Baia Tahta al-Shajarah ni mkataba wa kundi la masahaba na Mtume (s.a.w.w) ambao ulifanyika mwaka wa 6 Hijria jirani na Makka. Kwa mujibu wa Ibn Hisham mwandishi wa historia mashuhuri wa karne ya 3 Hijria katika kitabu chake cha al-Sirah al-Nabawiyyah ni kwamba, katika tukio hili, Mtume (s.a.w.w) alitoka nje ya Madina akiwa pamoja na masahaba kadhaa kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada ya Umra; hata hivyo washirikina waliwazuia kuingia Makka. Kukatumwa wajumbe na wawakilishi baina ya pande mbili yaani baina ya Mtume na washirikina. Tetesi na uzushi wa kuuawa na Qureshi mmoja wa wawakilishi wa Mtume (s.a.w.w) ulipelekea Mtume kuwaita masahaba kwa ajili ya baia na wao wakatoa baia na kiapo cha utiifu kwamba, madhali wako hai watamlinda Mtume hadi pumzi yao ya mwisho ya uhai. Tukio hili hatimaye lilipelekea kufikiwa Sulhu ya Hudaibiyah na ikaafikiwa kwamba, Waislamu wasitekeleze ibada ya Hija mwaka huu na badala yake waje Makka mwaka ujao kwa ajili ya ibada hiyo. [3]

Maudhui; ujira wa watoa baia

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu ameonyesha kuwaridhia waumini waliotoa baia kwa Mtume (s.a.w.w) katika Baiat al-Ridhwan. [4] Kwa mujibu wa Aya hii, Mwenyezi Mungu amewapatia ujira na malipo matatu waumini waliojitolea katika lahadha na wakati nyeti na wakatoa baia na kiapo cha utiifu kwa Mtume (s.a.w.w):

  1. Mwenyezi Mungu kuwa radhi nao: ((رَضِيَ اللَّه))
  2. Utulivu: ((فَأَنْزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ)): “Basi akateremsha utulivu juu yao”; Mwenyezi Mungu aliwateremshia utulivu kiasi kwamba, wakiwa katikati ya umati wa maadui na mbali kabisa kutoka katika mji wao, katikati ya silaha zao tayari, hawakuwa na hofu na woga mioyoni mwao, na walisimama imara na wima kama mlima.
  3. Ushindi wa karibu: ((أَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا)): Kwa mujibu wa wafasiri ni kuwa, ushindi huu ni ukombozi wa Khaybar na kutumiwa neno Qariban yaani karibu, kunaunga mkono nadharia hii; kwani ushindi wa Khaybar ulipatikana mwanzoni mwa mwaka wa 7 Hijria ikiwa ni pengo la miezi michache baada ya Sulhu ya Hudaibiyah. Kadhalika ibara ya: ((وَ مَغانِمَ کَثِیرَةً یَأْخُذُونَها)) ambayo imekuja katika inayofuata, inaashiria ghanima walizopata Waislamu katika ushindi na ukombozi wa Khaybar katika kipindi cha muda mfupi. [5]

Kutumiwa Aya hii kwa ajili ya kuthibitisha uadilifu wa masahaba

Baadhi ya Maulamaa wa Ahlu-Sunna wanaitambua Aya hii kama hoja ya kuthibitisha kwamba, masahaba wote ni waadilifu. [6] Wanazuoni wa Kisuni wanasema kuwa, kuwa radhi Mwenyezi Mungu na masahaba ni hoja kwamba, masahaba wote ni waadilifu na wanadai kwamba, mtu ambaye Mwenyezi Mungu yupo radhi naye katu hawezi kughadhibika naye. [7] Maulamaa wa Kishia kwa upande wao wanasema kuwa, Aya hii haionyeshi na kuthibitisha kwamba, masahaba wote ni waadilifu; kwa sababu Aya hii inawazungumzia masahaba ambao walikuweko tu katika tukio la Baia ya Ridhwan na wakasimama kidete na kubakia katika ahadi na kiapo chao cha utiifu na sio masahaba wote. [8] Kadhalika nadharia ya kwamba, masahaba wote ni waadilifu inapingana na Aya ya 101 Surat al-Tawba kwani Aya hiyo inaeleza kuwa, baadhi ya masahaba ni wanafiki. [9]

Wafasiri wa Qur'an waa Kishia wanasema kuwa, kuridhiwa na Mwenyezi Mungu katika Aya hii kuna sharti ambalo ni kusimama kidete katika kumfuata Mtume (s.a.w.w). [10] Ali bin Ibrahim Qommi, mwandishi wa Tafsir Qummi anasema, Aya ya 10 Surat al-Fat'h ilishuka baada ya Aya hii na Mwenyezi Mungu ndani ya Aya hiyo, anaeleza sharti la kuwaridhia waumini ni kutii amri na maagizo ya Mtume (s.a.w.w) na kujiepusha na kukiuka mkataba na makubaliano.[11]

Rejea

Vyanzo

  • Ibn ʿAbd al-Barr, Yūsuf b. ʿAbd Allāh. Al-Istīʿāb fī maʿrifat al-aṣḥāb. Beirut: Dār al-Jīl, 1412 AH.
  • Ibn Ḥajar al-ʿAsqalānī, Aḥmad b. ʿAlī. Al-Iṣāba fī tamyīz al-ṣaḥāba. Edited by ʿĀdil Aḥmad ʿAbd al-Mawjūd and ʿAlī Muḥammad Muʿawwaḍ. Beirut: Dār al-Kutub al-ʿIlmīyya, 1415 AH.
  • Ibn Hishām, ʿAbd al-Malik. Al-Sīra al-nabawīyya. Edited by Muṣṭafā al-Saqā. Beirut: Dār al-Maʿrifa, [n.d].
  • Khaṭīb Baghdādī, Aḥmad b. ʿAlī. Al-Kifāya fī ʿilm al-riwāya. Edited by Abū ʿAbd Allāh al-Suraqī and Ibrāhīm Ḥamdī al-Madanī. Medina: al-Maktabat al-ʿIlmīyya, [n.d].
  • Makārim Shīrāzī, Nāṣir. Tafsīr-i nimūna. Tehran: Dār al-Kutub al-Islāmiyya, 1374 Sh.
  • Qummī, ʿAlī b. Ibrāhīm al-. Tafsīr al-Qummī. Edited by Ṭayyib Mūsawī Jazāʾrī. Qom: Dār al-Kitāb, 1404 AH.
  • Ṭabāṭabāʾī, Sayyid Muḥammad Ḥusayn al-. Al-Mīzān fī tafsīr al-Qurʾān. Qom: Ismāʿīlīyān, [n.d].
  • Ṭūsī, Muḥammad b. al-Ḥasan al-. Al-Tibyān fī tafsīr al-Qurʾān. Edited by Aḥmad Qaṣīr al-ʿĀmilī. Beirut: Dār Iḥyāʾ al-Turāth al-ʿArabī, [n.d].