Annasu Niamun Faidhaa Matuu Intabahuu
Annasu Niamun Faidhaa Matuu Intabahuu / النَّاسُ نِیَامٌ فَإِذَا مَاتُوا انْتَبَهُوا "Watu wamelala, na watapokufa ndipo watakapoamka": Ni hadithi maarufu [1] inayosimuliwa kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) [2] pamoja na Imam Ali (a.s.), [3] ikiwa ni moja ya kauli zenye maana kubwa zinazogusa undani wa maisha ya mwanadamu.
Hadithi hii inatoa ukumbusho juu ya hali hailisi ya uhakika wa wanadamu, ikieleza kwamba; mara nyingi wanadamu huishi maisha yao wakiwa wameghilibiwa na umiliki wa mali za kidunia, heshima, na utukufu wa muda mfupi. Hata hivyo, baada ya kifo chao, huja kugundua kwamba walikuwa wakiishi katika udanganyifu wa muda mfupi mno, na mali walizodhani ni zao haziwezi kuwasaidia mbele ya ukweli wa maisha ya milele. [4]
Kauli ya Imamu Ali (a.s) katika Nahjul Balagha inayosema, "Watu katika dunia ni kama watu walio katika msafara unaowasafirisha huku wakiwa wamelala", [5] Imefafanuliwa ikiwa na maana sawa na Hadithi mashuhuri isemayo, "Watu wamelala, na watakapokufa ndipo watakapoamka". [6] Neno la Kiarabu "Intibah", lililomo ndani ya Hadithi kiasilia lina maana ya kuzinduka au kuwa na tahadhari, lakini katika Hadithi hii limefsiriwa kwa maana ya "kutoka katika usingizi" au "kupata ufahamu na kutambua hali halisi". [7]
Pia, katika moja ya mistari ya mashairi ya mshairi maarufu wa Iran aitwaye Mahmud Shabestari, kuna ubeti unaosema, "Upo usingizini na unachokiona ni taswira ya fikra zako tu", uliopo kwenye kitabu cha Gulshan-e-Raz, [8] ambacho ni mojawapo ya maandiko ya kifalsafa ya kidini ya Kiislamu, pia unaonekana kuwa umetokana na Hadithi hii mashuhuri. [9]
Mwanamashairi Jami (Aliyefariki 817 Hijria)
Katika beti zake, Jami anaashiria maana iliyomo katika Hadithi maarufu ya Mtume (s.a.w.w) kwa kusema:
“قال خَیْرُ الْوَرَی عَلَیْهِ سَلَام إِنَّمَا النَّاس هِجْعٌ و نِیام فإذا جائهم و إن کَرِهُوا سَکْرَةُ الْمَوْت بعدها انْتَبَهُوا”
" Mtukufu wa viumbe (Mtume), rehema iwe juu yake, alisema:
‘Hakika watu wamelala na wako usingizini. Na wanapokumbwa na sakaratu al-mauti, hata kama hawatamani (kufa), hapo wataamka baada ya kuzama katika wimbi la mauti.” [10]
Baadhi ya watafiti wanaamini kuwa; Hadithi hii isemayo: "Watu wamelala, na watakapokufa ndipo watakapoamka", inaashiria aina mbili za kifo: kifo cha lazima na cha kimaada, na cha pili ni kile kifo cha maana na cha kiroho, ambacho kinaweza kupatikana huku mtu akiwa bado anaendelea kuishi maisha ya hapa duniani. [11] Hii ndiyo sababu iliyopelekea wengine kuamini kuwa, Hadithi hii inatoa tahadhari ya kuwataka watu wasisubiri hadi siku ya kifo chao, ili kufumbuka macho kutoka usingizini wao wa kughafilika. [12]
Mulla Sadra, mwanazuoni na mwanafalsafa wa Kishia, ametumia Hadithi hii kupinga dhana isimayo kwamba; kifo ni hali ya kutokuwepo au kutoweka kwa mtu fulani. Yeye amedai kuwa; Hadithi hii ni ushahidi kamili ya kwamba, kifo ni aina ya kufumbuka macho na kupata ufahamu wa kuona uhalisia wa mambo, kinyume na ile imani inayoamini kwamba, maana ya kifo ni kutokuwepo au kutoweka. [13]
Al-Ghazali (aliyefariki mwaka 505 Hijria), mwanatheolojia na msufi wa Kiislamu, alifafanua Hadithi hii kwa njia ya taswira isemayo:
"Je! mtoto aliye tumboni mwa mama yake kisha akazaliwa ili kuona ulimwengu mpya na maeneo mapya. Hivi mtoto huyu anapozaliwa na kuuona ukubwa wa dunia, atatamani kurudi tena tumboni mwa mama yake?"
Kwa mtazamo wa Ghazali, dunia na Akhera zinafanana mno na mfano huu. Hivyo yeyote yule anayefariki akaiacha dunia hii na kuingia ulimwengu wa Akhera, kisha akauona ukubwa na uzuri wa akhera, si sawa wala haiwezeani kabisa kwa mtu huyo kutamani kurudi tena duniani. [14]
Jawadi Amoli, mwanazuoni na faqihi mashuhuri wa Kishia, akitoa uchambuzi wa Hadithi maarufu inayosema: “Watu wamelala, na watakapokufa ndipo watakapoamka” amesema kwamba; Mara nyingi waishao maisha ya kidunia hudhania kuwa wana rasilimali mikononi mwao, ila wakati wa kifo chao, hugundua kuwa yote yaliyokuwa yakionekana na kuhisabiwa kuwa ni mali yenye thamani fulani, sasa yamekuwa hayana msingi wala hawayaoni tena mbele yao. [15]
Nasafi, msufi wa Kiislamu wa karne ya saba Hijria, katika kazi yake andishi ya kifalsafa iliyoko katika kitabu kiitwacho “Insan Kamil”, akitegemea baadhi ya Riwaya, alitafsiri Hadithi hii maarufu ya "Al-naas Niyam..." akisema kwamba; Mambo yanayoonekana katika ndoto ni ya muda mfupi na yasiyo na uimara wa muda mrefu, hii sawa na mambo ya kidunia ambayo hayana uendelevu wa kweli. [16]
Aidha, watafiti wamehitimisha wakisema kuwa; Mara nyingi wanadamu wakiwa duniani huwa hawajui kwa undani athari na uhalisia wa matendo yao. Na ni baada ya kifo ndipo ambapo "uhalisia wa matendo yao" utakuwa wazi mbele yao, na kila mmoja atapata maarifa kamili kuhusiana na matokeo ya matendo na nyenendo zao walizokuwa nazo duniani humu. [17]
Mulla Sadra (mwanafalsafa wa Kishia), anaamini kuwa; kile ambacho binadamu hukiona katika ndoto zake ni mifano inayohusiana na viumbe halisi vilivyopo ulimwenguni humu. Vilevile, yale ambayo binadamu huyaona duniani humu pia ni mifano ya ukweli wa ulimwengu wa Akhera. Ukweli wa Akhera hauwezi kufunuliwa na kudhihiri moja kwa moja mbele ya mwanadamu, isipokuwa kwa njia ya mifano ambayo inahitaji kufasiriwa. [18]
Mwandishi wa tafsiri ya Makhzan al-Irfan pia naye anafafanua ukweli huu akisema kuwa; kile tunachokiona katika ulimwengu huu ni gamba la nje tu la ukweli halisi. Na mwanadamu hataweza kufikia na kutambua ukweli wa mambo haya isipokuwa baada ya kufa kwake. [19]