Ruhullahi (Lakabu)
Lakabu ya Ruhullahi Kiarabu “روح الله” ( Roho ya Mungu): Katika mila za Kiislamu na Kishia "Roho ya Mungu" (روح الله), ni jina litumikalo kama lakabuni moja maalumu kuhusiana na Nabii Isa (a.s). Lakabu hii imetajwa wazi katika Hadithi mbali mbali, pia inapatikana katika vitabu kadhaa vinavyozungumzia ziara (sala na salamu) zisomwazo kwa ajili ya watukufu fulani. [1] Miongoni mwa ibara zilizobeba jina hili ndani yake ni ibara isemayo:
"السَّلَامُ عَلَى عِيسَى رُوحِ اللَّهِ" (Amani iwe juu ya Isa, Roho wa Mungu). [2]
Aya ya 171 ya Surah An-Nisa pia inahusisha wazo hili, ingawa si kwa uwazi kabisa:
"Hakika Masihi Isa mwana wa Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni neno lake alilomtia Maryam, na ni roho iliyotoka kwake."
Sababu za Kuitwa Nabii Isa "Roho ya Mungu"
Wanazuoni wameelezea sababu kadhaa za Nabii Isa (a.s) kupewa lakabu hii ya kipekee miongoni mwa sababu zilizotajwa ni:
1. Kuumbwa Kwake Moja kwa Moja Kupitia Amri ya Mungu:
Nabii Isa (a.s) aliumbwa kwa amri ya Mungu mwenyewe bila kutumia mbegu ya baba, ambalo nit endo la muujiza wa kipekee wa kuumbwa kwake. [3]
2. Ufufuo wa Kiroho Kupitia Dini ya Mungu:
Nabii Isa (a.s) aliwafufua watu kiroho kupitia mafundisho yake na kuwaongoza katika dini ya haki. [4]
3. Kufufua Wafu:
Mojawapo ya miujiza ya Nabii Isa (a.s), ilikuwa ule uwezo wake wa kufufua wafu kwa idhini ya Mola wake. [5]
4. Rehema kwa Waja:
Neno roho katika muktadha huu linaweza pia kumaanisha rehema, na kwamba Nabii Isa (a.s) alikuwa chanzo cha rehema kwa wanadamu. [6]
Maana ya Kipekee ya "Roho ya Mungu" Kama Lakabu
Pale neno "Roho" linapo ambatanishwa na neno “Mungu”, huwa linabeba maana ya heshima maalumu ndani yake, ambayo kwa lugha ya kitaalamu (kifalsafa) huitwa (idhafatu tashrifiyya). Hii humaanisha kwamba; Nabii Isa (a.s) alikuwa na roho yenye hadhi ya juu na yenye heshima maalumu, inayostahili kuitwa "Roho ya Mungu". Hii pia inasisitiza hali ya kipekee aliyonayo binadamu ukilinganisha na wanyama wengine, ambapo yeye ameumbwa kupitia sehemu mbili, nazo ni sehemu ya kimwili, na roho inayohusiana na Mungu mwenyewe. [7]
Matumizi ya Jina "Roho ya Mungu" kwa Watu Maarufu na Wasio Mitume
Mbali na matumizi yake kama lakabu ya Nabii Isa (a.s), pia jina "Roho ya Mungu" limeonekana kutumika kama jina la watu wa kawaida, ambao si mitume. Mfano mashuhuri zaidi wa matumizi hayo, ni matumizi ya jina hilo kwa Imam Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye alipewa jina hili na wazazi wake, bila ya kukusudia matukuzo maalumu katika kumpa jina hili.