Diwani ya Imam Ali (a.s)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Diwani ya Imam Ali (as))

Diwani ya Imam Ali (as) (Kiarabu: ديوان الإمام علي (ع)) ni mjumuiko wa mashairi kwa lugha ya Kiarabu ambayo yananasibishwa kwa Imam Ali ibn Abi Twalib (as). Maulamaa na wahakiki wa Kiislamu wanatambua kwamba, idadi ndogo ya mashairi hayo yalitungwa na Imam Ali (as) na yaliyobakia yalitungwa na washairi na malenga wengine kuhusiana na Imam Ali (as) au wanayahesabu kuwa ni mashairi ambayo Imam Ali aliyanukuu kutoka kwa watu wengine. Mashairi haya yalikusanywa katika karne za baada ya Imam Ali (as) na ya kale zaidi miongoni mwayo ni yale yaliyokusanywa na Abdul-Aziz Jaludi aliyeaga dunia 322 Hijria. Idadi kadhaa ya mashairi haya yanatofautiana katika nakala mbalimbali ambayo yametajwa kuwa ni baina ya 190 hadi 506. Akthari ya wahakiki wanaaamini kwamba, diwani iliyoko hivi sasa inatabikiana na kitabu cha "Anwar al-Uqul Fi Ash'ar Wasii al-Rasul" kilichoandikwa na Qutb al-Din Kaydari Bayhaqi (aliyeaga dunia 548 Hijria). Miongoni mwa mambo yanayoonyesha kuwa, beti nyingi za mashairi zilizoko katika kitabu hiki sio za Imam Ali (as) ni: Kuweko mbinu ya utungaji mashairi ambayo hutumiwa na watu wa mtaani, kuweko mashairi ambayo yanasifia makabila, kuwa na udhaifu mashairi hayo kwa upande wa balagha na fasaha, kuweko hali ya kujifaharisha katika baadhi ya mashairi hayo, kutajwa methali ambazo zinahusiana na Wairani, Warumi na Wagiriki na kuweko mgawanyo wa falsafa ambao ulizungumziwa na kuweko baina ya Waislamu katika karne ya pili Hijria. Agha Bozorg Tehrani anasema kuwa, chapisho kongwe kabisa la nakala ya diwani ni: Chapa ya Leiden Uholanzi 1745 Miladia, chapa ya Bulaq Misri ya 1251 Hijria, chapa ya Misri ya 1276 Hijria na chapa ya Tehran ya 1284 Hijria. Diwani hii ya mashairi imetarjumiwa na kutolewa sherh (ufafanuzi) kwa lugha mbalimbali za Kifarsi, Kilatini, Kituruki na Kiurdu. Hii leo kuna nakala za machapisho mengi ya diwani hii ya mashairi.

Kuhusishwa mashairi haya na Imam Ali (as)

Wasomi na wanazuoni wa Kishia wanaamini kuwa, mashairi mengi yaliyoko katika diwani ya Imam Ali (as) sio ya Imam huyo. Kwa mfano Allama Majlisi, anatilia shaka suala la kuhusishwa na Imam Ali (as) mashairi yote na kubainisha kwamba, akthari ya mashairi hayo ni ya vitabu vingine. Ibn Shahrashub amenukuu na kusema kuwa, diwani ya mashairi ya Ali bin Abi Twalib imeandikwa na mtu anayejulikana kwa jina la Ali ibn Ahmad (Fanjgerdi) mwanafasihi wa Neishabour (aliyeaga dunia 513 Hijria). [1] Hassan Hassanzadeh Amoli ameyatambua akthari ya mashaitri ya kitabu hicho katika kitabu chake cha Takmilat Minhaj al-Bara'a kwamba, ni ya wengine na amewataja pia washairi wa mashairi hayo. [2] Kwa mujibu wa baadhi, ni asilimia 10 tu mashairi yaliyoko katika diwani ambayo inawezekana kuyanasibisha na kuyahusisha na Imam Ali ibn Abi Twalib (as) na mashairi yaliyobakia ima yapo katika diwani zingine za maishari au ni ya washairi na malenga wengine. [3]

Hoja

Kuna sababu na hoja mbalimbali zilizotajwa kuhusiana na jambo hili ya kwamba, mashairi yote yaliyoko katika diwani ya Imam Ali (as) sio ya kwake.:

Katika utangulizi wa kitabu cha "Diwan al-Imam Ali (as)" baada ya kufanyika uhakiki uliofanywa na Maktabat al-Iman ya Cairo kumepatikana ishkali na kasoro 10 katika kuyahusisa maishairi hayo na Ali ibn Abi Twalib. Miongoni mwa kasoro hizo ni: Kuweko mbinu ya utungaji mashairi ambayo hutumiwa na watu wa mtaani, kuweko mashairi ambayo yanasifia makabila, kuwa na udhaifu mashairi hayo kwa upande wa balagha na fasaha, kuweko hali ya kujifahrisha katika baadhi ya mashairi hayo, kuweko mashairi mengi ambayo yalikuwa ni majibizano baina ya Imam Ali na Muawiya na Amr ibn al-A's na kuweko makosa ya urari wa vina na mizani. [4] Keyvan Sami'i anasema kuwa, pamoja na kasoro hizo, kuna maneno ya Kifarsi katika mashairi hayo, kutajwa methali ambazo zinahusiana na Wairani, Warumi na Wagiriki na kuweko mgawanyo wa falsafa ambao ulizungumziwa na kuweko baina ya Waislamu katika karne ya pili Hijria sambamba na kuweko mafumbo katika diwani jambo ambalo halikuwa limeenea baina ya Wairabu ni nyaraka na ushahidi wa kutokuwa sahihi kauli ya kuyanasibisha maishairi haya na Imam (as) na kudai kwamba yametungwa na yeye. [5] Miongoni mwa hoja nyingine ni kwamba, licha ya kuwa Imam Ali (as) alikuwa mtu mwenye dhuku ya fasihi, balagha na mtu fasaha sana, lakini mashairi hayo hayana hilo, jambo ambalo linatilia shaka kama kweli yametoka kwa mtu mwenye fasaha na balagha kama Imam Ali. Baadh ya watu kama Jahidh (mwanafasihi wa karne ya pili na ya tatu Hijria) na vilevile Yaqut Hamawi (mwanahistoria wa karne ya sita na ya saba Hijria) wamekataa kukubali kama mashairi hayo ni kutoka kwa Ali ibn Abi Twalib (as). Jahid anasema, Ali hakutumia mbinu ya utungaji mashairi ambayo hutumiwa na watu wa mtaani. Yaqut naye amenasibisha na Imam Ali beti mbili tu za mashairi na mashairi yaliyobakia amesema, si sahihi kuyanasibisha na Ali bin Abi Twalib. [6] Kadhalika watu kama Muhammad ibn Jarir Tabari, Ibn Qutaybah, Ibn Maskawayh Razi, Zamakhshari, Tabarsi na Sharif Radhii pamoja na kuwa wamenukuu mashairi kutoka kwa Imam Ali ibn Abi Twalib, lakini hawajamtaja katika orodha ya washairi. [7] Pamoja na hayo yote Sha’abi, Ibn Abdurabbuh, (mshairi wa Kiarabu wa karne ya 9 na 10 Hijria) na Qalqashandi (mwanafasihi na mashairi wa zama hizi wa Misri) wamemtaja Imam Ali kuwa ni mshairi na kwamba ni mshairi zaidi ya Abu Bakr, Omar (na Othman). [10]

Idadi ya mashairi na mgawanyo wake

Katika diwani ambazo zimechapishwa kuna tofauti kubwa kuuhusiana na idadi ya beti za mashairi yake. Kunaonekana mjumuiko wa mashairi 190, 355, 374, 455 na 506. [9] Katika makala ya kiutafiti kuhusiana na diwani ya Imam Ali ibn Abi Twalib (as) mashairi hayo ya diwani yamegawanywa katika mafungu manne: Insha, hekaya, usomaji (mashairi) na maudhui.

Historia na kukusanywa kwake Wahakiki wanasema, hata kama unasibishaji wa mashairi haya kwa Imam Ali (as) utakuwa sahihi, hapana shaka kwamba, mkusanyaji wa mashairi haya hakuwa yeye. Agha Bozorg Tehrani katika kitabu cha al-Dhariah ameleta orodha ya mafungu 17 ya mashairi yaliyokusanywa ambapo nakala kongwe zaidi inahusiana na karne ya 4 Hijria.

Chapa

Diwani ya Imam Ali (as) imechapishwa mara chungu nzima. [10] Agha Bozorg Tehrani anasema kuwa, chapisho kongwe kabisa la nakala diwani ni: Chapa ya Leiden Uholanzi 1745 Miladia, chapa ya Bulaq Misri ya 1251 Hijria, chapa ya Misri ya 1276 Hijria na chhapa ya Tehran ya 1284 Hijria. [11]

Tarjuma na sherhe

Diwani hii ya mashairi imetarjumiwa na kutolewa sherh (ufafanuzi) kwa lugha mbalimbali za Kifarsi, Kilatini, Kituruki na Kiurdu. Hii leo kuna nakala za machapisho mengi ya diwani hii ya mashairi.

Rejea

Vyanzo