Aqilah Banī Hāshim (Lakabu)

Kutoka wikishia
(Elekezwa kutoka Aqilah Banī Hāshim)


Aqilah Banī Hāshim: Jina la Aqilah Banī Hāshim, ni jina maalumu alilopewa Bibi Zainab (a.s.), ambaye ni binti wa Imam Ali (a.s). Kwa mujibu wa kamusi kuu ya Kiarabu iitwayo Lisān al-‘Arab, ni kwamba; Pale jina au neno "‘Aqilah," linapohusishwa na mmoja wa watu wa kabila au kundi fulani, huwa na maana ya mkuu wa kabila. [1] Baadhi ya wanazuoni, akiwemo Ayatollahi Jawadi Amuli, wamesema kuwa; pale jina hili linapotumika kwa mtu fulani, huwa na maana ya kumpa yeye kiwango cha sifa za juu kabisa (ijulikanayo kwa Kiarabu kwa jina la sighatu al-mubalagha), yenye kumaanisha mwenye akili na hekima mno. [2]

Jina hili la heshima halipatikani katika vitabu vinne mashuhuri vya Hadithi (Kutub al-Arba‘a) wala halikutajwa katika kitabu marufu Bihar al-Anwar; hata hivyo, linapatikana katika vitabu vyengine vya karne ya kumi na nne Hijiria, kama vile Maqtal al-Muqarram, [3] Minhāj al-Barā‘ah fī Sharhi Nahju al-Balāghah, [4] Tanqīhu al-Maqāl. [5] Pia jina hili ni mashuri ndani ya vilivoandikwa katika vipindi vya baadae. [6] Jina hili la heshima la "‘Aqilah," linalomhusu Bibi Zainab (a.s), limetumika katika vitabu kwa ibara kadhaa tofauti kama vile: ‘Aqilah Banī Hāshim Sayyidah Zainab (a.s.), al-Sayyidah Zainab ‘Aqīlat Banī Hāshim, Bibi Zainab ‘Aqilah Banī Hāshim, na Zainab Kubra ‘Aqilah Banī Hāshim. [7] Pia pale makhatibu mbali mbali wakati mwengine katika hotuba zao, humtaja kwa jina la "‘Aqilah Banī Hāshim" badala ya kumtaja kwa jina la Bibi Zainab. [8]

Abū al-Faraj al-Isfahānī, katika kitabu chake Maqātil al-Tālibīyīn, anamtaja "Zainab ‘Aqilah, binti wa ‘Alī bin Abī Tālib" kuwa ndiye mama wa ‘Awn bin ‘Abd Allāh bin Ja‘far, katika maelezo yake haya, yeye amehusisha maneno haya moja kwa na, akisema kwamba Ibn ‘Abbās amenukuliwa akisema: "Maneno haya nilihadithiwa na ‘Aqīlatuna (Mkomavu wetu wa akili), Zainab binti ‘Alī bin Abī Tālib (a.s)." [9]

Yasemekana kwamba; kule Bibi Zainab (a.s.) kuwa na hekima na akili komavu, ndiko kulikomuezesha yeye kuongoza msafara wa familia ya bwana Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) baada ya kutekwa kwao. Ambapo aliuongoza msafara huo kutoka Karbala hadi Kufa, kisha kutoka mji wa Kufa hadi Sham, halafu kutoka Sham hadi Madina, na baadae kuufikisha Madina. Akiwa pamoja na Imamu Sajjad (a.s), alichukua jukumu muhimu katika mikusanyiko ya kumkumbuka za maombolezo Imam Hussein (a.s) na kufichua uhalifu wa Bani Umayyah. [10]

Sayyid Muhammad ‘Alī Qādhi Tabātabā’ī (aliyefariki: 1399 H) [11] katika kitabu chake "Tahqīq dar Bāriye Awwal Arba‘īn Sayyid al-Shuhadā’ (a.s)" na Dhibīhullāhi Mahallā (aliyefariki: 1406 H), [12] wao kwa pamoja wameonekana kutumia jina la "‘Aqīlat al-‘Arab" kwa ajili ya Bibi Zainab (a.s) ndani ya vitabu viwili vyao hivi.