Al-Hujjah Ala al-Dhahib Ila Takfir Abi Talib (Kitabu)
Al-Hujjah Ala al-Dhahib Ila Takfir Abi Talib au “Imanu Abu Talib” ni kitabu muhimu cha kielimu kilichoandikwa na Sayyid Fakhar bin Ma’ad Musawi, ambay ni mwanazuoni maarufu wa Kishia aliyefariki mnamo mwaka 630 Hijiria. Kitabu hichi, kilicho andikwa kwa lugha ya Kiarabu, kiliandikwa kwa lengo la kuthibitisha imani ya Abu Talib, baba yake Imam Ali (a.s), ambaye alikuwa na nafasi muhimu katika historia ya Uislamu, na ndiye aliye kuwa mlinzi na mtetezi wa bwana Mtume (s.a.w.w). Mwandishi, Sayyid Fakhar bin Ma’ad Musawi, alitumia vyanzo mbalimbali vya kihistoria na kidini ili kuthibitisha imani ya Abu Talib. Katika kitabu hichi, amejikita kisawa sawa katika uchambuzi wa mashairi ya Abu Talib, ambayo yanathibitisha imani yake juu Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (s.a.w.w). Aidha, ametumia ripoti za kihistoria na Hadithi kadhaa zinazothibitisha msimamo wa Abu Talib kama muumini mwaminifu. Mbali na hayo, mwandishi pia alitumia maafikiano ya Ahlul-Bait (a.s) na wanazuoni wa Kishia kama ni hoja kamili za kuthibitishia hoja zake. Kitabu hichi muhimu kimepata umaarufu mkubwa miongoni mwa wanazuoni wa Kishia. Hata Allamah Amini, mwanazuoni maarufu aliyefariki mwaka 1390 Hijiria, alinukuu na kutegemea ripoti za kitabu hichi katika kazi yake mashuhuri chini ya jina la, “Al-Ghadir”, inahusiana na ushahidi wa kihistoria juu ya nafasi ya Ahlul-Bait. Pia, Ibn Abi al-Hadid Mu’tazili (aliyefariki mwaka 656 Hijiria), Sayyid Muhammad Sadiq Bahrul-Ulum (aliyefariki mwaka 1399 Hijiria), na Abdul Fattah Abdul Maqsud (aliyefariki mwaka 1372 Shamsiya) walitoa hati na waraka wa kuunga mkono kitabu hichi, wakikithamini kwa mchango wake mkubwa katika kudhihirisha ukweli wa imani ya Abu Talib. Miongoni mwa rejea za Sayyid Fakhar bin Ma’ad Musawi katika maandalizi ya kitabu hichi, ni rasala (tasnifu) chini ya jina la “Imani Abu Talib” iliyotungwa na Sheikh Mufid, mwanazuoni wa Kishia mwenye heshima kubwa mbele ya wafwasi wa madhehebu ya Kishia. Rasala hii ilimpa msingi muhimu katika uandishi wake, ikijumuisha hoja na ushahidi ambao umekuwa ndio msingi wa tafiti za baadaye kuhusiana na imani ya Abu Talib. Kitabu Al-Hujjah Ala al-Dhahib Ila Takfir Abi Talib kimechapishwa mara kadhaa, na hadi sasa kuna matoleo tofauti ya kitabu hichi. Mojawapo ya matoleo yake maarufu ni toleo la mwaka 1410 Hijiria, ambalo lilihaririwa na kusahihishwa na Sayyid Muhammad Bahrul-Ulum, na hatimae kuchapishwa na Shirika la Uchapishaji la Sayyid al-Shuhada huko Qom. Toleo hili lina kurasa 441 na limekuwa ni rejeleo muhimu kwa wale wanaotaka kufanya tafiti za ziada juu ya imani ya Abu Talib, na nafasi yake katika historia ya Kiislamu. Kitabu hichi bado kinaendelea kuwa ndio chanzo kikuu kwa wanazuoni na wafuasi wa Kishia katika kuelewa imani halisi ya Abi Talib.
Mwandishi Makala Kuu: Sayyid Fakhar bin Ma'ad Musawi Sayyid Fakhar bin Ma'ad Musawi (aliyefariki mwaka 630 AH) alikuwa mwanazuoni, mshairi, na mtaalamu wa utambuzi nasabu wa Kishia, ambaye ukoo wake unafikia kwa Ibrahim Mujab, mjukuu wa Imamu Kadhim (a.s). [1] Fakhar bin Ma'ad pia alikuwa ni mwalimu wa Muhaqqiq al-Hilli huku yeye akiwa ni mwanafunzi wa Ibn Idris al-Hilli, ambao wote walikuwa katika jopo la miongoni mwa wanasheria maarufu wa Kishia. [2]
Majina ya Vitabu na Vishawishi Vilivyo Amsha Dhamira ya Uandishi Wake Sayyid Fakhar al-Musaawi alikipa kitabu chake jina la "Al-Hujjah 'ala al-Zahibi ila Takfiri Abi Talib" (Ushahidi Dhidi ya Anayemwona Abu Talib Kuwa Kafiri). [3] Hata hivyo, Agha Bozorge al-Tehrani katika kitabu chake "Al-Dhari'ah" amekitaja kitabu hicho kwa majina mawili: "Hujjat al-Zahibu ila Imani Abi Talib" (Ushahidi wa Anayekubaliana na Imani ya Abu Talib) na "Al-Radd 'ala al-Zahibi ila Kufri Abi Talib" (Majibu Dhidi ya Anayemwona Abu Talib Kuwa ni Kafiri). [4] Walakini, Sayyid Muhammad Bahr al-Ulum, mchambuzi wa kitabu hicho, amekipa jina la "Iman Abi Talib" akisema kuwa; amefanya hivyo kufupisha kwa ajili ya kumvutia yeyote yule mwenye kukiona hicho. [5] Sayyid Fakhar al-Musaawi aliandika kitabu hichi kwa ajili ya kumtetea Abu Talib, baba wa Imam Ali (a.s) na kuthibitisha imani yake mbele ya wanao kanya na kupinga ukweli huo. Kama alivyoeleza katika utangulizi wa kitabu chake kwamba; kundi fulani, kutokana na uadui wao dhidi ya Imam Ali (a.s), wameamua kukanusha imani ya Abu Talib na kumweka kwenye kundi la makafiri na washirikina, bila kujali mashairi ya Abu Talib pamoja na ripoti za kihistoria na Hadithi zinathibitisha imani na nafasi katika Uislamu. [6]
Umuhimu wa Kitabu Kitabu "Al-Hujjah 'ala al-Zahib ila Takfir Abi Talib" kinahisabiwa kuwa moja ya vitabu bora zaidi vilivyoandikwa katika kuthibitisha imani ya Abu Talib. [7] Kitabu hichi kimepata umaarufu mkubwa miongoni mwa wanazuoni wa Kishia, ambapo hata Allama Amini (aliyefariki mwaka 1390 AH) alikitumia kama ni moja reje za kitabu chake "Al-Ghadir." [8] Umuhimu wa kitabu hichi ni mkubwa mno kiasi kwamba kimewafanya baadhi ya wanazuoni wa Kishia na Sunni kuandika waraka maalumu wa kukiunga mkono kitabu hicho. Miongoni mwao ni waraka wa maelezo wa Ibn Abi al-Hadid al-Mu'tazili (aliyefariki mwaka 656 AH), ambaye mtaalamu wa elimu ya dini kutoka upande wa madhehebu ya Ahlu Sunna, waraka wa Sayyid Muhammad Sadiq Bahr al-Ulum (aliyefariki mwaka 1399 AH) na waraka Abd al-Fattah Abd al-Maqsud (aliyefariki mwaka 1372 SH). [10] Tafsiri ya sehemu ya maelezo ya waraka wa Muhammad Sadiq Bahr al-Ulum, ambao aliyapanga kwa mfumo wa nathari na kunukuliwa na Allama Amini, ni kama ifuatavyo: "Ewe Fakhar, hongera kwa bishara za thawabu utakazopewa na Mola Muumba siku ya Kiyama. Kwa hoja yako iliyo wazi na maandiko yako yenye kung'aa, yalioko kwenye tungo yenye jina la “Al-Hujjah”, umeweza kumsafisha mtukufu wa Makkah na baba wa Simba wa Mwenyezi Mungu kutokana na tuhuma za uabudu masanamu na pia dhidi ya tuhuma ya kufuru alizotwishwa na watangazaji wa idhaa ya uovu." [11]
Yaliyomo Mada kuu ya kitabu "Al-Hujjah 'ala al-Zahib ila Takfir Abi Talib" ni kuthibitisha imani ya Abu Talib. [12] Mwandishi ametumia makubaliano ya Ahlul Bait pamoja na muwafaka wanazuoni wa Kishia kama ni hoja na ushahidi kamili wa kuthibitisha imani ya Abu Talib, akisema kuwa; kama Abu Talib hakukuwa na tabia au nyenendo na lugha ya maneno yaendayo sawa na tabia za waumini na Waislamu, kusingekuwepo na madai ya kumtambua yeye kama ni muumini. [13] Mwandishi katika uandishi wa kitabu chake, alitumia kitabu cha Sheikh Mufid (aliyefariki mwaka 413 AH) kiitwacho "Risalah Iman Abi Talib" kama ni rejeo laku muhimu katika uandishi wa kitabu hiko. [14]
Kitabu Al-Hujjah 'ala al-Zahib ila Takfir Abi Talib" kimechapishwa kikiwa na utangulizi, sura kumi, pamoja na hitimisho: • Utangulizi: Sababu za kuandika kitabu na maelezo juu ya nafasi ya mababu wa bwana Mtume (s.a.w.w) na Abu Talib. • Sura ya Kwanza: Maana ya imani na uthibitisho wa imani ya Abu Talib kwa njia mbalimbali. • Sura ya Pili: Hoja za wale wanaodai kuwa Abu Talib alikuwa ni kafiri na majibu yao. • Sura ya Tatu: Uthibitisho wa imani ya Abu Talib kwa kutegemea mapenzi ya Mtume (s.a.w.w) kwa Abu Talib na umarufuku wa kuwa na urafiki na makafiri. • Sura ya Nne: Maneno na mashairi ya Abu Talib yanayo ashiria uhakika wa imani yake. • Sura ya Tano: Hadithi ya kupotea kwa kwa Mtume (s.a.w.w) na Imam Ali (a.s) na Abu Talib kumwagiza mwanawe Ja'far asali pamoja nao. • Sura ya Sita: Kifo cha Abu Talib na amri ya bwana Mtume (s.a.w.w) ya kumuosha na kumzika. • Sura ya Saba: Wema wa Abu Talib kwa kwa Mtume (s.a.w.w) na mashairi yanayo onesha Uislamu wake. • Sura ya Nane: Uthibitisho wa imani ya Abu Talib kwa mashairi ya Qasida ya Lamiyah na matukio kadhaa ya kihistoria. • Sura ya Tisa: Wasia wa Abu Talib kwa wanafamilia yake kumuunga mkono bwana Mtume (s.a.w.w) pamoja na sababu za kisiasa za kuibua mashaka juu ya imani yake. • Sura ya Kumi: Sababu za Abu Talib kuficha Uislamu wake na mlingano wake na As-habul Kahf na Muumini wa Firauni waliokuwa wakificha imani zao. [15] • Hitimisho: Mwandishi ameeleza kuwa; hapo awali alikusudia kuandika kuhusiana na maisha, imani, na sifa za mababu wa bwana Mtume (s.a.w.w) kuanzia Abdullah bin Abdul Muttalib hadi Adnan, na pia alikusudia kufafanua mashairi ya Abu Talib wakati wa kuyanukuu kwake, lakini ili kuepuka urefu wa kitabu chake, aliamua kuelezea tu imani ya Abu Talib peke yake. [16]
Uchapishaji Kwa mara ya kwanza kabisa, kitabu hichi kilichapishwa mnamo mwaka 1351 Hijria kupitia taasisi ya “Al-Matba'atu al-Alawiyya” huko Najaf nchini Iraq. [17] Qasida ya Sheikh Muhammad Samawi kumtukuza Abu Talib pia iliongezwa kwenye kitabuni humo kwenye toleo hilo. [18] Katika toleo hili, kitabu asili kilikuwa na kurasa 118, na kurasa 22 ziliongezwa mwanzoni na mwishoni mwa kitabu hicho. [19] Mnamo Mwaka 1408 Hijria, Dar al-Zahra ilioko mjini Beirut ilichapisha tena kitabu hicho, safari hii kilichapishwa kikiwa na kurasa 448. [20] Pia, Sayed al-Shuhada Publications ilioko Qom nchini Iran, ilichapisha kitabu hichi mwaka 1410 Hijria baada ya kupitiwa na kuhaririwa na Sayyid Muhammad Bahr al-Ulum. Katika toleo hili, Aya za Qur'ani na Hadithi zimewekewa rejea zilirejelea kwe Qur'ani na vitabu husika vya Hadithi. [21]
Aidha toleo hili lilijumuisha orodha mbalimbali ziliongezwa ndani yake, zikiwemo orodha ya yaliyomo, orodha ya wasifu wa watu waliotajwa kwenye maelezo ya chini ya kurasa, orodha ya majina maarufu, na orodha ya vyanzo vya utafiti. [22]
Nakala Zilizo Andikwa kwa Hati za Mkono Baadhi ya nakala za mkono za kitabu "Al-Hujjah 'ala al-Zahib" ni kama zifuatazo: 1. Nakala iliyokuwa mikononi mwa Sayyid Sadiq Kammunah, ambayo inahusishwa na karne ya 8 au 9 Hijria. Nakala hii ina kurasa 158, na kila ukurasa una mistari 15. [23] 2. Nakala iliyoandikwa kwa mkono na Mirza Muhammad Tehrani Askari, iliyokopiwa kutoka nakala ya maktaba ya Sadaat Al-Atar huko Baghdad. [24] 3. Nakala ya mwaka 1344 Hijria, ambayo inasemekana kuwa iliandikwa kwa mkono na Sheikh Ali Kashif al-Ghita, baba wa Muhammad Hussein Kashif al-Ghita. Nakala hii ina kurasa 122, na kila ukurasa una mistari 18, na kwa hivi sasa inahifadhiwa katika maktaba ya Muhammad Hussein Kashif al-Ghita chini ya hifadhi nambari 614. [25] Mada Zinazohusiana • Imani ya Abu Talib (Kitabu) • Imani ya Abu Talib • Orodha ya Vitabu Kuhusiana na Abu Talib