Ujauzito wa Bibi Mariamu (s.a)

Kutoka wikishia

Ujauzito wa Bibi Mariamu (s.a) (حَمل السيدة مريم بعيسى) ni muujiza uliotokea katika mazingira maalumu kabisa, ambapo Bibi Mariamu binti wa Imrani (s.a), alipata ujauzito bila kushiriki tendo la ndoa na mwanamme yeyote yule, na matokeo yake ikawa ni kuzaliwa kwa Nabii Isa (a.s). Tukio hili la ujauzito wa Bibi Mariamu (s.a), limeelezwa wazi kabisa katika Qur'ani na Injili huku kukiwa na hali fulani ya kufanana juu ya sifa za Bibi Mariamu (s.a) ndani ya riwaya ya vitabu viwili hivyo.

Kulingana na Qur'ani, Bibi Mariamu (s.a) alikuwa amejitenga na watu kwa ajili ya ibada katika eneo la faragha, ghafla malaika wa Mwenye Ezi Mungu alimtokea na kumpa habari ya kupata mtoto. Qurani inaelezea jinsi ujauzito huo wa Bibi Mariamu (s.a) ulivyotokea kwa maneno yasemayo: “Na tukampulizia ndani yake roho kutoka kwetu.” Baadhi ya wafasiri wanaamini kuwa hakuna maelezo kamili yanayo patikana katika upeo wa sayansi ya kibinadamu kuhusiana na jinsi gani Bibi Mariamu (s.a) alivyoweza kupata ujauzito.

Kulingana na Aya za Surat Mariamu ni kwamba; baada ya kukamilisha kipindi cha ujauzito, Bibi Mariamu (s.a) alipata maumivu ya hali ya kujifungua ambayo yalimlazimisha kuelekea kando ya mti wa mtende; hali hiyo ilimfanya Bibi Maria atamani mauti. Wafasiri wamyaelezea maneno hayo ya Bibi Mariamu (s.a), kuwa ni maneno yanayo tokana na hofu ya kulaumiwa na watu. Kulingana na maelezo ya Qur'ani; Mwenye Ezi Mungu alimwambia Bibi Mariamu (s.a) asihuzunike na ili kupunguza mateso yake, chemchemi ya maji ilianza kutiririka chini yake na tende mpya zikapatikana kutoka kwenye mtende alio uegemea. Pia Bibi Mariam (s.a) alitakiwa kuwa mchangamfu katika kukabilana na mtoto wake mchanga.

Kulingana na Aya za Qur'ani, Bibi Mariamu (s.a), ambaye alikuwa na hofu ya kukutana na watu, aliamrishwa kufunga saumu ya kuto zungumza na mtu, naye akarejea kwa watu wake akiwa pamoja na mwanawe. Kulingana na Aya ya 156 ya Surat An-Nisa; Bibi Mariamu (s.a) alishutumiwa shutuma kubwa mno kutokana na mimba na kujifungua bila ya kuwa na mume. Bibi Mariamu (s.a) akijibu shutuma hizo alielekeza ishara zake kwa mwanawe, na kwa muujiza wa kimungu, mtoto huyo alifungua kinywa chake na akasema: “Mimi ni mtumishi wa Mwenye Ezi Mungu. Amenipa Kitabu (cha mbinguni) na amenifanya kuwa Mtume.” Kulingana na baadhi ya Wfasiri, kwa muujiza huu, Isa (a.s) aliweza kuthibitisha utakatifu na kufuta tuhuma dhidi ya mama yake.

Muujiza wa Mimba ya Bibi Mariamu (a.s)

Tukio la ajabu na la kimiujiza la mimba ya Bibi Mariamu (s.a) linapatikana katika Injili na Qur'ani. Vitabu viwili hivi vimelielezea tukio hili kwa namna inayo fanana, haidhuru tofauti fulani katika nukuu za vitabu hivyo kuhusiana na kisa hicho.[1] Wafasiri wa Qur'ani wameelezea na kusifu tukio la mimba ya Bibi Mariamu (s.a) -ambaye hakuwa na mahusiano yoyote na mwanaume-, kama ni muujiza mkubwa, kitendo cha kipekee,[2] na Hadithi ya ajabu.[3] Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah (aliyefariki mwaka 1389 Shamsia), mfasiri wa Shia, aliuona kuwa asili ya muujiza uliopo katika tukio hili, ni kwamba; tukio hili la kuzaliwa kwa nabii Isa (a.s), limetokea kwa njia tofauti kabisa na zile zilizo zoeleka katika kuzaliwa kwa wanadamu, ambapo mtoto huyu alizaliwa kutoka kwa mama ambaye hakuwa na mahusiano ya kindoa na wanaume.[4] Mwenye Ezi Mungu katika Qur'ani amewataja Mariamu (s.a) na mwanawe Isa (Yesu) (s.a) kama ishara (Aya au ashirio la Mungu) kwa ulimwengu.[5] Sababu ya tukio hili kupewa sifa maalumu, linatokana na kule mwanamke bikira kupata mtoto bila ndoa au kuwa na mahusiano ya kindoa na mtu fulani, tukio ambalo limekuwa likizingatiwa kama ni muujiza mkubwa na ishara (Aya au ashirio la kuwepo kwa Mungu) kwa watu katika nyakati zote.[6]

Katika Qur’an, utakatifu wa Bibi Mariamu (a.s), umetajwa katika Sura mbili tofauti, nazo ni Surat al- Anbiya[7] na surat Tahrim.[8] Kutilia mkazo utakatifu wa Bibi Mariamu (a.s) katika Qur’an kumekuwa ni jibu dhidi ya shutuma za Wayahudi zilizo elekeza kwa Bibi Mariamu (a.s).[9] Katika baadhi ya riwaya za Kishia zinazo husiana na tafsiri ya Qur’ani, imeelezwa ya kwamba; ujauzito wa Bibi Mariamu (a.s) ulitokana na kupulizwa tu na malaika.[10] Katika Qur'an, uumbwaji wa Nabi Isa (a.s) umefananishwa na uumbwaji wa Adamu (a.s).[11] Sayyid Muhammad Husseinn Tabatabai (aliyefariki mwaka 1360 Shamsia), ambaye ni mfasiri wa Qur’ani wa Kishia, ameona kuwa; kiungo cha tasbihi hii ilioko katika Qur’ani, kinatoa sura kamili ya kwamba; mfanano uliopo baina Isa (a.s) na Adamu (a.s), ni kwamba wote wawili wameumbwa bila kuwa na baba.[12]

Uzaaji wa Bikira kwa Mtazamo wa Kisayansi

Nasser Makarim Shirazi, mfasiri wa Qur’ani wa Shia, amechopoa swali la kitaalamu kuhusiana na tukio la mimba ya Bibi Mariamu (s.a), akitoa uchambuzi wa swali lake amesema kwamba; “Tukiachana na upande wa ajabu na kimiujiza wa tukio hilo, je kisayansi, kuna uwezekano wa mtoto kuzaliwa bila baba?[13] Kulingana na maelezo ya Makarim Shirazi, kwa maendeleo ya sayansi yalio fikiwa katika zama za kisasa, bila shaka uwezekano wa jambo hili umekuwa sio ndoto tena, na wala si jambo la kushangaza, kwani jambo limesha thibitishwa katika zama zetu za leo.[14] Kibaiolojia uzalishaji wa viumbe ambao hukamilika kwa kupatikana kwa kiinitete, unahitaji jinsia ya kike tu, na jinsia ya kiume haina jukumu lolote katika uzalishaji wa uzao.[15] Inasemekana kuwa, kimaumbile aina hii ya uzaaji kupitia jinsia ya kike tu, inaweza kutimia kwa njia mbili; kupitia maumbile asilia au njia za kitaalamu, ambapo njia ya kimaumbile imeweza kugundilwa katika baadhi ya wadudu, yaani kuna wadudu amabo huzaa blia ya kuhitaji uwepo wa jinsia ya kiume.[16] Aidha aina ya pili (ya kitaalamu), imeweza kuthibitishwa kupitia majaribio mbali mbali.[17] Ripoti zinazo onesha kuwa; kuna jitihada kadhaa zilizo fanyika kwa nia ya kukamilisaha kitendo hiki kwa ajili ya kuzalisha mamalia, ambapo licha ya mafanikio ya awali,[18] ila bado hakuna uthibitisho wa kisayansi ulioweza kuidhinisha jambo hilo kwa ajili ya wanadamu.[19]

Ujauzito wa Bibi Mariamu (a.s) na Uchambuzi wa Tukio Hilo

Kwa mujibu wa Aya za Qur’ani, Bibi Mariamu (a.s) alikuwa amejitenga na watu[20] na kukaa katika eneo maalumu la faragha, lililopo kwenye upande wa mashariki wa Msikiti wa Al-Aqsa[21] kwa ajili ya kutenda ibada.[22] Akiwa huko, ghafla alitokewa na malaika, aliye tambuliwa katika Surat Aal-Imran kama ni Malaika[23] na katika Surat Maryam kama ni roho.[24] Wafasiri wamemtambua Mailka huyo kwa jina la Jibril.[25] Katika Surat Maryam, imebainishwa ya kwamba; katika tukio hilo, malaika alimtokea Bibi Mariamu (a.s) akiwa katika mfumo wa umbile la kibinadamu. [26] Kulingana na maeelezo ya wafasiri wa Qur’ani, tukio hili lilimkhofisha Bibi Mariamu (a.s).[27] Kulingana na wafasiri wa Qur’ani, Bibi Mariamu (a.s) alimwomba kinga kutoka kwa Mola wake dhidi ya uovu wa mtu yule (malaika) aliye mjia kwa ghafla bila ya matarajio.[28] Kulingana na Aya za Surat Aal-Imran na Suratu Maryam, na pia kulingana na baadhi ya tafsiri za Qurani, malaika huyo alijiarifisha kwa Bibi Mariamu (a.s) kama ni mtumwa aliyetumwa kwa amri ya Mungu,[29] aliyekuja kumletea Bibi Mariamu (a.s) habari njema kutoka kwa Mola wake[30] za kuzaliwa kwa mtoto maalumu kupitia kwake.[31] Katika Aya ya Surat Aal-Imran, mtoto huyu anaitwa Masihu bin Mariam (a.s), na anajulikana kuwa ni mmoja wa walio karibu na Mwene Ezi Mungu.[32] Kulingana na Qurani, pale Bibi Mariamu (a.s) alipo juzwa juu ya habari na Malaika huyo, aliuliza; ni jinsi gani nitakuwa ni mama wa mtoto, huku kukiwa hakuna mwanaadamu aliye nigusa,[33] na pia mimi sijawahi kuwa ni mwanamke mtenda dhambi (mzinifu).[34] Kulingana na Aya ya Suratu Maryam, Malaika huyo alimtambulisah Bibi Mariamu (a.s) ya kwamba; suala la kuzaliwa kwa mtoto bila baba, ni jambo rahisi mno mbele ya Menye Ezi Mungu.[35]

Kwa mujibu wa maoni ya Makarim Shirazi, Qurani haisemi kitu chochote kile kuhusu muda wa ujauzito wa Bibi Mariamu (Bikira Maria) (a.s),[36] Ila kwa upande wa wafasiri wa Qur’ani kuna maoni mbalimbali kuhusiana muda huo:[37] Wengine wanasema kuwa ujauzito huo ulichukua kipindi cha masaa machache tu,[38] huku wengine wakisema kuwa mimba wake ilichukua kipindi miezi tisa.[39] Pia katika riwaya mbali mbali kuna mida tufauti iliyo ripotiwa juu ya ujauzito wa Bibi Mariamu (a.s).[40] Ibn Kathir, ambaye ni mmoja wa mfasiri wa kutoka upande wa madhehebu ya Sunni, anasema kuwa; maoni maarufu juu ya muda wa ujauzito wake ni miezi tisa. [41]

Jinsi ya Uchukuaji Mimba wa Bibi Mariamu (a.s)

Kwa mujibu wa maoni ya Makarim Shirazi; Qur’an haitoi maelezo ya wazi kuhusiana na jinsi ya Bibi Mariamu (a.s) alivyo pata mimba, na badala yake inataja maelezo mafupi tu yasemayo: “Tulimpulizia ndani yake Roho yetu”.[42] Katika riwaya za Kishia zinazohusiana na tafsiri ya Qur’ani, imeelezwa kuwa; mimba yake ilikamilika kupitia mpulizo wa Malaika peke yake.[43] Bwana Makarim Shirazi amenukuu na kuandika maoni tofauti kutoka kwa wafasiri wa Qur’ani kuhusiana na jinsi ya utungaji wa mimba hiyo;[44] baadhi ya wafasiri wanaamini kuwa; mimba ya Bibi Mariamu (a.s), ilikamilika kupitia mpulizo wa Jibrilu alio upuliza ndani ya shingo ya vazi la Bibi Mariamu (a.s).[45] Imeelezwa ya kwamba; tafsiri hii ni tafsiri ya kimethali au kimifano, na maana ya vazi katika tafsiri hiyo ni tumbo la uzazi.[46] Sheikh Tusi (aliyefariki: mwaka 460 Hijiria), ambaye ni mfasiri wa Kishia, ameona kuwa; kauli hii ni kauli dhaifu isiyo na hadhi ya kupewa uzito.[47] Allama Tabatabai anachukulia suala hili la kupulizwa kwa roho ndani ya Bibi Mariamu (a.s), kuwa ni ishara ya maumbile yasiokuwa ya kawaida yaliotumika katika kuumbwa kwa Nabi Isa (a.s), ambaye kiuhalsia aliumbwa kwa jinsi tofauti na watu wengine. Kuja kwake kulitokea bila ya bila kufuata hatua na njia za kawaida, ambaye kuumbwa kwake kulikuwa ni matokeo ya irada(mapenzi) kamili ya Mwenye Ezi Mungu.[48] Muhammad Jawad Maqhiyya (aliyefariki mwaka 1400 Hijiria), ambaye ni mfasiri wa Kishia, anachukulia mchakato huu wa mimba ya Bibi Mariamu (a.s), na mfumo mzima wa kuumbwa kwa Nabi Isa (a.s), kuwa ni mambo ambayo hakuna mtu yeyote wa kawaida anaye anaye weza kupata ufahamu kamili juu yake, na ni Mwenye Ezi Mungu peke yake ndiye anayejua kiukamilifu kuhusiana na tukio hilo.[49]

Kutamani Mauti Hadi Kuzaliwa kwa Nabi Isa (a.s)

«Kuzaliwa kwa Masih» na mchoraji: Hussein Behzad; Kazi Iliyochaguliwa Katika Shindano la Kimataifa la Uchoraji Huko New York (1958).[50]

Kwa mujibu wa Qur’ani; Bibi Mariamu (s.a) aliondoka na kujitenga na watu, na akaelekea mahali ambapo alibaki mbali na watu.[51] Baadhi ya wafasiri wanaamini kwamba; mahali hapo palikuwa ni mji wa Naasira uliopo ndani ya mji wa Palestina ya leo.[52] Kulingana na moja ya Aya za Suratu Mariamu ni kwamba, wakati wa kujifungua kwa Bibi Mariamu (s.a), uchungu wa mimba hiyo ulimpeleka kwenye mtende[53] mkavu.[54] Wakati huo, Bibi Mariamu (s.a) alitamani kufa, hisia ambayo imenukuliwa na Qur’ani kwa kusema: “Yalaiti ningelikuwa nimekufa kabla ya haya na ningelikuwa nimesahaulika kabisa kabisa.”[55] Sababu ya Bibi Mariamu (s.a) kuwa na hisia hiyo imeelezwa kuwa; ni aibu ya kukabiliana na watu,[56] hofu ya shutuma kutoka kwao,[57] na hofu ya kupoteza heshima na hadhi yake.[58]

Sayyid Muhammad Taqi Mudarris, mfasiri wa Kishia, ameeleza sababu ya kauli hiyo ya Bibi Mariamu (s.a), akisema kuwa; Bibi Mariamu (s.a) alikuwa ni msichana mdogo ambaye alikuwa ameachana kabisa na dunia na hakuwa na jukumu lolote lile la kibinafsi au kijamii; sasa mwanamke kama huyo amepata maumivu ya uzazi na hajui cha kufanya. Baada ya yeye kuelewa matokeo mazito ya kijamii ya tukio kama hilo, yeye anatamani kuwa; kufa ni bora zaidi kuliko kukabiliana na hayo.[59] Makarim Shirazi anaona kuwa; ombi hilo la kifo kutoka kwa Bibi Mariamu (s.a) linaonesha kuwa; yeye alikuwa akienda ucha Mungu zaidi kuliko hata roho yake.[60]

Kwa mujibu wa maelezo ya Aya za Qurani; baada ya Bibi Mariamu (s.a) kutamani mauti, sauti ilimfikia kutoka chini yake,[61] ikimtuliza au kumbembeleza na kumwondolea huzuni.[62] Baadhi wanazuoni wamedai ya kwamba; mtoa sauti hiyo alikuwa Nabi Isa (a.s) na wengine wamedai kuwa alikuwa Jibrilu (a.s).[63] Kulingana na Qur’ani, Mwenye Ezi Mungu alijaalia mto mdogo uanze kutiririka kutoka chini ya miguu ya Bibi Mariamu (s.a),[64] naye akaletewa tende mbichi kutoka kwenye mtende aliopo chini.[65] Wafasiri wa Qurani wamesema kwamba; baada ya hayo, Bibi Mariamu (s.a) alipewa maagizo ya kula, kunywa maji, na kufurahie kwa kupata mtoto kama huyo.[66]

Vilevile tazama: Aya ya 23 Surat Maryam na Aya ya 26 Surat Maryam

Kurudi kwa Bibi Mariamu (a.s) Mbele ya Watu wake na Kukabiliana Nao

Kurejea kwa Bibi Mariamu (s.a.) mbele ya watu wake kulingana na Qurani, ni kwamba; Yeye pamoja na mwanawe (s.a) walirudi mbele ya watu na kukabiliana nao, baada ya kujifungua kwake mtoto huyo.[67] Kulingana na tafsiri za Qurani; wakati huo Bibi Mariamu (s.a) alipewa amri ya kutokusema na mtu yeyote ambapo aliamuria kufunga saumu ya kukaa kimya.[68] Kulingana na Qurani, watu wa jamii yake walikabiliana na Bibi Mariamu (s.a) maneno ya dhihaka[69] na walimwambia kwamba amefanya kitendo kiovu kilioje.[70] Qur’ani ikinukuu hayo inasema: “Ewe dada wa Haruna, [Maelezo 1] baba yako hakuwa ni mtu mbaya wala mama yako hakuwa mzinifu.”[71] Qurani inahesabu maneno haya kuwa ni maneno ya uongo na shutuma kubwa zisizo na mashiko.[72]

Kwa mujibu wa maoni ya Faidhu Kashani, Bibi Mariamu (s.a) alimwashiri mwanawe kwa ajili ya kujibu shutuma za watu wake.[73] Kulingana na Aya ya Suratu Maryam, wao walijiuliza kimshangao, ni jinsi gani wataweza kuzungumza na mtoto aliye mbelekono.[74] Inasemekana kuwa papo hapo -kupitia miujiza ya kimungup- Nabi Isa (a.s) alifungua kinywa chake na kusema:[75] “Mimi ni mtumishi wa Mwenye Ezi Mungu, Amenipa Kitabu (cha mbinguni) na akanifanya kuwa ni Mtume”.[76] Baadhi ya wafasiri wanaamini kuwa; Kutpia muujiza huu, Nabi Isa (a.s) aliweza kuthibitisha unyoofu na usafi wa khulka za mama yake.[77] Tofauti Kati ya Riwaya ya Qurani na Injili Kuhusiana na Ujauzito wa Bibi Mariamu (a.s)

Tofauti Baina ya Qur'an na Injili Juu ya Mimba ya Bibi Maryam (s.a)

Baadhi ya watafiti wamebainisha kwamba; kwa kuchunguza taswira na mtazamo wa Qura’ani na Injili kuhusiana na Bibi Mariamu, wamefikia hitimisho la kwamba; Qur’ani imemsifu na kumpa hadhi maalumu Bibi Mariamu (a.s), ila katika Injili, utakuta Bibi Mariamu (a.s) hutajwa tu katika matukio au masuala yanayo husiana na Nabi Isa (a.s). Thamani ya Bibi Mariamu (a.s) aliyo pewa na Injili, iantokana na kule yeye kuwa ni mama wa Nabi Isa (a.s), ila Qurani inamthamini Bibi Mariamu (a.s) kupitia hadhi binafsi, bila ya kujali ni mama wa mtu gani, yaani anathaminiwa yeye kama yeye sio kutokana na uzito wa mtu fulani.[78] Riwaya ilioko katika Qurani kuhussiana na asili ya tukio na kisa cha ujauzito wa Bibi Mariamu (a.s), ni riwaya yenye maelezo na ufafanuzi zaidi ikilinganishwa na riwaya iliopo ndani ya Injili;[79] Qurani na Injili zinawafikiana kuhusu ubikira wa Bibi Mariamu (a.s), lakini katika hadithi ya Injili kuna maelezo ya ziada kuhusiana na Bibi Mariamu (a.s), kabla ya ujauzito wake. Maelezo hayo ya zziada yaliopo katika Injili hayapatikani katika Qurani, miongoni mwayo ni pamoja na maelezo yasemayo kwamba; Bibi Mariamu (a.s) alikuwa ameposwa na mtu aitwaye Yusufu ila kabla ya ndoa yao, Bibi Mariamu (a.s) akawa tayari amekwisha pata ujauzito.”[80]

Kuna tofauti kubwa katika riwaya za Qurani na Injili kuhusiana na matukio yaliyo fuatia baada ya ujauzito wa Bibi Mariamu (a.s). Katika Qurani imeelezwa kwamba; Wakati wa kujifungua Bibi Mariamu (a.s) alikuwa nje ya mji huku akiwa peke yake chini ya mtende mkavu, lakini katika hadithi ya Injili, imeripotiwa kwamba; Yeye (a.s) alikuwa nyumbani kwa Yusufu au katika nyumba fulani ya wageni ilioko ndani ya mjini.[81] Katika Qurani imeelezwa ya kwamba; Nabi Isa (Yesu) (a.s) alizingumza akiwa bado ni mtoto mchanga ili kuthibitisha utakatifu na usafi wa mama yake, lakini katika Injili hakuna riawaya kama hiyo.[82] Pia katika Qurani, Nabi Isa (a.s) anatoa ushahidi wa unabii wake akiwa bado ni mtoto mchanga, ila katika Injili imeelezwa ya kwamba; unabii wa mtoto huyu ulikuja kuligunduliwa watu wengine kabisa, kama vile wachungaji na wanajimu.[83]

Maelezo

  1. Makarem Shirazi amesema ya kwamba; ufafanuzi bora zaidi kuhusiana na ibara hii ni kwamba: Haruna (Aaron) alikuwa mtu msafi na mwadilifu, na alikuwa ni mtu mwenye kupigiwa mfano kati ya wana wa Waisraeli, na mtu yeyote yule waliotaka kuonesha kwamba yeye ni mtu msafi na mwaminifu, walikuwa wakimnasibisha na Haruna wakisema; Yeye ni kaka au dada wa Haruna. (Makarem Shirazi, Tafsiri Nemune juz 1, uk 51, chapa ya mwaka 1374 Shamsia.

Rejea

  1. Puya, Tavallud-e Masih-e (a.s) dar Qur'an va Injili, uk. 3.
  2. Ja'fari, Tafsir Kausar, juz. 2, uk. 125.
  3. Zuhaili, Tafsir al-Wasit, juz. 2, uk. 1468.
  4. Fadhlullah, Tafsir Min Wahyi al-Qur'an, juz. 15, uk. 30.
  5. Surat al-Anbiya: Aya ya 91.
  6. Mudarrisi, Min Huda al-Qur'an, juz. 7, uk. 370.
  7. Surat al-Anbiya: Aya ya 91.
  8. Surat Tahrim: Aya ya 12.
  9. Tahiri-Niya, Sakhtar-e Neshaneh-i Shakhshiyat-e Hazrat-e Maryam dar Qur'an-e Karim, uk. 51.
  10. Tabrasi, Majma' al-Bayan, juz. 6, uk. 789.
  11. Surat al-Imran: Aya ya 59.
  12. Tabatabai, al-Mizan, juz. 3, uk. 212.
  13. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 13, uk. 58.
  14. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 13, uk. 58.
  15. Bikrzai Inqilabi dar Danesh-e Taulid Mithli, site irna.ir.
  16. Tahqiq dar Maurid Bikrzai, site magirans.com.
  17. Tahqiq dar Maurid Bikrzai, site magirans.com.
  18. Bikrzai Inqilabi dar Danesh-e Taulid Mithli, site irna.ir.
  19. Bikrzai Inqilabi dar Danesh-e Taulid Mithli, site irna.ir.
  20. Surat Maryam: Aya ya 17.
  21. Tabatabai, al-Mizan, juz. 14, uk. 35.
  22. Tabatabai, al-Mizan, juz. 14, uk. 35.
  23. Surat al-Imran: Aya ya 45.
  24. Surat Maryam: Aya ya 17.
  25. Tazama: Mughniyah, Tafsir al-Kashif, juz. 2, uk. 63.
  26. Surat Maryam: Aya ya 17.
  27. Tazama: Zuhaili, Tafsir al-Wasit, juz. 2, uk. 1468.
  28. Tazama: Najafi Khomeini, Tafsir Āsan, juz. 2, uk. 315.
  29. Surat Maryam: Aya ya 19.
  30. Surat al-Imran: Aya ya 45.
  31. Tazama: Husseini Hamdani, Anwar Derakhshan, 1404 H, juz. 3, uk. 78.
  32. Surat al-Imran: Aya ya 45.
  33. Surat al-Imran: Aya ya 45.
  34. Surat Maryam: Aya ya 20.
  35. Surat Maryam: Aya ya 21.
  36. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, 1374 S, juz. 13, uk. 40.
  37. Ibnu Kathir, Tafsir al-Quran al-Adhim, 1420 H, juz. 5, uk. 196.
  38. Faidh Kashani, Tafsir al-Safi, juz. 3, uk. 277.
  39. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, 1374 S, juz. 13, uk. 40.
  40. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, 1374 S, juz. 13, uk. 40.
  41. Ibnu Kathir, Tafsir al-Quran al-Adhim, juz. 5, uk. 196.
  42. Surat Maryam: Aya ya 12.
  43. Tazama: Maqatil bin Suleiman: Tafsir Maqatil bin Suleiman, juz. 4, uk. 380.
  44. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 13, uk. 39.
  45. Tazama: Maqatil bin Sulaiman: Tafsir Maqatil bin Suleiman, juz. 4, uk. 380.
  46. Tusi, al-Tibyan, juz. 10, uk. 54.
  47. Tusi, al-Tibyan, juz. 7, uk. 276.
  48. Tabatabai, al-Mizan, juz. 14, uk. 316.
  49. Mughniyah, Tafsir al-Kashif, juz. 2, uk. 10.
  50. «[https://sadmu.ir/detail/8007 «Kuzaliwa kwa Masih / Makumbusho katika mji wa Behzad», Miongoni mwa tamaduni za kihistoria katika mji wa Saad-Abad.
  51. Sadiqi Tehrani, al-Balagh, uk. 306.
  52. Tazama: Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, juz. 13, uk. 40.
  53. Tabatabai, al-Mizan, 1417 H, juz. 14, uk. 42.
  54. Surat Maryam: Aya ya 23.
  55. Surat Maryam: Aya ya 23.
  56. Tabatabai, al-Mizan, 1417 H, juz. 14, uk. 42.
  57. Baidhawi, Anwar al-Tanzil, juz. 4, uk. 8.
  58. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, 1374 S, juz. 13, uk. 44.
  59. Mudarrisi, Min Huda al-Quran, juz. 7, uk. 32.
  60. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, 1374 S, juz. 13, uk. 44.
  61. Surat Maryam: Aya ya 24.
  62. Surat Maryam: Aya ya 24.
  63. Tabrisi, Majma' al-Bayan, juz. 6, uk. 790; Ja'fari, Tafsir Kauthar, juz. 6, uk. 510.
  64. Shaibani, Nahj al-Bayan, 1413 H, juz. 3, uk. 309.
  65. Surat Maryam: Aya ya 25.
  66. Makarim Shirazi, Tafsir Nemuneh, 1374 S, juz. 13, uk. 42.
  67. Surat Maryam: Aya ya 25
  68. Tazama: Tayyib, Atyab al-Bayan, juz. 8, uk. 433.
  69. Surat Maryam: Aya ya 27.
  70. Husseini Hamdani, Anwar Derakhshan, 1405 H, juz. 10, uk. 374.
  71. Surat Maryam: Aya ya 28.
  72. Surat an-Nisaa: Aya ya 156>.
  73. Faidh Kashani, Tafsir al-Safi, juz. 3, uk. 279.
  74. Surat Maryam: Aya ya 29.
  75. Ja'fari, Tafsir Kauthar, 1376 S, juz. 6, uk. 513.
  76. Surat Maryam: Aya ya 28.
  77. Ja'fari, Tafsir Kauthar, 1376 S, juz. 6, uk. 513.
  78. Negahaye Qur'an Kareem wa Kitab Muqaddas be Maryam (s.a) Chegune ast?, Tovuti Islamquest.net.
  79. Puya, «Tavallud Masih (a.s) dar Qur'an wa Injil», uk. 5.
  80. Puya, «Tavallud Masih (a.s) dar Qur'an wa Injil», uk. 6.
  81. Bayabani Askui, «Tavallud Hazrat Masih dar Qur'an wa Ahd Jadid», uk. 35.
  82. Bayabani Askui, «Tavallud Hazrat Masih dar Qur'an wa Ahd Jadid», uk. 35.
  83. Bayabani Askui, «Tavallud Hazrat Masih dar Qur'an wa Ahd Jadid», uk. 35.

Vyanzo

  • Qur'an Kareem
  • Baidhawi, Abdullah bin Umar. Anwar al-Tanzil wa Asrar al-Ta'wil. Mhakiki: Muhammad Abdul rahman al-Mar'ashli. Beirut: Dar Ihya al-Turath al-Arabi, Chapa ya kwanza, 1418 HS.
  • Biyabani Askui, Muhammad, «Tavallud Hazrat Masih dar Qur'an wa Ahd Jadid». Dar Sahife Mubin, juz. 8, 1375 S.
  • Fadhlullah, Sayyid Muhammad Hussein. Tafsir min Wahyi al-Quran. Beirut: Dar al-Milak lit-Tabai wa an-Nashr, 1419 HS,
  • Faidh Kashani, Muhammad bin Shah-Murtadha. Tafsir al-Safi. Mhakiki: Hussein A'alami. Teheran: Intishar al-Sadr, 1415 HS.
  • Husseini Hamdani, Sayyid Muhammad Hussein. Anvar Derakhshan dar Tafsir Qur'an. Mhakiki: Muhammad Baqir Bahbudi. Tehran: Buniyad Daire al-maarif Islami, 1404 HS.
  • Ibnu Kathir, Ismail bin Omar. Tafsir al-Qur'an al-Adhim. Mhakiki: Sami bin Muhammad Salamah. Dar Tayibah li an-Nashr wa Tauzii', 1420 HS.
  • Ja'fari, Ya'qub. Tafsir Kauthar. Qom: Intisharat Hijrat, 1376 S.
  • Makarim Shirazi, Nashir. Tafsir Nemuneh. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiah, Chapa ya kwanza, 1398 HS.
  • Maqatil bin Suleiman. Tafsir Maqatil bin Suleiman. Mhakiki: Abdullah Mahmud Shahateh. Beirut: Dar Ihya al-Turath al-Arabi, 1423 HS,
  • Mudarrisi, Sayyid Muhammad Taqi. Min Huda al-Quran. Tehran: Dar Muhibbi al-Hussein, 1419 HS.
  • Mughniyah, Muhammad Jawad. Tafsir al-Kasyif. Tehran: Dar al-Kutub al-Islamiah, 1424 HS.
  • Najafi Khomeini, Muhammad Jawad. Tafsir Āsan. Tehran: Intisharat Islamiyyah, Chapa ya kwanza, 1398 HS.
  • Puya, Aa'dham. Tavallud Masih (a.s) dar Qur'an va Injil. Dar Sahife Fiqh wa Huquq Khanevadeh, juz. 6, Tabistan, 1376 S.
  • Sadiqi Tehrani, Muhammad. al-Balagh fi Tafsir a-Quran. Qom, 1419 HS.
  • Tovuti ya irna.ir. Bakrzai Inqilabi dar Danesh Taulid Mithli. Darje matalib: 5 Urdibehesht 1383 S, Tarikh bazdid: 14 Dey 1402 S.
  • Tovuti ya islamquest.net. Negahaye Qur'an Karim wa Kitab Muqaddas be Maryam (s.a) Cheguneh ast?.
  • Tovuti ya magirans.com. Tahqiq dar Maurid Bakrzai. Darje matalib: 14 Dey1402 S.
  • Shaibani, Muhammad bin Hassan. Nahj al-Bayan an Kashf Ma'ani al-Qur'an. Mhakiki: Hussein Dargahi. Tehran: Buniyad Daire al-Ma'arif Islami, 1413 HS.
  • Tabatabai, Sayyid Muhammad Hussein. al-Mizan fi Tafsir al-Quran. Qom: Daftar Intisharat Islami, 1417 HS.
  • Tabrasi, Fadhl bin Hassan. Majma'u al-Bayan fi Tafsir al-Qur'an. Mhakiki: Muhammad Jawad Balaghi. Tehran: Nashir Khusru, 1372 S.
  • Tahri-Niya, Ali & Zahrah Haidari, «Sakhtar Neshanehai Shahksiyat Hazrat Maryam dar Qur'an Karim». Dalam jurnal Mubin, juz. 15, Bahar, 1393 S.
  • Tayyib, Sayyid Abdul-Hussein. At-yab al-Bayan fi Tafsir al-Qur'an. Tehran: Intisharat Islam, 1378 S.
  • Tusi, Muhammad bin Hassan. al-Tibyan fi Tafsir al-Quran. Riset: Ahmad Habib al-'Amili. Beirut: Dar Ihya al-Turath al-Arabi.
  • Zuhaili, Wahbah bin Mustafa. Tafsir al-Wasit. Damascus: dar al-Fikr, 1422 HS.